Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-27 16:36:35    
Mchora picha wa Taiwan Kang Yaonan

cri

Bw. Kang Yaonan ni mtu mwenye furaha na ni hodari wa kuongea, alivaa shati jeupe na suruali ya kubana, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mada ya maonesho yake ni "Kupambana na UKIMWI na Kuishi Salama". Picha zilizooneshwa, zote ni majagi ya maua, ambazo alizichora miaka kadhaa ya karibuni. Alipoulizwa kwa nini zote ni picha za majagi ya maua? Alieleza kuwa, jagi la maua ni pambo la maisha, na ni alama ya maisha tulivu na salama. Alisema,

"Salama ni baraka, natumai watu watajisikia salama kwa kuangalia jagi langu la maua, na natumai zaidi kwamba maonesho yangu yatakuwa kama ni kichocheo cha kuyafanya mashirika, hasa kampuni za biashara zishiriki katika juhudi za kuwasaidia wagonjwa wa UKIMWI."

Ndani ya ukumbi, picha za majagi ya aina mbalimbali ziliwavutia watazamaji na kuwafanya waziangalie kwa muda mrefu. Kuna aina za kisasa za majagi yaliyochorwa na aina za kale za majagi ya China, na maumbo ni ya aina nyingi kama ya tunguri, na mwili wa binadamu. Rangi mbalimbali zilizotumika kwa usanii mkubwa zilisaidiana na kufanya kila jagi lipendeze sana.

Bw. Kang Yaonan ana umri wa miaka 43, baada kuhitimu chuo kikuu aliajiriwa katika shirika moja, lakini kutokana na kuwa na tabia ya kukaa peke yake, alishindwa kuishi maisha ya kikazi yaliyo sawa kila siku kwa saa maalumu, mwishowe alipokuwa na umri wa miaka 30 alifanya uamuzi wa kuacha kazi, ingawa wazazi wake walimpinga sana, lakini yeye alianza kuchora picha. Uamuzi wake huo ulikuwa ni ujasiri kwake yeye, ambaye hakuwahi kufundishwa uchoraji. Lakini Bw. Kang Yaonan aliona kuwa ni kuchora picha tu ndiyo kazi anayoipenda na ni picha tu ndio zinaweza kueleza hisia zilizo moyoni mwake.

Bw. Kang Yaonan ni mtu mwenye kipaji cha uchoraji ingawa hakuwahi kufundishwa. Kutokana na mazoezi ya kuchora picha nyingi na kujifunza mwenyewe, amekuwa mchoraji mkubwa mwenye mtindo wake pekee. Alisema,

"Naona kuchora picha ni limbikizo la uzoefu wa maisha, chochote unachopenda usiache kuchora. Hadi sasa hamu yangu ya kuchora vitu haijakauka. Mimi sikufundishwa katika chuo kikuu, kwa hiyo sina miiko mingi katika uchoraji wangu. Kila nilipomaliza picha moja hujipatia elimu fulani na kuifanya picha iwe nzuri kwa kiasi fulani kuliko iliyotangulia, ama sivyo haina maana ya kuchora."

Bw. Kang Yaonan alisema, kuchora picha sio tu kumemfanya afanikiwe katika kazi, bali pia kumembadilisha tabia yake ya kuishi na upweke na jakamoyo. Bw. Kang Yaonan alipokuwa mtoto mdogo alikuwa na ugonjwa wa pumu, afya yake ilikuwa sio nzuri, na mama yake alifariki mapema, yeye alikuwa mtu wa kukosa furaha. Tokea alipoanza kuchora picha alijaribu kuondoa simanzi na upweke moyoni mwake, na alijitahidi kuwasaidia watu kama yeye. Miaka hadi miaka tabia yake imebadilika na moyo wake umekuwa mchangamfu. Bw. Kang Yaonan anaona kuwa kuwasaidia wengine ndio kujisaidia mwenyewe. Aliwahi kujifunza nadharia ya tiba ya saikolojia kwa sanaa na aliwahi kufundisha madarasa ya saikolojia katika gereza la wafungwa wa kike. Alisema,

"Sanaa ikiwa ni kitu binafsi cha msanii, basi sanaa hiyo haina tofauti na shajara yake, lakini kama sanaa hiyo ikiwa na maana ya kijamii basi kazi yake ni kubwa, na ikiweza kusaidia watu wa aina fulani basi nishati ya sanaa hiyo itakuwa kubwa zaidi."

Mwezi Agosti mwaka jana, kwa bahati alifuatana na watu wengine kwenda hospitali moja ya wagonjwa wa UKIMWI mkoani Hebei, alisikia vibaya rohoni mwake alipoona wagonjwa wakielemewa shinikizo kubwa la kimawazo na kiafya, wakati huo alijiwa na mawazo ya kubadilishia mazingira yao na kuwafanya wawe wachangamfu. Aliwapeleka kwenye "kijiji cha wasanii" mjini Beijing kuwatembeza na kuwafahamisha kila kitu cha sanaa chenye maana ya undani.

Bw. Kang Yaonan alitumia muda mwingi na akili nyingi kuwasaidia wagonjwa wa UKIMWI wapate ahueni kisaikolojia. Maonesho ya picha zake aliyofanya mjini Beijing, ni moja ya hisani zake, kwamba atachangia mfuko wa wagonjwa wa zinaa na UKIMWI kwa pesa alizouza picha zake baada ya maonesho. Alisema, uwezo wa mtu mmoja ni mdogo sana, anatumai atawahamasisha watu wengi zaidi kuwasaidia wagonjwa hao.

Licha ya kuchora picha na kuwasaidia wagonjwa wa UKIMWI Bw. Kang Yaonan pia anajitahidi kuimarisha maingiliano ya wasanii kati ya China bara na kisiwa cha Taiwan na kuwajumuisha kwenye maonesho ya sanaa kwa ajili ya kuwasaidia zaidi wagonjwa wa UKIMWI.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-27