Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-11 14:41:02    
Mwandishi chipukizi Wang Xiaoli

cri

Vitabu vya safari ya utalii au vitabu vya kueleza mandhari, mila na desturi katika nchi za ng'ambo havikosi kupatikana katika maduka ya vitabu, ingawa vitabu hivyo havionekani sana ndani ya vitabu chungu nzima. Lakini vitabu hivyo vikiwa katika mtandao wa internet mara vinaingia machoni mwa wanamtandao.

Kitabu cha "Burudika na Maisha ya Paris" kilichotangazwa kwenye mtandao wa internet mwanzoni mwa mwaka huu kinasomwa sana na wanamtandao wa internet. Kitabu hicho kinamwelezea mwanafunzi wa Beijing aliyesoma Ufaransa Bi. Wang Xiaoli jinsi alivyofurahia maisha alipokuwa Paris. Kwa maneno ya kawaida kimeeleza kwa hadithi fupi fupi zilizomkuta mwandishi huko Paris zinamfanya msomaji kama mwenzake anayefuatana naye katika maisha yake. Tofauti na vitabu vingine, kitabu hicho hakielezi yale majengo maarufu ya kale ambayo hayakosi kutajwa au kuelezwa kwa kirefu katika vitabu vingine, wala hakikusimulia maisha ya mwanafunzi huyo yalivyokuwa magumu, bali kimeeleza hisia zake na watu walivyoishi kwa raha mustarehe katika mji huo wa kisasa kabisa.

Mwandishi wa kitabu hicho ni msichana wa kawaida wa Beijing, lakini baada ya kumaliza elimu ya sekondari alifanya uamuzi usio wa kawaida kama wanafunzi wenzake, kwamba aliacha mtihani wa kujiunga na chuo kikuu bila kujali upinzani wa wazazi wake, na alianza kuishi bila shughuli maalumu. Baadaye, mnamo mwaka 2001 alikwenda Paris peke yake. Alipokuwa mtoto aliwahi kusikia hadithi nyingi kuhusu mji wa Paris na pia alisoma vitabu vingi kuhusu mji huo, aliona ni mji wa kisasa kabisa, na kila kitu ndani ya mji huo ni kizuri hata hewa. Kutokana na makala za majarida mengi, akilini mwake Paris ni pepo duniani. Siku moja waandishi wa habari walikutana na mwandishi huyo mwenye nywele ndefu nyeusi na kuongea kistaarabu. Alisema,

"Nilienda Ufaransa sio kwa ajili ya kujipatia elimu ya juu bali nilitaka kujifunza lugha ya Kifaransa. Nilipokuwa mdogo niliwahi kusikia watu wengine wakiongea Kifaransa. Niliona lugha hiyo inanivutia sana na sauti yake ina mvuto wa kijinsia. Naona msichana akiwa na sura nzuri na kuongea Kifaransa atakuwa wa kupendeza zaidi. Nilikwenda Ufaransa kutokana na tumaini hilo."

Lakini kinyume na alivyofikiri, hali ilikuwa mbaya sana katika mwaka wa kwanza alipokuwa Paris, hakusikia raha yoyote alipokuwa "peponi". Maisha aliyokuwa nayo yalikuwa upweke, alikuwa hajui lugha, hakuweza kujichaganya na Wafaransa, hali hiyo ilikuwa mbaya zaidi kwa kuwa alikuwa hajui kupika chakula, ilimpasa kila siku anunue chakula barabarani. Alikonda vibaya na mara kwa mara aliugua. Lakini alivumilia, ili atimize ndoto yake. Alipokumbuka maisha hayo, alisema,

"Maisha magumu katika mwaka wa kwanza yalinifanya nikomae. Naona mtu lazima awe mvumilivu wa shida, ukiwa katika hali mbaya unapaswa kujipa moyo na kusema 'nivumilie, nione hali itakuwa mbaya mpaka kiasi gani'. Sasa nikiwa katika kisiwa kitupu kilichotengwa, siwezi kusema nitaishi muda mrefu lakini nahakika ninaweza kuishi mwaka mzima."

Wang Xiaoli alijifunza Kifaransa katika chuo kikuu kimoja cha binafsi, baada ya mwaka mmoja aliweza kuongea Kifaransa kwa ufasaha. Kutokana na maendeleo ya lugha alifahamiana na marafiki wengi, eneo la maisha yake lilipanuka, na hakuona tena upweke. Mara kwa mara alikuwa akishiriki kwenye tafrija za marafiki zake na kutembelea madukani na kuzuru majengo maarufu na huku akiandika shajara ambayo ilikuwa msingi wa kitabu chake cha "Paris". Paris ni mji unaojulikana duniani kwa kumbukumbu zake za sanaa na majengo ya fahari, ni mji unaojulikana kwa maisha ya 'romantiki".Wang Xiaoli ana ufahamu wake kuhusu maisha ya "romantiki". Alisema,

"Maisha ya 'romantiki' ni hisia tu, kwa mfano ninapotembea barabarani, ghafla mvua ikinyesha, nitawasha sigara na kuendelea safari yangu kama mvua hainyeshi. Kama kuna baa ya kahawa basi nitaingia nipate kikombe kimoja cha kahawa au glasi moja ya mvinyo, naona hayo ndiyo maisha ya 'romantiki'."

Ndani ya kitabu cha "Paris" kuna picha nyingi, na zote zilipigwa na mwandishi mwenyewe, baada ya kumaliza kusoma kitabu hicho, wasomaji huona kama Parisi iko karibu nao. Wang Xiaoli aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kabla ya kwenda Paris alikuwa anapenda kupigwa picha, na baada ya kufika Paris alikuwa anapenda kupiga picha mwenyewe na amekuwa mpenda kupiga picha. Alisema,

"Naona picha zinanisaidia sana, baadhi ya mambo yanayonishinda kueleza nayaeleza kwa picha, kwa sababu unaweza kupiga picha hali uliyoiona kwa dakika, lakini ukieleza kwa maneno utashindwa kuyaeleza vilivyo."

Wang Xiaoli alisema, akiwa na fursa atakwenda ng'ambo kujifunza usanii wa kupiga picha, na kufanya maonesho ya picha zake. Na alisema kuwa, ataandika kitabu kingine, lakini kitabu hicho sio tena kueleza maisha yake ya raha mustarehe bali ni uchungu na uvumilivu wa maisha yake magumu mjini Paris.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-11