Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-17 20:12:23    
Mkutano muhimu wa kuongeza ushirikiano na maendeleo kati ya kusini na kusini

cri

Mkutano wa pili wa wakuu wa kusini wa "kundi la nchi 77 pamoja na China" ulifungwa tarehe 16 huko Doha, mji mkuu wa Qatar, mkutano huo umepitisha "Taarifa ya Doha" na "Mpango wa utekelezaji wa Doha", na watu waliohudhuria mkutano huo wametoa mwito kwa kauli moja kuzitaka nchi zinazoendelea ziimarishe ushirikiano na kutafuta maendeleo kwa pamoja.

"Taarifa ya Doha" na "Mpango wa utekelezaji wa Doha" vimefanya uchambuzi wa kina juu ya madeni ya nje yanayobebwa na nchi zinazoendelea, masuala ya umaskini na utandawazi wa uchumi duniani yanayozikabili, na vimesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya kusini na kusini katika mwelekeo wa utandawazi wa uchumi duniani, na kutoa mapendekezo halisi kuhusu nchi zilizohudhuria mkutano jinsi zitakavyoongeza zaidi ushirikiano katika miaka minne ijayo.

Mkutano huo ulifanyika kwa siku mbili, nchi wanachama 131 wa kundi la nchi 77 walituma ujumbe kuhudhuria mkutano huo, naibu waziri mkuu wa China Bwana Zeng Peiyan aliongoza ujumbe wa China kuhudhuria mkutano huo.

Baada ya majadiliano ya siku mbili, viongozi wa nchi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wanaona kuwa, utandawazi wa uchumi duniani ni changamoto inayozikabili nchi zote zinazoendelea, nchi zinazoendelea zinapaswa kutunga mikakati yao ya maendeleo kwa kufuata hali zao halisi, kufanya juhudi kuondokana na umaskini na kuimarisha marekebisho ya udhibiti wa uchumi katika mchakato wa maendeleo ya uchumi wao; wakati huo huo nchi za kusini zinapaswa kuimarisha ushirikiano hasa ushirikiano katika sekta ya uchumi na biashara.

Wajumbe waliohudhuria mkutano huo pia wametoa hatua halisi kuhusu namna ya kuzidisha ushirikiano kati ya kusini na kusini, hatua hizo ni pamoja na kuanzisha mfuko wa maendeleo ya kusini, ambapo Qatar, China na India zitatoa michango kwa mfuko huo; kuanzisha sehemu za biashara huria kati ya nchi zinazoendelea, kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi katika sekta za fedha; kuanzisha duru la tatu la mazungumzo kuhusu "utaratibu wa kutoa kipaumbele wa biashara duniani wa nchi zinazoendelea; kuunga mkono uendelezaji wa mashirika madogo na ya wastani, na kuwahamasisha watu binafsi kuwekeza vitega uchumi na kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu.

Viongozi waliohudhuria mkutano huo wameridhika na mafanikio yaliyopatikana katika siku zilizopita. Pia wameona kuwa nchi za kusini zikitaka kupata mafanikio makubwa zaidi katika ushirikiano kati ya kusini na kusini zinapaswa kufanya juhudi kubwa katika kutekeleza taarifa ya mkutano wa kwanza wa wakuu wa kusini wa mwaka 2000 na "Mpango wa utekelezaji wa Havana" pamoja na maoni ya pamoja yaliyofikiwa kwenye mkutano wa safari hii.

Wajumbe waliohudhuria mkutano huo pia wanazitaka nchi zilizoendelea kiviwanda za kaskazini ziongeze misaada yao kwa maendeleo ya nchi za kusini, kama vile kupunguza madeni ya nchi maskini ya kusini, kubeba jukumu la kuyasaidia maendeleo ya nchi za kusini bila kuweka sharti lolote la kisiasa, na kuondoa vizuizi vya kibiashara dhidi ya nchi zinazoendelea.

Viongozi waliohudhuria mkutano huo pia wameona kuwa, nchi za kusini zinapaswa kuongeza mshikamano, kujitahidi kuchukua vitendo vya pamoja katika mambo makubwa ya kimataifa na masuala yanayohusika na maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea, kushiriki zaidi shughuli za Umoja wa Mataifa, shirika la WTO na jumuiya nyingine za kimataifa, na kutoa sauti na kuongeza athari katika jumuiya hizo.

Vyombo vya habari vinaona kuwa, mkutano huo ni mwanzo mpya wa ushirikiano wa kusini na kusini, maoni ya pamoja yaliyofikiwa kwenye mkutano huo yatahimiza zaidi ushirikiano kati ya kusini na kusini, na kuhimiza mazungumzo kati ya kusini na kaskazini, kusawazisha misimamo ya nchi za kusini kuhusu masuala makubwa ya kimataifa pia kuongeza zaidi athari mkutano huo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-17