Ikulu ya Misri tarehe 7 ilitoa taarifa ikithibitisha kuwa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Misri nchini Iraq Bw. Ihabal-Sherif aliyetekwa nyara ameuawa. Kwenye taarifa hiyo, ikulu ya Misri ilisema kuwa imesikitika na tukio la kuuawa kwa shujaa huyo wa mambo ya kidiplomasia wa Misiri, na kulaani kuwa magaidi waliomteka nyara wanafanya shughuli za kigaidi kwa kisingizio cha "kulinda dini ya Kiislamu". Ikulu ya Misri imesisitiza kuwa matukio ya kigaidi kama hayo hayataathiri msimamo imara wa Misri ya kuiunga mkono Iraq na wananchi wake na kuwaunga mkono Waarabu na jitaihada zao.
Bw. Sherif alitekwa nyara tarehe 2 usiku magharibi mwa Baghdad. Tarehe 5, kundi la al-Qaeda la Jihad lilitoa taarifa kwenye tovuti likitangaza kuhusika na utekaji nyara huo; tarehe 6 mapema, leseni ya dereva ya Bw. Sherif, kitambulisho chake cha kazi cha wizara ya mambo ya nje na vitambulisho vingine vitano vilioneshwa kwenye tovuti kama ni ushahidi uliothibitisha kutekwa nyara kwake; baadaye kundi hilo lilitoa taarifa tena kwenye tovuti likisema litamuua.
Baada ya tukio hilo kutokea, serikali ya Misri ilikuwa inajaribu kumwokoa. Rais Hosni Mubarak tarehe 3 alitoa amri akimtaka waziri wa mambo ya nje Bw. Ahmed Abu Gheit afuatilie tukio hilo, na kumwarifu hali mpya kila baada ya muda mfupi; Wizara ya mambo ya nje ya Misri iliwasiliana na pande husika za Iraq kwa njia mbalimbali, na kuunda kikundi kilichoshughulikia tukio hilo, na kukitaka kifuatilie hali tukio hilo inavyoendelea na kuwasiliana mara kwa mara na idara za kidiplomasia za Iraq nchini Misri, ili Bw. Sherif aachiwe huru mapema iwezekanavyo.
Lakini, tarehe 7 alasiri kundi hilo lilitoa taarifa kwenye tovuti likitangaza kuwa limemwua Bw. Sherif. Taarifa hiyo imesema kuwa kundi hilo lilipata ushahidi kuhusu Bw. Sherif kuisaliti dini ya Kiislamu na kuwa rafiki wa wayahudi, na yeye alikiri ushahidi huo, hivyo kundi hilo lilimwua kwa mujibu wa "hukumu ya Mungu". Taarifa hiyo pia iliilaani vikali serikali ya Misri kupambana na waislamu wenye msimamo mkali.
Baada ya habari kuhusu kuuawa kwa Bw. Sherif kujulikana, jumuiya ya kimataifa imekilaani kitendo hicho cha magaidi. Katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu Bw. Amr Moussa tarehe 7 usiku alitoa taarifa akimsifu Bw. Sherif kuwa ni mwanadiplomasia hodari wa Misri na wa dunia ya kiarabu, amelinda maslahi ya taifa lake na ya Waarabu. Bw. Moussa alilaani vikali kuwa kitendo cha kumwua Bw. Sherif ni uovu mkubwa na upumbavu, na kimechafusha sifa ya dini ya Kiislamu. Ofisa wa ngazi ya juu kabisa wa Chuo Kikuu cha al-Azhar cha Misri, ambacho ni chuo kikuu maarufu zaidi cha kidini nchini Misri, Bw. Mohammed Seid Tantawi amesema kuwa watekaji nyara hao ni kundi la wahalifu wanaofanya ufarakanishaji kati ya Waislamu, lazima wataadhibiwa vikali kutokana na uovu wao.
Wachambuzi wanaona kuwa tukio la kuuawa kwa mwanadiplomasia wa Misri ni pigo kwa juhudi za kidiplomasia za utawala wa Iraq. Mwezi Juni misri ilisema kuwa itapandisha ngazi ya ujumbe wa kidiplomasia wa Misri nchini Iraq hadi kuwa ubalozi, na Bw. Sherif huenda angekuwa balozi. Misri ikiwa nchi kubwa ya kidiplomasia kati ya nchi za kiarabu, kama itaweza kuanzisha tena uhusiano wa kibalozi na Iraq na kupelekeana mabalozi, hali hiyo itaisaidia serikali ya mpito ya Iraq uhalali wake katika dunia ya nchi za Kiarabu na kuinua hadhi ya kidiplomasia ya Iraq. Lakini kuuawa kwa Bw. Sharif kutapunguza mwendo wa mchakato wa kuanzishwa tena uhusiano wa kibalozi kwa Misri na nchi nyingine za kiarabu na Iraq, na kuathiri mchakato wa ukarabati wa kidiplomasia wa Iraq.
Lakini kwa upande mwingine, vitendo vya kikatili vya magaidi wa kundi la al-Qaeda vitaongeza uungaji mkono wa Wairaq kwa mchakato wa kisiasa. Kutokana na tukio hilo, Wairaq watatofautisha shughuli za kupambana na ukaliaji na shughuli za ugaidi, na kushikamana zaidi na kuweka kando maoni tofauti ya madhehebu ya kidini, kufikiri tena na kusukuma mbele mchakato wa siasa ya kidemokrasia wa Iraq, ili kutimiza amani na utulivu nchini humo.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-08
|