Mkutano wa 15 wa mawaziri wa Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini ulimalizika tarehe 23 mjini Soeul. Baada ya kuanzisha tena mazungumzo yaliyosimamishwa kwa miezi kumi, mkutano huo ulipata maendeleo makubwa, na umesukuma mbele mchakato wa maafikiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Kwenye mkutano muhimu uliofanyika mwaka 2000, wakuu wa Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini walifikia makubaliano ya kimsingi ya kutimiza muungano wa amani kwa kujitegemea. Ili kutimiza maafikiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, serikali ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini zilianzisha hatua kwa hatua utaratibu kamili wa mazungumzo kuhusu siasa, uchumi na majeshi, na mkutano wa mawaziri unafanya kazi muhimu katika utaratibu huo. Mwezi Julai mwaka jana, kutokana na mabadiliko ya hali ndani na nje ya Peninisula ya Korea, mazungumzo kati ya serikali hizo mbili yalisimamishwa. Kwenye mkutano wa manabu mawaziri uliofanyika mwezi Mei mwaka huu, pande mbili zilipata maoni ya pamoja kuhusu kuanzisha tena mazungumzo. Baadaye kwenye maadhimisho ya kusherehekea miaka mitano tangu mkutano wa wakuu wa Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini ulipofanyika mjini Pyongyang, kiongozi wa Korea ya Kaskazini Bw. Kim Jong-il alikutana na waziri wa muungano wa Korea ya Kusini Bw. Chung Dong Young, na pande mbili zilipata maoni ya pamoja kuhusu kuendelea kusukuma mbele maafikiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Katika hali hiyo, maendeleo yaliyopatikana kwenye mazungumzo ya mawaziri yanafuatiliwa sana na nchi za nje.
Kwanza, mazungumzo hayo yameonesha kuwa pande mbili zimerejesha kikamilifu utaratibu wa sasa wa mazungumzo kati yao, yakiwemo mazungumzo ya mawaziri, mazungumzo kati ya vyama vya msalaba mwekundu, mazungumzo ya kamati ya kusukuma mbele ushirikiano wa kiuchumi, na mazungumzo ya majenerali.
Pili, maendeleo mapya yamepatikana kwenye mazungumzo hayo. Pande mbili zimeamua kuanzisha mazungumo ya manaibu mawaziri kuhusu ushirikiano wa kilimo, kuanzisha mazungumo kuhusu sekta ya uvuvi, kujadili masuala halisi likiwemo kupanga sehemu ya pamoja ya uvuvi; pande mbili zimekubali kujadili suala la kuthibitisha watu waliopotea vitani kama walikufa au la kwenye mazungumzo ya vyama vya msalaba mwekundu, kufanya majaribio ya mkutano wa jamaa zilizotengana. Hivyo maoni ya pamoja ya mkutano huo wa mawaziri yameweka msingi mpya kwa mawasiliano na ushirikiano kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini.
Aidha, mkutano huo pia umetoa ishara nzuri kuhusu suala la nyuklia la Peninsula ya Korea. Kwenye taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo, pande mbili zilisema kuwa kutokuwa na silaha za nyuklia katika Peninsula ya Korea ni lengo la mwisho, na kukubali kutatua suala hilo kwa mazungumzo ya amani.
Wachambuzi wanaona kuwa, wakati ambapo mustakabali wa suala la nyuklia la Peninsula ya Korea na mazungumzo ya pande sita yanayohusika na suala hilo bado haujulikani, ni muhimu sasa kwa Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini kupata maoni hayo ya pamoja. Kwanza, baada ya kiongozi wa Korea ya Kaskazini Bw. Kim Jong-il tarehe 17 kusema kuwa kutokuwa na silaha za nyuklia kwenye Peninsula ya Korea ni mafundisho ya hayati mwenyekiti Kim il Sung, Korea ya Kaskazini ilieleza tena msimamo huo kwenye mazungumzo ya mawaziri. Pili, ni vizuri kwa pande mbili kufanya mazungumzo ya kirafiki kuhusu suala la nyuklia la Peninsula ya Korea, na kusema kuwa zinapenda kuchukua hatua halisi kusukuma mbele mazungumzo kuhusu suala hilo. Hivi sasa Bw. Kim Jong-il alisema kuwa, kama Marekani ikaikiri na kuiheshimu wazi Korea ya Kaskazini, Korea ya Kaskazini inatazamiwa kushiriki tena kwenye mazungumzo ya pande sita mwezi Julai. Kwenye mazungumzo ya mawaziri, Korea ya Kaskazini ilisisitiza tena msimamo wake wa amani, na hii ni ishara nzuri ya kufanya tena mkutano wa pande sita.
Jitihada zilizofanyika kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini zimefuatiliwa na pande nyingine za mazungumzo ya pande sita. Wachambuzi wanaona kuwa, pande husika zikiendelea kuonesha udhati wao na kutumia fursa nzuri, mazungumzo ya pande sita yatafanyika tena mapema.
Idhaa ya Kiswahili 2005-06-24
|