Katikati ya mwezi Agosti mwaka huu, Israel itaanza rasmi mpango wa kuondoka kutoka kwenye eneo la Gaza na sehemu za kaskazini za kando ya Mto Jordan. Hivi sasa, kazi mbalimbali za maandalizi za serikali ya Israel na jeshi lake zimeanzishwa, ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa bila matatizo.
Kwenye mkutano maalum wa bunge la Israel uliofanyika tarehe 5 kuhusu kazi za maandalizi za mpango wa upande mmoja, wajumbe wa baraza la mawaziri akiwemo waziri mkuu wa Israel Bw. Ariel Sharon walijibu maswali 150 yaliyotolewa na wabunge na wajumbe wa walowezi, pia walieleza hali ya maendeleo ya kazi mbalimbali za maandalizi.
Bw. Sharon kwenye mkutano huo alisisitiza kuwa, mpango huo hakika utaanzishwa kwa wakati uliopangwa na serikali. Alisema kuwa, "Mnaweza kufanya maandamano, pia mnaweza kuukosoa, lakini hamruhusiwe kuzuia mawasiliano, wala kutumia njia ya mabavu." Aliwataka wakazi wawafikirie watoto wao. Bw. Sharon alisema kuwa, serikali itawapanga vizuri walowezi watakaoondoka. Pia alionya kuwa, kama Wapalestina wenye silaha watashambulia shabaha la Israel wakati wa kuondoka, jeshi la ulinzi la Israel litalipiza kisasi kwa njia mbalimbali. Alisema, Israel haitaondoka kutoka eneo la Gaza katika hali ya mapambano.
Waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Shaul Mofaz kwenye mkutano huo alitangaza kuwa, idara za ulinzi za Israel zimeanza kufanya maandalizi kwa mpango huo. Alidokeza kuwa, idara ya usalama ya Israel itatuma wanajeshi 41,000 na polisi 3,800 kutekeleza kazi ya kuondoka. Idadi hiyo ni mara 5 ya wakazi watakaoondoka. Wanajeshi hao watapangwa kwa ngazi 6 kushughulikia kazi hiyo, na kazi hiyo itafanyika kwa wiki 4. Bw. Mofazi pia alitangaza kuwa, hivi sasa serikali ya Israel inafanya mashauriano na mamlaka ya utawala wa Palestina kuhusu kubomoa nyumba za makazi. Alisema kuwa kazi hiyo itatumia miezi mitatu, na itagharamu dola za kimarekani milioni 50 hadi milioni 60.
Idara ya polisi ya Israel ilidokeza kuwa, hivi sasa polisi 14,000 nchini Israel wamepokea mafunzo husika, na kazi yao ni kuwaondoa wakazi, kuimarisha kazi ya ulinzi wa Jerusalem na Temple Mount na kulinda idara za serikali, ili kuepusha hali ya vurugu kutokea, na kuhakikisha utaratibu wa jamii. Idara ya usimamizi wa sheria ya Israel ilieleza kuwa, itaongeza mahakama ya muda na idadi ya mahakimu, ili kushughulikia kesi zinazoweza kuongezeka wakati wa kuondoka.
Kuhusu kazi ya kupanga wakazi, kwa mujibu wa mpango wa serikali ya Israel, wakazi hao watakaa katika makazi ya daima baada ya miaka minne, na katika kipindi hicho, serikali itawapatia wakazi nyumba za muda. Hivi sasa, mpango wa nyumba za muda umetayarishwa, hivyo kuanzia siku ya kwanza ya kuondoka, familia zaidi ya 1,500 zitapata nyumba za muda. Ofisi ya mpango wa upande mmoja wa Israel ilidokeza kuwa, hivi sasa familia 400 zimetoa ombi la kupata fidia, na familia zinazokubali mpango huo zimefikia 500. Wizara ya viwanda na biashara ya Israel imejenga kituo cha ajira katika sehemu za kati na magharibi za Israel na kaskazini ya kando ya Mto Jordan, ili kuwasaidia wakazi hao kupata ajira.
Palestina pia imeanza kazi za maandalizi. Tarehe 4, wanajeshi 5,000 wa kikosi cha usalama cha Palestina walianza kupewa mafunzo, ili kulinda utulivu wa eneo la Gaza wakati Israel inaondoka kutoka eneo hilo. Aidha, katika ushirikiano wa Israel, Palestina na Misri, shughuli za Wapalestina wenye silaha kufanya magendo ya silaha katika eneo la Gaza kutoka nchini Misri zimezuiliwa. Hivi sasa, Israel na Misri zinajadiliana kuhusu kupanga polisi 750 wa Misri kwenye sehemu za Gaza na mpaka wa Misri baada ya Israel kuondoka.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-06
|