Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-17 20:28:57    
Iraq yapiga hatua muhimu katika mchakato wa utungaji wa katiba

cri

Kiongozi wa pili wa Chama cha Dawa cha Kiislamu cha Iraq kinachoongozwa na waziri mkuu wa serikali ya mpito Bw. Ibrahim al-Jaafari, ambaye pia ni mjumbe wa Tume ya utungaji wa katiba ya Iraq Bw. Jawad al-Maliky tarehe 16 alitangaza kuwa, tume ya utungaji wa katiba imeamua kukubali kuongeza wajumbe 25 wa madhehebu ya Suni katika tume hiyo. Wachambuzi walisema kuwa, hii ni hatua muhimu ya makundi mbalimbali nchini Iraq kusukuma mbele mchakato wa utungaji wa katiba.

Uamuzi huo ni maafikiano kati ya makundi mbalimbali baada ya kufanya majadiliano. Miongoni mwa wajumbe hao 25, wajumbe 15 ni wajumbe rasmi, na wengine 10 ni washauri. Wiki ijayo madhehebu ya Suni yatatoa orodha ya wajumbe wapya na kuiwasilisha kwenye tume ya utungaji wa katiba. Bunge la Iraq litatoa taarifa likikubali kupanuliwa kwa tume hiyo.

Tume ya utungaji wa katiba ya Iraq yenye wabunge 55 iliundwa tarehe 10 mwezi Mei. Kutokana na madhehebu ya Suni kususia kuipinga uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Januari mwaka huu, madhehebu hayo yalichukua viti 17 tu miongoni mwa viti 275 katika bunge la mpito, na wabunge wawili tu waliingia katika tume ya utungaji wa sheria, hivyo kwa ujumla madhehebu hayo hayashiriki kwenye mchakato wa utungaji wa katiba. Madhehebu ya Suni hayaridhiki na hali hiyo. Tarehe 8 mwezi huu mkutano wa wananchi wa madhehebu ya Suni uliohudhuriwa na makundi mbalimbali ya madhehebu hayo ulitoa ombi la kuongeza wajumbe wa madhehebu hayo kufikia 25 katika tume ya utungaji wa katiba, na kusema kuwa kama ombi hilo halitatimizwa, madhehebu ya Suni huenda yatapinga upigaji kura wa raia wote kuhusu mswada wa katiba. Rais Jalal Talabani wa Iraq tarehe 9 alikubali kikanuni ombi hilo, lakini Waislamu wa madhehebu ya Shia na wabunge wa Wakurd wana maoni tofauti kuhusu jambo hilo. Baada ya majadiliano ya siku kadhaa, tarehe 16 pande mbalimbali ziliafikiana kuhusu suala hilo.

Wachambuzi wanaona kuwa, serikali ya Iraq iliafikiana na madhehebu ya Suni kutokana na sababu kadhaa. Kwanza, hivi karibuni migogoro mingi ilitokea nchini humo, na polisi, wananchi na askari wa Marekani wengi walijeruhiwa au kuuawa. Tarehe 15 watu zaidi ya 50 waliuawa katika migogoro, na siku hiyo ilikuwa siku ambapo kuna watu wengi zaidi waliojeruhiwa au kuuawa katika wiki 3 zilizopita. Makundi ya watu wenye silaha ambayo mengi yao ni ya madhehebu ya Suni kuanzisha migogoro hiyo kunahusiana na madhehebu hayo kutoshiriki kwenye mchakato wa ukarabati wa kisiasa. Ili kuyataka makundi hayo yasianzishe tena migogoro, inaibidi serikali ijali zaidi maslahi ya kisasa ya madhehebu ya Suni, na kuafikiana na madhehebu hayo kuhusu mchakato wa kisiasa.

Pili, mchakato wa ukarabati wa kisiasa wa Iraq umeingia katika kipindi muhimu, upigaji kura wa watu wote kuhusu mswada wa katiba na uchaguzi mkuu utafanyika mwaka huu. Mswada wa katiba utakaomalizika tarehe 15 mwezi Agosti ukipitishwa kwenye upigaji kura wa watu wote utakaofanyika mwezi Oktoba, utaweka msingi kwa uchaguzi mkuu ili ufanyike kwa wakati mwezi Desemba. Pande mbalimbali zimetambua umuhimu wa Waarabu wa madhehebu ya Suni kushiriki kwenye utungaji wa katiba. Kutokana na katiba ya muda, kama theluthi mbili ya wapiga kura katika mikoa mitatu miongoni mwa mikoa 18 wakipinga mswada wa katiba, mswada huo hautapitishwa. Hivi sasa idadi ya watu wa madhehebu ya Suni ni kubwa zaidi katika mikoa isiyopungua mitatu, hivyo madhehebu hayo yana uwezo wa kuipinga mswada huo. Lakini mswada huo ukikataliwa, bunge litavunjwa, uchaguzi mkuu utafanyika tena, na mchakato wa kisiasa utarudishwa. Serikali ya Iraq bila shaka haitaki mambo hayo kutokea.

Tatu, ili kuifanya Iraq iwe mfano wa demokrasia katika Mashariki ya Kati, Marekani inataka mchakato wa ukarabati wa kisiasa wa Iraq uendelee kwa mafanikio. Mchakato huo ukikabiliana na vikwazo vikubwa, Marekani itazidi kusumbuliwa na suala la Iraq, na siku ya askari laki kadhaa wa Marekani kuondoka kutoka Iraq itakuwa mbali zaidi, hivyo Marekani pia iliishinikiza serikali ya Iraq kuishirikisha madhehebu ya Suni katika mchakato wa utungaji wa katiba, ili kuhakikisha kuwa mchakato huo unaaminika na utafanikiwa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-17