Mkutano wa viongozi wakuu wa kundi la nchi nane tajiri (G 8) utafanyika kuanzia tarehe 6 hadi 8 mwezi huu huko Gleneagles Scotland, kaskazini mwa Uingereza. Viongozi hao watajadili namna ya kusaidia Afrika iondokane na umaskini na tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Ingawa mambo hayo mawili ni mada muhimu katika mkutano huo, lakini wachambuzi wanaona kuwa mkutano huo utakuwa na "tofauti kubwa kuliko mapatano" kutokana kila nchi kutaka kulinda maslahi yake.
Mada ya kusaidia Afrika iondokane na umaskini ni mara ya kwanza kutokea katika historia ya mikutano ya viongozi wakuu wa nchi nane tajiri. Miaka ya karibuni, kutokana na utandawazi wa dunia unavyoendelea, nchi maskini zinazoendelea na hasa nchi za Afrika zinapuuzwa siku hadi siku. Baadhi ya nchi tajiri zimegundua kuwa tofauti ya nguvu za taifa na maisha ya wananchi kati ya nchi tajiri na nchi maskini imekuwa kubwa na ya kushitusha, na tofauti hiyo italeta madhara makubwa katika utulivu na maendeleo ya uchumi duniani. Waziri mkuu wa Uingereza Blair alisema kuwa ikiwa hali hiyo haitabadilika "nchi zilizoendelea hazitaweza kutimiza lengo la maendeleo". Kwa hiyo kusaidia Afrika iondokane na umaskini sio tu ni kwa ajili ya kuzisaidia nchi maskini kukomesha umaskini, bali pia ni kwa ajili ya maslahi ya nchi hizo tajiri.
Kuhusu tatizo hilo, sio tu wanasiasa wamefahamu umuhimu wake, bali pia watu wa kawaida wa Afrika ambao walifanya maandamano, walitaka viongozi wa nchi nane watimize ahadi zao kwa vitendo.
Ingawa masuala mawili ya kusaidia nchi maskini kuondokana na umaskini na mabadiliko ya hali ya hewa duniani yamepewa uzito katika mkutano huo, lakini vyombo vya habari vya Uingereza vinaona kuwa mkutano huo hautapata mafanikio kwa sababu masuala hayo yanakumbwa na vizuizi.
Kuhusu suala la kusaidia Afrika, mkutano wa mawaziri wa fedha uliofanyika mwezi uliopita ulifikia maafikiano kuhusu kuzisamehe nchi 14 maskini madeni yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 40. Huu ni msamaha mkubwa wa madeni uliokubaliwa katika mkutano huo wa mawaziri wa fedha. Lakini msamaha wa madeni peke yake hautoshi kwa utatuzi wa suala la umaskini mbaya wa Afrika, bali inahitajika kuongeza misaada ya kuendeleza uchumi na kuchukua hatua za kuondoa ruzuku ya kilimo na kufungua soko. Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Blair kwa makusudi alizishawishi nchi mbalimbali za Ulaya, lakini hakupata mafanikio kuhusu ongezeko la misaada na kuboresha mfumo wa biashara, kwa hiyo ni dhahiri kuwa suala hilo haliwezi kutatuliwa katika mkutano huo.
Kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani, vizuizi vinatokana na Marekani. Marekani ni nchi inayotoa hewa chafu kwa kiasi kikubwa kabisa duniani, lakini mwaka 2001 rais Bush alijitoa kutoka "Mkataba wa Kyoto" kwa kisingizio cha "kupunguza utoaji hewa chafu kutaathiri uchumi wa Marekani" na "nchi zinazoendelea pia zinapaswa kubeba jukumu la kupunguza utoaji wa hewa chafu". Ingawa Uingereza ilifanya juhudi nyingi ili kuifanya Marekani irejee tena kwenye "Mkataba wa Kyoto" lakini msimamo mgumu wa Bush haukubadilika hata kidogo mpaka sasa. Wachambuzi wanaona kuwa kwa sababu mashuriano kati ya Uingereza na Marekani hayakupata matokeo yoyote kuhusu suala hilo, pengine suala la mabadiliko ya hali ya hewa litafutwa katika taarifa ya mkutano huo.
Wachambuzi wanaona kuwa inawezekana maafikiano fulani kuhusu masuala ya kimataifa yatapatikana kwa kiasi fulani, lakini kutokana na kila nchi kulinda maslahi yake, "tofauti kati ya nchi hizo ni kubwa kuliko makubaliano".
Idhaa ya kiswahili 2005-07-06
|