Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-04 16:52:52    
Maktaba za umma zaendelea haraka nchini China

cri

Mradi wa pili wa ujenzi wa Maktaba ya Taifa ya China ulizinduliwa hivi karibuni mjini Beijing. Hii inaashiria kuwa maktaba za umma nchini China, zimeingia katika kipindi kipya cha maendeleo nchini China.

Maktaba nchini China zimegawanyika katika aina nne, yaani maktaba za umma, maktaba za idara za sayansi na teknolojia, maktaba za shule na maktaba za mashirika. Hivi sasa kwa jumla nchini China kuna maktaba za umma za ngazi ya wilaya na mikoa 2700.

Mradi wa pili wa ujenzi wa Maktaba ya Taifa ya China utagharimu yuan bilioni 1.3. Baada ya mradi huo kukamilika maktaba hiyo itakuwa kituo kikuu cha kuhifadhi vitabu vya Kichina. Mradi huo utamalizika na kuanza kutumika mwezi Oktaba, mwaka 2007. Wakati huo maktaba hiyo ya taifa itakuwa maktaba kubwa kabisa ya umma na yenye huduma za kisasa kabisa nchini China. Uzinduzi wa mradi huo ni dalili ya maendeleo ya haraka ya maktaba za umma katika miaka ya karibuni. Naibu mkurugenzi wa Taasisi ya Maktaba ya China Bw. Zhan Furui alisema, "Katika miaka ya karibuni serikali imetenga fedha nyingi katika sekta ya utamaduni. Hivi sasa maktaba za umma na majumba mengi ya makumbusho yamejengwa katika mikoa na miji mikubwa. Hali hiyo inamanisha kuwa maktaba za umma zimepanda ngazi mpya ya maendeleo."

Kutokana na takwimu za Wizara ya Utamaduni, idadi ya vitabu vilivyopo ndani ya makataba za umma inaongezeka kwa 10% kila mwaka na vitabu ndani ya maktaba za umma kwenye sehemu za mwambao, vinaongezeka hata maradufu kwa mwaka.

Kadiri uchumi unavyokua, ujenzi wa miji pia unaendelea haraka. Licha ya maktaba za umma za nganzi ya taifa, mkoa na wilaya, maktaba za umma pia zimetokea ambazo hazikuwepo hapo kabla katika sehemu za makazi. Katibu mkuu wa Taasisi ya Maktaba ya Taifa Bi. Tang Gengsheng alieleza kuwa katika nchi zilizoendelea maktaba kwenye sehemu za makazi ni sehemu muhimu ya utamaduni wa wakazi. China ni nchi inayoendelea, ujenzi wa miji haujakamilika, kazi za kujenga maktaba katika sehemu za makazi bado zina nafasi kubwa ya kuendelea. Alisema, "Maktaba kwenye sehemu za makazi zinalenga maktaba kwenye sehemu za makazi mijini, kwenye mitaa ya makazi na vijijini, Wizara ya Mambo ya Raia inaposukuma mbele maendeleo ya utamaduni wa sehemu za makazi, inazingatia zaidi ujenzi wa maktaba, kwani maktaba hizo ziko karibu zaidi na wakazi. Kama mambo mengine yanavyoendelea, maktaba nchini China pia zimeingia katika kipindi kipya cha ustawi."

Ili kuzifanya maktaba za umma zitoe mchango mkubwa zaidi, kuanzia mwishoni mwa karne iliyopita, maktaba nyingi za umma zimeamua mwezi Desemba wa kila mwaka kuwa ni "mwezi wa kusoma". Katika mwezi huo maktaba hufanya mihadhara na kuwafahamisha wasomaji vitabu bora vipya. Licha ya "mwezi wa kusoma", kila mwaka katika "siku ya haki ya kunakili duniani", yaani tarehe 23 Aprili, maktaba za umma hufanya shughuli za kuhamasisha watu kusoma vitabu na kufanya mashindano ya kuandika insha, na kuwavutia watu wengi kwenye maktaba na kuwafahamisha kwamba maktaba ni mahali pa kujielimisha katika maisha yote ya binadamu.

Ni kweli kwamba maendeleo ya maktaba katika miaka ya karibuni ni makubwa nchini China, lakini maendeleo hayo yakilinganishwa na nchi zilizoendelea bado yako nyuma sana. Mathalan, idadi ya vitabu vinavyohifadhiwa ndani ya maktaba za umma, hivi sasa ni nakala milioni 500 tu kote nchini China. Idadi hiyo ni ndogo sana kiasi cha kusikitisha, ikilinganishwa na idadi kubwa ya Wachina bilioni 1.3, na maendeleo hayo yanatofautiana sana kati ya miji na vijiji, kati ya sehemu ya mashariki na magharibi. Mkurugenzi wa Taasisi ya Maktaba alipozungumzia matatizo ya maktaba alisema, "Maktaba za umma huwekezwa na serikali, lakini kutokana na sababu fulani fedha hazikutengwa au fedha chache zilitengwa, kwa hiyo maendeleo yanaathirika. Tatizo lingine ni kutokuwa na katiba ya maktaba. Matatizo hayo mawili ni sababu muhimu za kukwamisha maendeleo ya maktaba nchini China.

Bi. Tang Gengsheng alisema, ustawi wa huduma za jamii unategemea sana uchumi, kwa hiyo kutokana na jinsi uchumi unavyoendela, maktaba za umma nchini China hakika zitapiga hatua kubwa zaidi katika siku za mbele.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-03