Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-05 15:21:39    
Umoja wa Afrika wafanya mkutano wa 5 wa wakuu

cri

Mkutano wa 5 wa Umoja wa Afrika ulifunguliwa tarehe 4 huko Syrte, mji wa pwani mwa Libya. Wakuu wa nchi na serikali au wajumbe wao kutoka nchi wanachama 53 wa Umoja wa Afrika, pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Afrika, mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Ulaya, na katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu wamehudhuria mkutano huo wa siku mbili. Umoja wa Afrika ukiwa umoja halisi wa kisiasa ulio mkubwa zaidi wa bara zima, mkutano wake huo umefuatiliwa na dunia nzima.

Suala la maendeleo la dharura linaloikabili Afrika kwa hivi sasa limekuwa mada kuu ya mkutano huo. Kwa kuwa mkutano wa wakuu wa kundi la nchi 8 utakaofanyika tarehe 6 utalichukulia suala la maendeleo kuwa mada kuu ya mkutano, nchi za Afrika zinatumai kutumia fursa hii kuzitaka nchi zilizoendelea zitekeleze ahadi zao za kuisaidia Afrika, ili Afrika ifuate njia ya kuendelea vizuri. Kwenye mkutano wa wakuu wa Sirte, nchi kadhaa za Afrika ziliwataka viongozi wa kundi la nchi 8 kuwa nchi zilizoendelea zinapaswa kufuta kabisa madeni ya nchi maskini bila sharti lolote; kutekeleza ahadi zao za kutoa misaada ya fedha kwa Afrika; kuondoa vikwazo vya biashara na kurahisisha mauzo ya bidhaa za Afrika kwenye soko la nchi zilizoendelea. Juu ya hiyo, kiongozi wa Libya Kadhafi alisema kwenye mkutano huo kuwa, nchi za Afrika zinapaswa kuzishukuru nchi zilizoendelea kwa misaada yao, lakini zinakataa msaada wowote wenye masharti. Anaona kuwa, kuomba msaada kwa nchi za magharibi hakuna mustakbali kwa Afrika, kutaweza tu kuongeza pengo kubwa zaidi kati ya umaskini na utajiri duniani.

Matumaini ya Afrika ya kupiga hatua ya maendeleo kwa haraka yanaungwa mkono na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan. Kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Bwana Annan alitoa hotuba akizitaka nchi za Afrika zichukue hatua zenye ufanisi, kufanya juhudi za kutokomeza ugonjwa wa malaria na magojwa mengine na kueneza elimu ya msingi. Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso alisema kwenye mkutano huo kuwa, uhusiano barabara na wa haki wa kiwenzi kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika utasaidia kutimiza maslahi ya pamoja ya pande hizo mbili.

 

Mkutano huo pia umejadili hasa migogoro ya kisiasa barani Afrika. Suala la usalama la Afrika limekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya Afrika. Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika tarehe 4 lilitoa ripoti kwenye mkutano wa wakuu kuwa, tokea Umoja wa Afrika uanzishwe mwaka 2002, umoja huo umefanya juhudi za kushiriki kwenye usuluhishi wa migogoro iliyotokea nchini Somalia, Burundi, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Cote d'ivoire na Sudan, na kupata maendeleo makubwa kwa kutatua migogoro hiyo. Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Mustafa Othman Ismail alisema siku hiyo kuwa, kuhusu suala la Darfur la Sudan, Umoja wa Afrika ulitoa nguvu kubwa kabisa kwa kushiriki usuluhishi wa mgogoro wa kisehemu, hii imeonesha nia ya Umoja wa Afrika ya kutatua masuala ya Afrika kwa kujiamulia.

Lakini ripoti ya Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika imeonesha pia kuwa, matokeo ya juhudi za Umoja wa Afrika kwa ajili ya amani ya Afrika bado ni dhaifu, na lazima kufanya juhudi kubwa zaidi kwa kulinda amani iliyoletwa katika baadhi ya sehemu na kuzuia mgogoro mpya usitokee. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha, mipango ya Umoja wa Afrika ya kutuma jeshi la ulinzi wa amani kwa sehemu kadha wa kadhaa imekumbwa na vizuizi fulani. Hivyo nchi za Afrika zinaitaka jumuiya ya kimataifa iongeze misaada na kuongeza fedha za kuusaidia Umoja wa Afrika katika vitendo vyake vya kulinda amani.

Mkutano huo wa wakuu wa Umoja wa Afrika pia umejitahidi kutafuta maoni ya pamoja kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa. Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Bwana Alpha Oumar Konare amesema kuwa, Umoja wa Afrika unaunga mkono mageuzi ya Umoja wa Mataifa, na nchi za Afrika zitaonesha umuhimu wake mkubwa katika Umoja wa Mataifa baada ya kufanyiwa mageuzi.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-05