Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-29 21:49:21    
Sera ya "watu wa Iraq kuitawala Iraq" yakabiliwa changamoto kubwa

cri

Tarehe 28 ilikuwa siku ya kutimiza mwaka mmoja tangu utawala wa jeshi la muungano la Marekani na Uingereza kukabidhi mamlaka kwa Iraq. Katika kipindi hicho, mwelekeo wa hali ya Iraq umeonesha kuwa, ingawa nchi hiyoimekomesha rasmi kisheria hali ya kukaliwa, lakini lengo la watu wa Iraq kuitawala Iraq bado linakabiliwa na changamoto kubwa.

Kwanza, hali ya usalama ya nchi hiyo inazidi kuwa mbaya. Baada ya jeshi la muungano la Marekani na Uingereza kukabidhi mamlaka kwa Iraq, vikundi vya wanamgambo vya Iraq vilifanya mashambulizi bila kusita dhidi ya jeshi la Marekani, jeshi la muungano, askari polisi wa Iraq, maofisa wa serikali, waumini wa dini na raia wa kawaida. Shirika la habari la AP lilitoa takwimu ikisema kuwa, katika mwaka mmoja uliopita, nchini Iraq yalitokea matukio zaidi ya 480 ya mashambulizi ya milipuko ya mabomu yaliyotegwa katika magari, na kusababisha vifo vya askari zaidi ya 890 wa Marekani na askari 74 wa jeshi la muungano. Baada ya serikali ya mpito ya Iraq kuasisiwa mwishoni mwa mwezi Aprili, vikundi vya wanamgambo vilizusha mkondo mpya wa milipuko ya mabomu.

Pili, baada ya kukabidhiwa mamlaka, ili kurejesha usalama na utulivu, jeshi la Marekani na utawala wa Iraq yalishirikiana kuanzisha operesheni kubwa nyingi za kijeshi dhidi ya wanamgambo, kuwaua wanamgambo zaidi ya elfu moja na mia kadhaa, na kuwakamata washitakiwa wa usalama zaidi ya elfu kumi. Lakini Marekani na Iraq bado haziwezi kuzuia kwa ufanisi shughuli za kimabavu zilizofanywa na vikundi vya wanamgambo likiwemo kundi la al-Qaeda Group of Jihad lililoongozwa na Abu Musab al-Zarqawi, ambaye ni kiongozi wa nambari ya tatu wa kundi la al-Qaeda. Marekani imekiri hivi karibuni kuwa, Marekani imefanya mazungumzo ya siri na vikundi kadhaa vya upinzani ili kutafuta ufumbuzi wa kisiasa. Lakini hayo yote bado hayajaleta matokeo mazuri.

Tatu, ukarabati wa kisiasa wa Iraq umekumbwa na matatizo mengi. Katika mwaka mmoja uliopita, Iraq ilitimiza shughuli kubwa za ukarabati wa kisiasa kama vile kufanya uchaguzi wa bunge la mpito na kuundwa kwa serikali ya mpito. Lakini mchakato wa ukarabati wa kisiasa wa nchi hiyo unakabiliwa na matatizo mengi. Madhehebu ya Suni kususia uchaguzi wa bunge uliofanyika mwishoni mwa Januari kumesababisha uchaguzi huo wa kwanza wa kidemokrasia kukosa uhalali, baadaye madhehebu ya Suni, Shia na kundi la Wakurd yaligombana kwa mfululizo kutokana na mgawanyo mbaya wa kisiasa, na kusababisha serikali ya mpito iahirishwe kuundwa. Hayo yote yametia mashaka kuhusu lini Iraq mpya yenye demokrasia inayodaiwa na Marekani inaweza kuundwa.

Nne, kutokana na athari ya mazingira ya usalama na hali ya kisiasa, kazi ya ukarabati wa kiuchumi wa Iraq inaendelea pole pole. Misaada ya kimataifa haiwezi kufika kwa haraka, wakazi wengi wa Iraq bado wanakumbwa na ukosefu wa kazi na maisha magumu.

Wachambuzi wanaona kuwa, katika mwaka mmoja uliopita tangu utawala wa jeshi la muungano la Marekani na Uingereza kukabidhi mamlaka kwa Iraq, mchakato wa ukarabati wa kisiasa, kiuchumi na usalama wa nchi hiyo unaendelea kwa shida, sababu yake kubwa ni kuwa, japokuwa hali ya kukaliwa imemalizika kisheria, lakini matakwa ya wakazi wa Iraq bado hayawezi kuheshimiwa ipasavyo. Marekani inashikilia kuweka jeshi nchini Iraq, na kujaribu chini juu kuunda Iraq mpya kutokana na usanifu wake. Ufumbuzi wa suala la Iraq ni kutimiza kihalisi sera ya watu wa Iraq kuitawala Iraq, kuwaachia watu wa Iraq washughulikie mambo yao kwa kujiamulia.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-29