Mkutano wa pili wa viongozi wakuu wa "Kundi la Nchi 77 pamoja na China" ulifunguliwa tarehe 15 mjini Doha, mji mkuu wa Qatar. Wajumbe kutoka nchi wanachama 131 wa kundi hilo pamoja na China walihudhuria mkutano huo. Ujumbe wa China unaongozwa na naibu waziri mkuu Zeng Peiyan.
Mada ya mkutano huo ni "kutimiza lengo la maendeleo ya milenia". Mkutano huo utakagua utekelezaji wa azimio na "programu ya Havana" iliyopitishwa katika mkutano wa kwanza uliofanyika mwaka 2000 na kuweka mpango wa ushirikiano wa kusini kusini na kufanya maandalizi ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu. Mkutano huo utafanyika kwa siku mbili na utakapomalizika utatoa "Taarifa ya Kisiasa" na "Programu ya Vitendo".
Katika mchakato wa utandawazi duniani nchi zinazoendelea zitawezaje kukabili changamoto, kusukuma maendeleo na kutatua matatizo ya umaskini na madeni ni swala linalofuatiliwa sana na nchi zinazohudhuria mkutano huo. Mjumbe wa nchi inayoandaa mkutano huo, Qatar, Bw. Khalifa Al-Thani kwenye ufunguzi alisema, kuimaisha ushirikiano wa kusini kusini ni hatua muhimu kwa nchi zinazoendelea kushiriki katika biashara ya kimataifa. Katika mchakato wa utandawazi duniani nchi za kusini zinastahili kunufaika katika mkakati wa maendeleo uliobuniwa na nchi hizo kutokana na hali zao zilivyo. Bw. Khalifa Al-Thani alitoa ushauri kuanzisha mfuko wa maendeleo ya nchi za kusini ili kuendeleza nchi wanachama wa kundi hilo kiuchumi, kijamii na kiafya, na kwamba Qatar ingependa kuchangia mfuko huo dola za Kimarekani milioni 20.
Waziri mkuu wa Jamaika, nchi mwenyekiti wa Kundi la Nchi 77, Bw. Percival Patterson alisema Kundi la Nchi 77 linapaswa kupambana na njaa, umaskini na maradhi. Alisema kuwa ushirikiano kati ya nchi za kusini haujafikia kiwango kilichotarajiwa na mkutano uliopita, nchi hizo zinapaswa kufanya juhudi kubwa zaidi. Kadhalika, alizitaka nchi zilizoendelea zitoe msaada wa dawa kwa nchi wanachama wa kundi hilo.
Waziri mkuu wa Malaysia Bw. Ahmad Badawi alisema, madeni ya nchi zinazoendelea yanakwamisha vibaya maendeleo, suala hilo lazima litatuliwe. Bw. Badawi alionesha furaha kwa kundi la nchi nane kusamehe madeni ya nchi maskini kabisa, na huku aliomba nchi tajiri zitoe misaada mingi zaidi kwa nchi maskini za kusini. Mjumbe wa Algeria alisema, nchi za kaskazini hazikuzingatia vya kutosha madeni ya nchi za kusini.
Naibu waziri mkuu wa China Zeng Peiyan kwenye mkutano alitoa mapendekezo manne: 1, kuimarisha mshikamano kati ya nchi za kusini, na kuchukuka hatua za pamoja katika masuala muhimu ya kimataifa na yanayohusu maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea, na zipiganie haki nyingi zaidi katika Umoja wa Mataifa na WTO. 2, kuimarisha kwa kina ushirikiano wa uchumi na teknolojia. Nchi zinazoendelea zinapaswa kufunguliana zaidi masoko na kusukuma biashara huria na kurahisisha urasimu wa kuwekeza, kupeana uzoefu na kupanua nyanja za ushirikiano. 3, kuimarisha uwezo wa kujitegemea. Nchi zinazoendelea zinapaswa kuchagua njia yake zenyewe kulingana na hali ilivyo ya taifa. 4, kuimarisha mazungumzo kati ya nchi za kaskazini na kusini na kusukuma nchi zilizoendelea zitilie maanani zaidi matakwa ya nchi zinazoendelea na kuimarisha maingiliano ya kiuchumi kati ya kaskazini na kusini.
Washiriki wa mkutano huo wote wanaona kuwa mkutano huo umetoa nafasi ya kusawazisha msimamo katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kusini kusini, kupanua maingiliano ya kibiashara, na utaweka msingi wa kupanua ushirikiano baina ya nchi hizo na China.
|