Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-05 15:13:55    
Barua 0705

cri
     Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa P.O. Box 161 Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, yeye ni mzima wa afya njema akiendelea na shughuli za kila siku za ujenzi wa taifa la Tanzania, na kusikiliza vipindi na matangazo ya kila siku ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa.

Anasema anapenda kutujulisha kuwa amepokea barua yetu tuliyomtumia mwezi Machi mwaka huu, pamoja na kadi maalumu ya kumtakia kheri ya mwaka mpya wa 2005 ikiambatana na kalenda, karatasi zilizokatwa kwa ufundi na ustadi mkubwa, zikiwa zinaonyesha picha ya vifaranga vya kuku na kuku dume yaani jogoo. Picha hizo zilimthibitishia kuwa mwaka huu ni mwaka wa kuku, ikiwa ni alama ya kumi kuelekea duru moja lenye miaka 12 kwa wanyama 12 wanaotambuliwa na China kama wanyama maalumu kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 12, kukamilisha duru na kuanza upya. Anasema yeye anavutiwa na mnyama wa kufikirika katika China ya Kale Dragoni, akiwa amepangwa wa tano kati ya wanyama hao 12.

Anasema vilevile amevutiwa sana na mnyama (ndege) wa 10 ambaye ni kuku na kukubaliana kabisa na sifa tano alizopewa na wahenga wa China yaani sifa ya kwanza kilemba chake chekundu kichwani kinaoyesha sifa ya utamaduni; sifa ya pili miguu yake hodari kwa kukwatua, inaonesha ana sifa ya ushupavu; anapopata au kugundua chakula huwaita wenzake, ana sifa ya roho nzuri na ya kusaidiana; na sifa ya tano anawika kila alfajiri, ana sifa ya uaminifu: hakika hii ni falsafa ya kweli inayokubalika kabisa.

Waafrika wengi ni wafugaji wa kuku hivyo Waafrika wengi kama ilivyo kwa marafiki na ndugu zao wa China, wanavutiwa sana na hadithi ya kuku na kuwafanya watu waone ufahari mkubwa katika ufugaji wa kuku. Siyo kwa wachina na waafrika tu, lakini kwa watu wote katika dunia nzima. Anasema sifa hizi alizozitaja kuhusu kuku, amezinukuu kutoka katika barua tuliyomtumia.

Anatushukuru sana kwa maneno na maelezo matamu matamu tuliyomtumia kuhusu mwaka huu wa 2005 ukiwa ni mwaka wa kuku uliopangwa na wahenga wa kale wa China. Anatarajia na kuamini kwamba mwaka huu wa 2005 utakuwa mwaka wenye baraka na mafanikio makubwa kwa watu wote wapendao maendeleo duniani wakiwemo watumishi wote wa Radio China Kimataifa pamoja na wasikilizaji wake wote katika pembe zote za dunia.

Bwana Kulwa pia ameshukuru sana kwa Gazeti la Picha toleo la 2/2005 ambalo pia lina habari kemkem ndani yake. Anasema atafurahi sana kama tutaendelea kumtumia majarida na magazeti mbalimbali kutoka China likiwemo jarida dogo la Daraja la Urafiki tunalolichapisha kwa lugha ya Kiswahili.

Katika barua yake nyingine Bwana Kulwa anasema, anafurahi na kushukuru sana kwa juhudi zetu kubwa tunazozifanya ili kuhakikisha wasikilizaji wanapata na kupokea vipindi motomoto na habari za uhakika zisizo na mashaka wala wasiwasi. Hiyo imewafanya wasikilizaji kuiamini na kuipenda sana Radio China Kimataifa, ikiwa na wahariri, watayarishaji na watangazaji waliobobea na wenye umahiri wa kiwango kikubwa katika kazi zao. Anatutaka tupokee hongera na tupokee shukrani kwa kazi zetu nzuri za kuwapasha mambo makubwa na yenye uhakika.

Bwana Kulwa anasema ni mwaka mmoja umepita tangu tumewajulisha kwamba tunatengemea kuanza kuchapisha jarida la Kiswahili litakalojulikana kama "Daraja la Urafiki", yeye alifurahishwa sana na taarifa hiyo kwa kuwa ilikuwa inaonesha hatua nyingine itakayopigwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, kwa kuchapisha jarida hilo. Kwa sababu hii anapenda kuwatia shime na pia kusisitiza juu ya umuhimu mkubwa wa jarida hilo la Daraja la Urafiki, na kama tulivyoeleza katika barua zetu ambazo tumewahi kuwatumia kwamba jarida hilo dogo litaimarisha mawasiliano na urafiki kati ya Radio China Kimataifa na wasikilizaji wake, na pia kuongeza mawasiliano kati ya wasikilizaji wa sehemu mbalimbali.

Anakubaliana kabisa na ukweli huo na anaomba kwamba Gazeti hilo tuanze kulichapisha na kama tumeshachapisha basi wanaomba tuanze kuwatumia wasikilizaji wetu. Kuhusiana na mambo ya kuchapisha, pamoja na kuchapisha barua, makala, mashairi mafupi, hadithi, maoni na mapendekezo ya wasikilizaji ni vizuri pia kama tutachapisha ratiba ya vipindi na muda wa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili. Anwani yetu ya posta pamoja na tovuti ya Kiswahili ya Mtandao wa Internet, nayo iwekwe kwenye jarida hilo, ili watu au wasikilizaji watakaolisoma waweze kuwasiliana nasi kwa urahisi.

Vilevile anasema ingekuwa ni vema zaidi kama katika jarida hilo pamoja na kutangaza majina ya washindi wa mashindano mbalimbali ya chemsha bongo yanayoendeshwa na Radio China Kimataifa kwa njia ya Radio, pia tunaweza kuchapisha majina ya washindi waliopata ushindi mkubwa. Anasema angependa kuona picha za wahariri na watangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwatambulisha na kuwafahamisha wafanyakazi hao kwa wasomaji na wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa.

Anasema zaidi ya hayo tunaweza pia kuchapisha baadhi ya picha za wageni mbalimbali ambao waliwahi kutembelea Idhaa ya Kiswahili ya CRI na kufanya mahojiano nasi wakiwemo marais, mabalozi na wageni wengine mashuhuri kutoka Afrika ambao walifika hapa Beijing na tukazungumza nao kwa Kiswahili, kwa kweli jarida hilo litaweza kuvutia sana na litaleta mvuto mkubwa miongoni mwa watu wengi.

Anasema, vilevile katika gazeti hilo tunaweza pia kuchapisha baadhi ya picha za wasikilizaji wetu picha moja au mbili kwa kila toleo inatosha sana ili kulifanya gazeti hilo lilingane na maana halisi ya kuongeza urafiki na ushirikiano na wasikilizaji wetu wote wa Idhaa ya Kiswahili. Anakamilisha kwa kusema kuwa akiwa msikilizaji wetu wa kudumu ataendelea kuwa mshiriki hai wa vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali.

Tunamshukuru sana Bwana Kilulu Kulwa kwa barua yake na maoni yake juu ya jarida dogo la Daraja la Urafiki, tunadhani sasa atakuwa ameshapata toleo la kwanza la jarida hilo, tunasubiri kusikiliza maoni na mapendekezo yake baada ya kusoma jarida hilo. Tumeona kuwa mapendekezo mengi aliyotutumia, baadhi tumeyazingatia na yapo kwenye jarida hilo dogo.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-05