Mkutano wa sita wa mawaziri wa fedha wa Asia na Ulaya ulifanyika tarehe 26 mjini Tianjin, China. Mkutano huo ulilenga kuzidisha ushirikiano wa mambo ya fedha kati ya Asia na Ulaya na kuhimiza uhusiano wa uchumi na biashara uwe mzuri zaidi. Waziri mkuu wa China Wen Jiabao Alipohutubia sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo alieleza kuwa katika hali mpya ya kimataifa, Asia na Ulaya zinapaswa kuendeleza zaidi uhusiano kati yao, na China itatoa mchango muhimu katika kuhimiza ushirikiano huo.
Mkutano wa mawaziri wa fedha wa Asia na Ulaya ulianzishwa mwaka 1996, ambao madhumuni yake ni kutekeleza kwa vitendo uamuzi na moyo wa mkutano wa wakuu wa Asia na Ulaya kuhusu mambo ya fedha na kuhimiza ushirikiano kati ya Asia na Ulaya katika uchumi na fedha. Hii ni mara ya kwanza kwa China kuandaa mkutano huo ikiwa nchi mwenyekiti. Mawaziri wa fedha wa nchi wanachama 39 za mkutano wa Asia na Ulaya pamoja na maofisa waandamizi wa mfuko wa kimataifa, benki ya dunia na jumuiya nyingine za kimataifa walihudhuria mkutano huo.
Kwenye mkutano huo, waziri mkuu Wen Jiabao alieleza kuwa ongezeko tulivu la uchumi wa Asia na Ulaya ni msukumo mkuu wa kudumisha na kuhimiza ongezeko la uchumi wa dunia. Alisema kuwa pande mbili za Asia na Ulaya zinapaswa kuimarisha ushirikiano na maingiliano katika sera ya uchumi wa jumla, ushirikiano wa kikanda na mageuzi ya fedha na kuendeleza zaidi ushirikiano wa fedha kati ya Asia na Ulaya. Wen Jiabao alisema:
"Asia ni sehemu yenye uhai mkubwa kabisa wa uchumi duniani kwa hivi leo na Muungano wa Ulaya ni jumuiya ya uchumi iliyoendelea kabisa duniani. Mustakbali wa ushirikiano wa kunufaishana kati yao ni mkubwa sana. Baada ya kupanuliwa kwa mkutano wa Asia na Ulaya, idadi ya watu wa nchi wanachama za mkutano huo inachukua asilimia 40 ya idadi nzima ya dunia na jumla ya thamani ya pato la nchi hizo ni nusu ya ile ya dunia nzima na utafanya kazi kubwa zaidi katika mambo ya kimataifa".
Bw. Wen Jiabao alisema kuwa mwaka 2001, China iliyokuwa nchi mwenyekiti wa jumuiya ya ushirikiano wa uchumi wa Asia na Pasifiki, ilipendekeza kuanzisha miradi ya fedha na maendeleo ya jumuiya hiyo. Mwaka 2004, China ilianzisha mazungumzo yasiyo rasmi ya mawaziri wa China na kikundi cha nchi saba. Mwaka huu, China imekuwa nchi mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri wa fedha wa Asia na Ulaya na mkutano wa mawaziri wa fedha wa kikundi cha nchi 20 na wakuu wa benki kuu za nchi hizo. Wen Jiabao alisema:
"Ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na nchi mbalimbali za Asia na Ulaya umeingia kwenye kipindi kipya. China imekuwa nguvu yenye juhudi katika maendeleo ya Asia, Ulaya na dunia".
Waziri mkuu Wen Jiabao alieleza kuwa katika siku za usoni, serikali ya China itaendelea kuchukua hatua za kudumisha maendeleo tulivu ya uchumi. Wakati huo huo, China itajitahidi kuimarisha ushirikiano na nchi mbalimbali za Asia na Ulaya, kupambana kwa pamoja na changamoto zinazokabili uchumi wa dunia, kuhimiza utulivu na ustawi wa ukanda huo na kuhimiza amani na maendeleo ya dunia.
Mkutano wa tarehe 26 pia ulitoa "pendekezo la Tianjin" linalohimiza ushirikiano mkubwa zaidi kati ya Asia na Ulaya katika mambo ya fedha.
Idhaa ya kiswahili 2005-06-27
|