Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-23 14:23:30    
Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Iraq waunga mkono mchakato wa ukarabati wa Iraq

cri

Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Iraq tarehe 22 ulifanyika katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya yaliyoko Brussels, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zaidi ya 80 akiwemo Bw. Li Zhaoxing wa China na wajumbe kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Muungano wa Nchi za Kiarabu, NATO na benki ya dunia walihudhuria mkutano huo wa siku moja.

Ajenda ya mkutano huo ni mchakato wa ukarabati, ujenzi mpya wa kiuchumi na ujenzi wa kisheria nchini Iraq. Taarifa iliyotolewa na mkutano huo imeahidi kuendelea kusaidia mchakato wa ujenzi mpya wa Iraq wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini haikutaja hatua halisi za kutekeleza ahadi hizo.

Taarifa hiyo inazitaka nchi husika zitekeleze ahadi zao za kusamehe madeni ya Iraq na kukaribisha nchi zinazodai madeni ziendelee kupunguza au kufuta madeni ya Iraq kwa masharti nafuu. Kadhalika, taarifa pia inataka nchi husika zitekeleze ahadi zao na kukaribisha jumuyia ya kimataifa iendelee kutoa misaada ya fedha. Taarifa imeitaka serikali ya mpito ya Iraq itoe maombi halisi ili yajadiliwe katika mkutano wa nne wa kuchangisha fedha utakaofanyika Amman, mji mkuu wa Jordan, mwezi ujao.

Ujumbe wa Iraq ulioongozwa na waziri mkuu wa serikali ya mpito Bw. Ibrahim al-Jaafari ulihudhuria mkutano huo. Kwenye mkutano, waziri wa mambo ya nje wa Iraq Bw. Hoshyar Zebari alitoa kazi nne muhimu katika mambo ya nje ya Iraq, nazo ni kukamilisha mchakato wa mageuzi ya kisiasa kwa mujibu wa tarehe iliyowekwa katika azimio la Baraza la Uslama la Umoja wa Mataifa Nam. 1546; kuhakikisha utulivu wa jamii kwa kusaidiwa na jumuyia ya kimataifa; kujitahidi kupata misaada ya jumuyia ya kimataifa katika mambo ya fedha, kuandaa na kufundisha wataalamu teknolojia; kuhimiza jumuyia ya kimataifa itambue tena Iraq kama ni nchi ya kawaida katika maingiliano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mikutano ya kimataifa na kuweka mikataba ya kimataifa.

Kwenye mkutano, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alihimiza jumuyia ya kimataifa iheshimu ahadi zao na kuzitekeleza kwa vitendo ili kuisaidia Iraq ijengwe upya. Alisema, watu wa Iraq wanaona mkutano huo kama ni ahadi ya jumuyia ya kimataifa kukabiliana na changamoto pamoja nao. Mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa Luxembourg Bw. Jean Asselborn aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano akisema ujenzi mpya wa Iraq unakabiliwa na changamoto nyingi, na alisema lengo la mkutano huo ni kutaka kuwaambia watu wa Iraq kwamba katika wakati huu mgumu wa mpito "sisi tunasimama pamoja nao: Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice alisema kuwa serikali ya mpito ya Iraq inapaswa kufanya juhudi za kuboresha hali ya usalama na maendeleo ya uchumi. Alisisitiza kuwa jumuyia ya kimataifa inapaswa kusaidia Iraq kupambana na magaidi humu nchini Iraq.

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing alieleza msimamo wa serikali ya China kuhusu suala la Iraq, alitoa mapendekezo matatu yakiwemo "nchi Iraq itawaliwe na watu wa Iraq wenyewe", na katika uratibu wa mambo ya taifa na ujenzi wa uchumi kuifanya Iraq iwe na uwezo wa kujiendeleza, na alisema kuwa China itaendelea kufanya juhudi katika mchakato wa ujenzi mpya wa Iraq kwa pamoja na jumuyia ya kimataifa.

Vyombo vya habari vinaona kuwa mkutano huo ulifanywa kwa lengo hasa la kusawazisha misimamo na vitendo vya jumuyia ya kimataifa katika suala la ujenzi mpya wa Iraq, na ni maandalizi ya mkutano wa kuchangisha fedha utakaofanyika mwezi ujao mjini Amman.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-23