Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-16 20:22:48    
OPEC kuongeza uzalishaji wa mafuta kutaweza kupunguza bei ya mafuta?

cri

Mkutano maalum wa 136 wa mawaziri wa OPEC ulifanyika tarehe 15 huko Geneva, Uswisi, mkutano huo uliamua kuongeza kikomo cha uzalishaji wa mafuta kwa siku kufikia mapipa milioni 28 kutoka mapipa milioni 27.5 ya hivi sasa kuanzia tarehe 1 mwezi Julai mwaka huu, ili kupunguza bei kubwa ya mafuta kwenye soko la kimataifa. Lakini siku hiyo, bei ya kimataifa ya mafuta haikushuka bali iliongezeka zaidi. Kutokana na hali hiyo, inaonekana kuwa uamuzi wa OPEC kuongeza uzalishaji wa mafuta hauwezi kuondoa wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa kuhusu kuongezeka kwa bei ya mafuta.

Wachambuzi wanaona kuwa, hali hiyo inatokana na sababu zifuatazo:

Kwanza, jumuiya ya kimataifa bado ina mashaka kuhusu kama kweli OPEC inaweza kuongeza uzalishaji wa mafuta. Mwanzoni, OPEC kuweka kikomo cha uzalishaji wa mafuta kwa siku kulilenga kudhibiti bei ya kimataifa ya mafuta kupitia kurekebisha uzalishaji wa mafuta. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, uwezo wa OPEC kudhibiti soko la kimaitaifa umepungua sana. Hali hiyo inatokana na kuwa, nchi nyingi wanachama zinazalisha mafuta kwa kuvuka kikomo kwa ajili ya maslahi yao yenyewe. Hivyo OPEC kuongeza kikomo cha uzalishaji wa mafuta hakutasaidia vyovyote soko la kimataifa.

Pili, migongano iliyopo kati ya utoaji wa mafuta na usafishaji wa mafuta. OPEC iliainisha kwenye mkutano huo kuwa, ingawa mahitaji ya mafuta duniani yataongezeka zaidi katika robo ya nne ya mwaka huu, lakini hivi sasa utoaji wa mafuta kwenye soko la kimataifa bado yanatosha. Sababu kubwa kwa hali ya hivi sasa ni kwamba uwezo wa usafishaji wa mafuta hautoshi. Kutokana na hifadhi ya mazingira, Marekani haikujenga kiwanda hata kimoja cha kusafisha mafuta katika miaka 30 iliyopita, na Ulaya pia haikujenga kiwanda hata kimoja. Kutokana na faida ndogo za kiuchumi, viwanda vingi vya kusafisha mafuta vya Marekani vilitangaza kufungwa miaka zaidi ya kumi iliyopita, na hali hiyo imepanua zaidi pengo lililopo kati ya utoaji wa mafuta na uwezo wa usafishaji wa mafuta.

Aidha, akiba na mahitaji ya mafuta ya Marekani, ambayo ni nchi ya kwanza duniani kwa matumizi ya nishati, pia zinasababisha moja kwa moja kuongezeka kwa bei ya mafuta. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa tarehe 15 na wizara ya nishati ya Marekani, katika wiki iliyopita, akiba ya mafuta asili na dizeli ya Marekani imepungua kwa kiasi kikubwa kuliko iliyokadiriwa. Lakini, mahitaji ya mafuta yaliyosafishwa bado yanaongezeka.

Maoni ya umma yanaona kuwa, bei kubwa ya mafuta ya kimataifa itaweka athari mbaya kwa utulivu na maendeleo mazuri ya uchumi wa dunia. Na kutokana na hali ya hivi sasa, kupungua kwa bei ya kimaitaifa ya mafuta hakuwezi kutimizwa kwa OPEC peke yake kuongeza kikomo cha uzalishaji wa mafuta kwa siku, bali kunahitaji juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-16