Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-30 18:08:43    
Geng Ruixian awaongoza wanakijiji kujiendeleza kwa njia ya kistaarabu

cri

Kijiji cha Gengzhuang kiko katika kitongoji cha mji wa Xinxiang, mkoani Henan, katikati ya China. Zaidi ya miaka kumi iliyopita, kijiji hicho kilikuwa maskini sana, pato la wanakijiji lilikuwa dogo, hali duni inaonekana kote kijijini, lakini katika miaka ya karibuni, kijiji hicho kimepata mabadiliko makubwa. Muda mfupi uliopita mwandishi wetu wa habari alikitembelea kijiji hicho, akiona barabara za saruji ambazo zimefika mpaka kwenye majengo maridadi ya kisasa. Wanakijiji walisema kwa fahari kuwa, mabadiliko hayo yote yalitokea kutokana na uongozi wa mkurugenzi wa kamati ya kijiji hicho Bwana Geng Ruixian.

Bw. Geng Ruixian mwenye umri wa miaka 36 aliwahi kujiunga na jeshi. Baada ya kumaliza kulihudumia jeshi alirudi kijijini  kufuga kuku , na pia alikuwa anaendesha Taxi. Baada ya kipindi kifupi familia yake ilipata maendeleo.

Watu wengi wa kijiji cha Gengzhuang walikuwa wakiishi kwa kutegemea kilimo, lakini kutokana na idadi kubwa ya watu na uhaba wa ardhi, wanakijiji waliishi maisha ya kujikimu tu. Kuona maisha duni ya wanakijiji, Bw. Geng Ruixian hawezi kufurahia maendeleo yake mwenyewe. Anasema: 

"Ingawa mimi mwenyewe nimetajirika, lakini wanakijiji wenzangu bado wanaishi maisha duni. Nafikiri thamani yangu itaonekana katika kuwahudumia wanakijiji wenzangu na jamii kwa ujumla ili wote watajirike."

Mwezi Aprili mwaka 1995, kamati ya kijiji cha Gengzhuang ilifanya uchaguzi wa mkurugenzi mpya, Bw. Geng Ruixian aliyekuwa na umri wa miaka 26 wakati huo alipata asilimia 95 ya kura, na kuwa kiongozi mpya wa kijiji hicho chenye watu zaidi ya 2000.

Bw. Geng Ruixian aliona kuwa jukumu lake ni kubwa, aliacha biashara yake mwenyewe ya kuendesha taxi na ufugaji kuku, akijitumbukiza kabisa shughuli za kijijini. Alianza kazi yake kwa kushughulikia mambo yaliyohusu zaidi maisha ya kila siku ya wanakijiji, kama vile maji safi, umeme, na barabara. Alipokabiliana na upungufu wa fedha, alichukua fedha zake mwenyewe kununua zana na malighafi, pia aliwaongoza makada wa kijiji kujaribu kuchangisha fedha na kutengeneza njia tatu za saruji katika miezi miwili. Baada ya kupata maendeleo ya kiuchumi , kijiji hicho kwa nyakati tofauti kiliwekeza yuan milioni 17 kukarabati barabara, kutengeneza mabomba ya maji, na kujenga mfumo kamili wa kuondoa maji machafu. Hali ya makazi ya wanakijiji inaboreshwa kidhahiri. Mwanakijiji Bi. Geng Junzhi anasema:

"Sasa barabara za kijiji chetu ni nzuri zaidi kuliko sehemu kadhaa za mjini, usiku taa za mitaani zinamulika, hatuna wasiwasi tena kutembea njiani wakati mvua inanyesha au hata kama theluji inaanguka usiku."

Katika miaka ya karibuni, Bw. Geng Ruixian aliwaongoza wanakijiji kujenga majengo ya kisasa ya shule, kuanzisha channel ya televisheni ya waya, maktaba, na kuweka simu kwa familia zote. 

Aliposhika madaraka Bw. Geng Ruixian alifanya uamuzi muhimu, yaani kuendeleza kilimo cha jadi sambamba na kukuza viwanda. Kiwanda cha kwanza cha kijiji hicho ni cha Carbon Bisulfide. Baada ya miaka michache, thamani ya uzalishaji mali ya kiwanda hicho ilifikia yuan milioni 100 kwa mwaka, na kikawa uti wa mgongo wa uchumi wa kijiji hicho.

Hivi sasa kijiji cha Gengzhuang kina mashirika 8 yaliyodhibitiwa na kamati ya kijiji, kila mwaka thamani ya uzalishaji mali inafikia yuan milioni 250, pato la wastani la mwanakijiji limefikia yuan 6300, likiwa limeongezeka mara kumi kuliko lile la miaka kumi iliyopita.

Licha ya viwanda, kilimo cha jadi cha kijiji hicho pia kilipata maendeleo makubwa, hivi sasa mashamba yote yanalimwa kwa mitambo, mashamba zaidi ya hekta 90 ya kijijini yaliyohitaji nguvukazi ya watu zaidi ya 1000 zamani, sasa yanashughulikiwa na watu 13 tu.

Mwaka 2001, kamati ya kijiji cha Gengzhuang iliamua kujenga kijiji cha likizo cha viumbe na kukuza utalii wa viumbe. Bw. Geng Ruixian aliwaongoza wanakijiji kufanya kazi usiku na mchana, huku wakichapa kazi kwa miezi 18, kijiji cha likizo chenye mazingira mazuri ya maumbile kilichowekezwa yuan milioni 50, na kuchukua ardhi zaidi ya hekta 50 kilijengwa tayari. Baada ya kufunguliwa kwa watalii kijiji hicho kimeleta ufanisi mzuri sana wa kiuchumi kwa wakulima. Bw. Geng Ruixian anasema:

"Ili kuondokana na umaskini, hatuna budi kuchapa kazi kwa moyo wa kujitolea."

Jitihada za Bw. Geng Ruixian na wenzake zilileta matokeo mazuri. Muda si mrefu uliopita, kijiji cha Gengzhuang kilipewa sifa ya kijiji cha ustaarabu cha kitaifa, Bw. Geng Ruixian mwenyewe alipewa sifa ya mfanyakazi bora wa kitaifa kutokana na kuwaongoza wanakijiji kujiendeleza kwa kujitegemea. 

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-30