Rais Muammar al-Qadhafi wa Libya jana alipotoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano wa tano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika uliofanyika katika mji wa Sirte nchini Libya, alisisitiza kuwa nchi za Afrika zinatakiwa kutatua suala la maendeleo yake kwa kujitegemea. Alisema kuwa ikiwa Afrika inategemea sana misaada ya nchi za magharibi, itaathiri mustakabali wake. Maneno hayo ya rais Qadhafi yanaonesha Afrika iliyopata uhuru inaanza kufuata njia ya kujiimarisha kiuchumi.
Katika muda mrefu uliopita bara la Afrika lilikuwa katika hali ya umaskini duniani. Mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika unaofanyika hivi sasa mjini Sirte pamoja na mkutano wa wakuu wa nchi wa kundi la nchi 8 utakaofanyika hivi karibuni unachukulia suala la maendeleo ya Afrika kuwa ni moja ya ajenda muhimu ya mikutano. Katika miongo kadhaa iliyopita nchi za viwanda za magharibi ziliwahi kutoa misaada ya kiuchumi kwa nchi za Afrika, lakini misaada hiyo haikuboresha kihalisi uchumi wa Afrika kutokana na kuwa misaada hiyo iliambatana na masharti magumu yasiyo ya haki, utaratibu wa kimataifa wa uchumi na biashara usio wa haki uliokuwepo kwa miaka mingi, pamoja na misaada iliyotolewa na baadhi ya nchi za magharibi ambayo ilikuwa kidogo ikilinganishwa na ahadi zao, hata kufanya baadhi ya nchi za Afrika kubeba mzigo mzito wa madeni na kupunguza juhudi za nchi za Afrika za kuleta maendeleo ya uchumi.
Katika miaka ya karibuni, nchi za Afrika zimefahamu kuwa kimsingi, maendeleo ya Afrika yanazitegemea nchi za Afrika zenyewe. Afrika lazima ijitoe kutoka kwenye hali ya kutegemea nchi zilizoendelea, na kufuata njia ya kujiimarisha kiuchumi kwa kutumia akili na uvumbuzi wake. Ni katika hali ya namna hiyo, rais Qadhafi ametoa mwito wa kutaka nchi za Afrika zilete maendeleo kwa kujitegemea. Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Bw. Alpha Oumar Konare pia alitoa wito akizitaka nchi za Afrika zijitegemee na kutatua suala la mitaji kwa kuendeleza raslimali za nchi zake.
Kufuata njia ya kujitegemea, kwanza kabisa inazipasa nchi za Afrika zijitahidi kadiri ziwezavyo. Kuhusu suala hilo rais Qadhafi alisema, "Afrika yetu siyo maskini, bara letu ni bara lenye utajiri. Sisi tuna maji, mafuta ya asili ya petroli na gesi, tatizo letu ni kushindwa kusimamia na kutumia ipasavyo raslimali zetu." Ni kweli kuwa kutokana na kiwango cha chini cha maendeleo, uendelezaji wa teknolojia na usimamizi wa uchumi wa Afrika uko katika kiwango cha chini. Jambo la haraka kwa hivi sasa ni kuwa nchi za Afrika zingekomesha haraka iwezekanavyo mapigano na migogoro ya kikabila na kujenga mfumo kamili wa kuendesha jamii na wenye ufanisi ili kuanzisha mazingira bora ya jamii kwa maendeleo ya uchumi.
Lakini msingi wa uchumi wa nchi za Afrika bado ni dhaifu na ni vigumu kuleta maendeleo kwa kutegemea nguvu zake zenyewe. Hivyo nchi zilizoendelea zinatakiwa kutekeleza majukumu yake na kutoa misaada kwa nchi za Afrika ili ziondokane na umaskini. Mkutano wa mawaziri wa kundi la nchi 8 uliofanyika mwezi Juni mwaka huu mjini London uliamua kusamehe kabisa madeni ya dola za kimarekani bilioni 40 ya nchi 18 zilizo maskini kabisa barani Afrika, mpango mkubwa huo wa kusemehe madeni umeleta uungaji mkono na nafasi nzuri kwa maendeleo ya Afrika. Katika wakati huu nchi za magharibi zinatakiwa kutekeleza kwa makini ahadi zilizotoa, kupunguza na kusamehe zaidi madeni ya nchi maskini na kupiga hatua katika kuhamisha teknolojia na kuondoa vizuizi vya kibiashara. Aidha, jumuiya ya kimataifa pia inatakiwa kujitahidi kwa pamoja na kuhimiza kujengwa mapema utaratibu mpya wa kisiasa na kiuchumi wa kimataifa, ambao ni masharti muhimu kwa maendeleo ya Afrika.
Idhaa ya Kiswahili
|