|
Kamati ya usimamizi wa katiba ya Iran ilitoa taarifa tarehe 29, ikitangaza kuidhinisha matokeo ya upigaji kura wa duru la pili katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika tarehe 24 mwezi huu. Hivyo, meya wa mji wa Teheran Bw. Mahmood Ahmadi Nejad alichaguliwa rasmi kuwa rais wa awamu ya tisa wa Iran. Wachambuzi wanaona kuwa, Bw. Nejad akiwa ni mwanasiasa mpya nchini Iran, atakabiliana na changamoto mbalimbali katika mambo ya ndani na ya nje.
Bw. Nejad anachukuliwa kuwa mwakilishi wa kundi la wahafidhina. Watu wengi wameingiwa na wasiwasi kuwa atatekeleza "sera kali ya uhafidhina" baada ya kushika madaraka. Na kutakuwepo na migongano mikubwa kati ya kundi la wahafidhina na kundi la watu wanaopendelea mageuzi. Namna ya kuboresha uhusiano kati ya makundi hayo mawali ni suala linalotakiwa kutatuliwa baada ya Bw. Nejad kushika madaraka. Kuhusu hali hiyo, Mshauri wake mmoja tarehe 29 alisema kuwa, Rais huyo mpya "hatarudi nyuma", na pia huenda ataweka sera yenye uwazi na unyumbufu zaidi.
Katika uchaguzi huo, waungaji mkono wengi wa Bw. Nejad ni watu wa kawaida katika jamii. Wakati alipokuwa meya wa mji wa Teheran, aliweka mkazo katika kuendeleza uchumi, kuongeza nafasi za ajira, na kuboresha hali ya elimu na mawasliano mjini humo. Hatua hizo zilimwekea msingi thabiti wa umma wakati akigombea urais. Hivyo, namna ya kuendeleza uchumi na jamii ya Iran, kuwaendeleza wananchi na kuwapatia nafasi za ajira na elimu ni suala la pili linalokabili Bw. Nejad.
Kuhusu mambo ya nje, Bw. Nejad pia anakabiliana na matatizo mbalimbali. Kwanza ni suala la nyuklia la Iran. Bw. Nejad tarehe 26 alisema kuwa, Iran inataka kuendelea kushiriki kwenye mazungumzo ya nyuklia na Umoja wa Ulaya kwenye msingi wa kulinda maslahi ya taifa la Iran na kushikilia haki za kutumia teknolojia za nyuklia kwa njia ya amani. Lakini mipaka ya msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala hilo ni kutaka Iran isimamishe daima shughuli za kusafisha uranium. Pande hizo mbili zina mgogoro wa kimsingi kuhusu suala hilo. Hivyo, namna ya kutatua suala hilo ni changamoto ya kwanza inayokabili Bw. Nejad katika mambo ya nje.
Changamoto nyingine kwa Bw. Nejad ni namna ya kupanua mazingira ya kimataifa ya Iran chini ya shinikizo la Marekani. Baada ya Bw. Nejad kuchaguliwa, Marekani imetangaza kuwa haitabadilisha sera ya hivi sasa kwa Iran. Kuhusu hali hiyo, Bw. Nejad alisisitiza kuwa, kama Marekani ikiendelea na msimamo wa uadui kwa Iran, Iran haina haja wala haitaboresha uhusiano kati yake na Marekani. Kama hivyo, uhusiano kati ya nchi hizo mbili hautaboreshwa katika muda mfupi, na huenda utakuwa mbaya zaidi.
Mwishowe, namna ya kushughulikia uhusiano kati ya Iran na nchi jirani pia ni shughuli muhimu kwa Bw. Nejad katika mambo ya nje. Baada ya Bw. Nejad kuchaguliwa, nchi za kiarabu zote zina wasiwasi kuhusu kuathiriwa kwa uhusiano kati yao na Iran. Ili kuondoa wasiwasi huo, Bw. Nejad amesema kuwa, atatetea uhusiano mzuri kati ya Iran na nchi za kiarabu.
Bw. Nejad aliwahi kusema kuwa, atajaribu kujenga mfano wa "jamii ya kiislam ya kisasa yenye nguvu". Wachambuzi wanaona kuwa, si rahisi kutimiza lengo hilo kubwa. Namna Bw. Nejad atakabiliana na changamoto hizo, itafuatiliwa na wananchi wa Iran na jumuiya ya kimataifa.
Idhaa ya Kiswahili 2005-06-30
|