Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-24 21:08:04    
Mafanikio makubwa yapatikana katika ushirikiano kati ya China na shirika la SOS la kimataifa

cri

Mwaka huu ni miaka 20 tangu China na shirika la SOS la kimataifa zilipoanzisha ushirikiano wa kirafiki. Kwenye sherehe iliyofanyika tarehe 23 mjini Tianjin, China, mwenyekiti wa shirika hilo Bw.Helmut Kutin alisifu sana maendeleo ya vijiji vya SOS vya China. Alieleza matumaini yake kuwa shirika hilo nqa serikali ya China zitajitahidi kwa pamoja kujenga vijiji vyingi vya SOS nchini China, ili kuwawezesha watoto yatima wengi zaidi wakue kwa afya.

SOS ni shirika la hisani la kimataifa lenye makao yake makuu mjini Vienna, Austria. Shirika hilo limeweka vijiji vya SOS vipatavyo 440 katika nchi na sehemu zaidi ya 130. Kazi ya vijiji vya SOS ni kuwalea watoto yatima na kuwatunza kwa njia ya familia. Kila kijiji cha SOS kina familia zaidi ya kumi na kila familia inawalea watoto yatima sita hadi wanane wa kiume na kike na kumwalika mwanamke asiyeolewa na kutokuwa na mtoto awe mama wa familia hiyo.

Mwaka 1985, kundi la kwanza la vijiji vya SOS vilijengwa mjini Tianjin na mjini Yantai, mkoani Shandong, China. Katika miaka 20 iliyopita, kutokana na jitihida za serikali ya China na shirika la SOS la kimataifa, vijiji vya SOS vya China vimeendelezwa. Naibu waziri wa mambo ya raia Bw. Li Liguo alisema:

"Kwa kushirikiana barabara kwa pande hizo mbili, hadi hivi leo, vijiji 9 vya SOS, shule mbili na shule 9 za chekechea zimejengwa. Vijiji hivyo vimewalea watoto yatima 1500".

Habari zinasema kuwa ili kujenga vijiji vya SOS nchini China, shirika la SOS la kimatifa limegharamia Yuan za Renminbi zaidi ya milioni mia tatu. Katika mchakato wa ujenzi wa vijiji hivyo, wizara ya mambo ya raia ya serikali za miji viliyoko vijiji hivyo pia imetoa misaada mikubwa.

Msichana Liu Ling mwenye umri wa miaka 20 alipokuwa na umri wa miaka minne, mama yake alifariki kwenye ajali ya gari na baba yake pia alikufa kwa ugonjwa alipokuwa na umri wa miaka 9. Hivyo Liu Ling alilelewa na kijiji cha SOS kilichoko mjini Qiqihar, mkoani Heilongjiang. Sasa amekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha teknolojia. Alipokumbusha maisha yake katika kijiji cha SOS alisema:

"Mazingira ya kijiji cha SOS ni mazuri. Mama yangu mpya alininunulia nguo na mfuko wa vitabu. Mama yangu pia alinifahamisha lengo na maana ya maisha na nimekuwa na maadili mema na tabia nzuri ya maisha hatua kwa hatua".

Kutokana na takwimu, kati ya watoto yatima waliolelewa katika vijiji vya SOS nchini China, watoto mia tatu wamekuwa watu wazima na kufanya kazi au kusoma katika shule mbalimbali.

Maendeleo ya vijiji vya SOS nchini China yalisifiwa sana na shirika la SOS la kimataifa. Mwenyekiti wa shirikl hilo Helmut Kutin alisema kwenye sherehe iliyofanyika tarehe 23:

"Najivunia ushirikiano mzuri kati ya serikali ya China na SOS. Kutokana na jitihada za pamoja kwa mama na wafanyakazi wote, watoto waliopoteza familia wamekuwa na familia mpya. Natumai kuwa vijiji vingi zaidi vitajengwa nchini China na kuwawezesha watoto wengi wakue kwa afya".

Naibu waziri Bw. Li Liguo alidokeza kuwa kijiji cha kumi cha SOS cha China kiko mbioni kujengwa mjini Beijing na kitakamilika mwakani.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-24