Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-21 16:23:44    
Barua 0621

cri
      Msikilizaji wetu Benjamin Wachie Binale ambaye barua zake huhifadhiwa na Bob Morgan Services LTD sanduku la posta 21606 Nairobi Kenya, ametuletea barua akisema kuwa, ni furaha kuu kwake kupata fursa hii ya kuwasiliana nasi kupitia njia hii ya barua. Mwanzo kabisa anasema angependa kutupa pongezi nyingi sana kwa kazi yetu nzuri tunayoifanya. Yeye amekuwa akisikiliza vipindi vyetu vinavyowafikia kupitia idhaa ya Kiswahili ya KBC kuanzia saa 11 kamili hadi saa 11na nusu. Ama kwa hakika amekuwa akitafuta njia hiyo rahisi kuwasiliana nasi bila mafanikio.

Anasema Alibahatika kukutana na Bw Xavier Telly Wambwa na kuweza kukaa naye hapo jijini Nairobi hadi alipokuja nchini China, na aliporudi akamletea zawadi na kumpa bahasha iliyolipiwa ili aweze kuwasiliana nasi. Atashukuru sana tukimtumia kadi za salamu na habari zote ambazo tutamruhusu kujua kuhusu hii idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa.

Kwa kweli anayotueleza msikilizaji wetu huyo mpya Benjamin Wachie Binale hatukuyatarajia, tunamshukuru na kumpongeza Bwana Telly Wambwa kwa juhudi zake za kutusaidia kuwafahamisha wasikilizaji wetu na marafiki zake hali ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Ni matumaini yetu kuwa msikilizaji wetu huyo ataendelea kusikiliza vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo yake.

Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161 Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, yeye huko Shinyanga hajambo kabisa anaendelea na shughuli za kila siku za ujenzi wa taifa la Tanzania, bila kusahau kusikiliza matangazo na vipindi vya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa inayotangaza moja kwa moja kutoka Beijing China na pia kupitia Radio KBC Nairobi Kenya.

Anasema alivutiwa sana na kipindi cha Tazama China kilichoelezea mambo mbalimbali yaliyopo katika mji wa Beijing ikiwa ni pamoja na mji wa Xian mkoani Shanxi ambayo Alibahatika kuitembelea akiwa hapa China. Anasema ni ukweli usiopingika kwamba mtu anapofika Beijing au Xian anakuwa kama amefika mbinguni. Ni miji inayovutia kweli kweli yenye mvuto siyo tu kwa wageni waliofika, bali pia hata kwa wachina wenyewe.

Mji wa Beijing ambao ulichaguliwa na kamati ya olimpiki ya kimataifa kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, una sifa na hadhi zote na miundo mbinu ya hali ya juu inayostahili, hakika ni mji unaovutia sana na wenye heshima zote.

Kwa sababu hii anawapongeza sana wakazi wa mji wa Beijing na wachina wote kwa mafanikio makubwa waliyofikia kustawisha na kuendeleza miji yao ikiwemo Beijing, Tianjin, Xian na Shanghai.

Msikilizaji wetu Bi.Minza S. Kasili wa sanduku la posta 161 Bariadi Shinyanga Tanzania anasema katika barua yake kuwa, anafurahi sana kuandika barua hii akitusalimia kwa njia ya waraka huu. Vipindi vyetu wanavisikiliza sana na kuwaalika pia marafiki zao wasikilize Radio China kimataifa. Madhumuni makubwa yake ya kuandika barua hii ni kutupongeza kwa kazi yetu nzuri, pia anataka tumtumie jarida la Daraja la Urafiki kama tayari limechapishwa na pia magazeti mengine ya picha na filamu. Atashukuru sana, na anataka kuwasalimia wachina wote wanaofahamu lugha ya kiswahili.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-21