Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-28 10:58:14    
Barua 0628

cri
       Msikilizaji wetu Hilal Nasor Zahor Al- Kindy wa sanduku la posta 22 P.C.119, Al-Amrat, Oman ametuletea barua akishukuru kupokeajarida dogo la daraja la urafiki, na kubahatika kuona picha za baadhi ya wasikilizaji wanaoipenda Radio ya Kimataifa ya China na barua zao nzuri. Pia anashukuru kwa salamu za mwaka mpya zilizotolewa na mkurugenzi wa Radio ya Kimataifa Bwana Wang Gengnian kwa wasikilizaji wote wanaofuatilia mambo muhimu ya China, na anatoa pongezi kwa Radio China kwa juhudu zake za miaka 64 kuwaletea wasikilizaji matangazo mbalimbali. Anasema katika maendeleo yake na utamaduni wake wa kuwahudumia wananchi wake, Radio China pia haijawasahau wasikilizaji wake wakongwe.

Msikilizaji wetu Moffat Oseko, wa shule ya msingi Bokimai sanduku la posta 3657 Kisii Kenya, anasema katika barua yake kuwa, ndugu na jamaa zake wa CRI, anatumai tuko katika hali njema, tukiendelea na kuwafunulia watu matukio mbali mbali ya duniani kila siku. Kwanza kabisa anashukuru kwa kumjali yeye kama msikilizaji wetu kwa barua zetu. Kosa ni lake na tena si lake kwa maana amekuwa na shughuli nyingi sana katika maskani yake, hata hivyo anatoa pongezi kwa yote.

Swala la bahasha kutumika au la? Kwa hakika hii ndio mara yake ya kwanza kushuhudia bahasha ya namna hii lakini anatumai inatumika. Pili swala la mtandao wa internet ni jambo geni sana haswa katika sehemu wanakoishi, hivyo sio kusema eti kompyuta hazipo, zipo lakini ni chache mno na ziko mbali kama kilomita 25 hivi kutoka anaopishi, hata hivyo anashukuru sana kwa kumjulisha kuhusu tovuti ya idhaa yetu, anasema itakuwa yenye manufaa sana kwake.

Msikilizaji wetu Hilal Nasor Zahor Al- Kindy, P.O.Box 22, Al-Amrat, Oman anasema katika barua yake nyingine kuwa, leo anapenda kutoa yake machache, hasa anaomba Mola atuongezee amani katika dunia ya leo, kwani mambo mengi yanazidi kuwa sio ya kuvutia. Kila ukiamka unasikia mbali na matatizo mengine vita vinaendelea, anaomba ndugu zake tujaribu kuungana na kuwa kitu kimoja, ili vita kama vile vya Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Darfur visitokee tena. Kwani kumwaga damu bila sababu ya msingi sio jambo la busara. Anamaliza kwa kusema anaomba mola awe nasi.

Msikilizaji wetu mwingine Deogratius Mageni wa sanduku la posta 1484 Tabora Tanzania anasema katika barua yake kuwa, anatushukuru sana kupokea barua kutoka kwetu rafiki zake wapendwa. Anaungana nasi kusherehekea mwaka mpya wa kichina wa 2005, na anatutakia heri katika mwaka mpya huu wa kuku. Anapenda kutushukuru kwa kuboresha vipindi vyetu kwenye masafa mafupi na vipindi vyetu vyote vya aina mbali mbali katika tovuti ya kiswahili kwenye tovuti yetu.

Anatutakia furaha wananchi wa China na amani utulivu na mshikamano katika mwaka huu wa kuku. Anasema twende sambamba kama samaki na maji, hapo ndipo tunaweza kufika tunakotaka.

Msikilizaji wetu Asha Shabani Ally wa sanduku la posta 8 Tutuo, Tabora, Tanzania anasema katika barua yake yenye kichwa cha Udumu urafiki wetu na Radio China Kimataifa. Anatoa pongezi zake nyingi kwa uongozi wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anasema yeye anajivuna kuwa msikilizaji wa idhaa hii, kwani anaona ni idhaa inayomjali sana.

Anatoa shukrani nyingi kwa juhudi tunazozitoa kwa ajili ya kuwahudumia wasikilizaji wetu, hususan kwa kuwatumia kalenda, kadi, pamoja na bahasha zilizopiwa. Anatuomba tuzidi kuwafadhili zaidi ili kurahisha mawasiliano yetu. Akigeukia katika upande wa mawimbi, yaani usikivu wa matangazo yetu, anasema wao huko Tabora yanawafikia barabara kabisa. Labda tu kama kuna uwezekano, anataka tuongeze muda wa matangazo ya lugha ya kiswahili. Anamaliza kwa kusema atashukuru kama hili wazo lake tutalifanyia kazi.

Tunamshukuru sana kwa maoni yake kuhusu usikivu na vipindi vyetu, tunaendelea na juhudi kwa tuwezavyo, maoni na mapendekezo ya wasikilizaji wetu tunayakumbuka barabara, kama ikiwezekana, tutakidhi mahitaji ya wasikilizaji juu ya vipindi vyetu.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-28