Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-11 14:48:35    
Luxembourg Yaunga Mkono Katiba ya Umoja wa Ulaya

cri

Tarehe 10 Luxembourg ilifanya upigaji kura kuhusu katiba ya Umoja wa Ulaya, na watu wengi wameunga mkono katiba hiyo.

Matokeo ya upigaji kura nchini Luxembourg ni kuwa zaidi ya 56% ya watu wanaunga katiba ya Umoja wa Ulaya na 44% wanapinga, ingawa kisheria matokeo hayo sio ya mwisho mpaka bunge la Luxembourg lipitishe, lakini kabla ya upigaji kura, bunge la Luxembourg lilikuwa limetangaza kuwa litaheshimu matokeo ya upigaji kura. Kwa hiyo Luxembourg imekuwa nchi ya kwanza kukubali katiba ya Umoja wa Ulaya baada ya Ufaransa na Uholanzi kupigia kura ya kuipinga.

Baada ya matokeo ya upigaji kura kutangazwa, waziri mkuu wa Luxembourg Jean-Claude Juncker alisema kuwa matokeo hayo yanamaanisha kuwa katiba ya Ulaya "bado haijafa", na matokeo hayo yataleta taathira nzuri kwa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya ambazo bado hazijafanya upigaji kura. Mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza pia walitoa pongezi kwa matokeo hayo, mkuu wa Chama cha Kisoshalisti katika bunge la Umoja wa Ulaya Bw. Martin Schulz alitangaza kuwa matokeo hayo yameupatia nafasi mpya mchakato wa kupitisha katiba ya Umoja wa Ulaya.

Wachambuzi wanaona kuwa matokeo ya Luxembourg kuikubali katiba ya Umoja wa Ulaya, kwa kiasi fulani yamepunguza wasiwasi unaoikabili katiba ya Umoja wa Ulaya.

Kwanza, Luxembourg ni nchi ndogo kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Lakini nchi hiyo ina nafasi yake isiyo ya kawaida katika Umoja huo, kwamba ni moja ya nchi waanzilishi wa Umoja huo, na siku zote inaunga mkono kithabiti mchakato wa kuungana kwa nchi za Ulaya. Kwa hiyo msimamo wa Luxembourg kuhusu hatima ya katiba ya Umoja wa Ulaya una maana nzito. Waziri mkuu wa Luxembourg aliwahi kusema kabla ya upigaji kura kufanyika, kwamba kama Luxembourg ikipinga, basi katiba ya Umoja wa Ulaya "kweli itakuwa imezikwa kabisa", alitumai kuwa Luxembourg itaitilia katiba hiyo uhai mpya.

Pili, matokeo hayo ya Luxembourg kukubali katiba yanawatia moyo wale waliounga mkono katiba hiyo. Baada ya Ufaransa na Uholanzi kuipinga katiba hiyo mwezi Mei na Juni, viongozi wa Umoja wa Ulaya walipaswa kusimamisha kwa muda taratibu za kupitisha katiba hiyo kwenye mkutano uliofanyika katikati ya mwezi Juni. Kisha nchi nyingi za Uingereza, Denmark na nchi nyingine zilitangaza kusimamisha au kuahirisha kutekeleza taratibu hizo za kupitisha katiba hiyo, lakini Luxembourg iliamua kupiga kura kama mpango ulivyowekwa. Zaidi ya hayo, waziri mkuu wa nchi hiyo Bw. Juncker aliahidi kuwa kama katiba hiyo haitapitishwa katika upigaji kura atajiuzulu. Hivi sasa, katiba hiyo imepitishwa, jambo hilo sio tu limewaletea matumaini watu waliounga mkono katiba hiyo, tena limembakiza waziri mkuu madarakani.

Lakini, matokeo ya Lixembourg sio matokeo ya mwisho wakati katiba hiyo inapokumbwa na wasiwasi mkubwa. Baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa hakika matokeo ya upigaji kura nchini Luxembourg yamepunguza wasiwasi huo, lakini hatima yake bado ni kitendawili. Kwa upande mmoja, nchi zilizosimamisha au kuahirisha upigaji kura hazijaamua lini zitaanza tena kutekeleza taratibu za kupitisha katiba hiyo. Kwa upande mwingine, ikiwa nchi zikatazopinga katiba hiyo zikizidi tano, basi katiba hiyo haitapona.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-11