Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-11 15:08:52    
Zhaoxian, mji mdogo wa kaskazini ya China

cri

Zhaoxian iko kusini ya kati mkoani Hebei, mji huo mdogo umekuwa na historia zaidi ya miaka 2500. Katika mji huo mdogo, Daraja la Zhaozhou lililojengwa zaidi ya miaka 1400 iliyopita na Hekalu la Bolinchan la kale yanajulikana nchini na ng'ambo.

Daraja la Zhaozhou liko kusini ya Zhaoxian, ingawa daraja hilo lina historia ya miaka mingi, lakini bado linaonekana ni daraja imara, ambalo ni daraja la mawe lililojengwa mapema zaidi na kuhifadhiwa kikamilifu zaidi kuliko mengine duniani.

Daraja hilo lilijengwa kwa mawe matupu, hivyo wakazi wa huko wanaliita kuwa ni "daraja kubwa la mawe". Umbo lake ni la nusu duara, usanifu maalum wa umbo la daraja hilo uliokoa matumizi ya mawe na kupunguza uzito wa daraja kwa tani 500 hivi, kutokana na kuweka duara mbili ndogo kwenye kila upande wa mhimili, hivyo ulipanua njia ya mtiririko wa maji chini ya daraja hilo, na kupunguza hatari ya mafuriko dhidi ya daraja na kuhakikisha usalama wa daraja. Katika zaidi ya miaka 1400 iliyopita, Daraja la Zhaozhou lilihimili mafuriko yaliyotokea mara 10, vurugu za vita mara 8 na tetemeko la ardhi lililotokea mara kadhaa, lakini daraja lenyewe bado ni ngumu na halikuharibiwa. Usanifu huo ulikuwa uvumbuzi wa kwanza katika historia ya ujenzi wa daraja duniani. Katika Bara la Ulaya, madaraja yenye umbo la nusu duara kama Daraja la Zhaozhou lilivyo, yalitokea kuanzia karne ya 18.

Kitabu cha historia kiliweka kumbukumbu kuwa, fundi maarufu Li Chun wa zama za kale za China aliongoza wafanyakazi wengine kujenga Daraja la Zhaozhou. Lakini watu wengi waliona kuwa, daraja hilo ni gumu sana, na haitakuwa rahisi kulijenga kwa kutegemea tu uwezo wa binadamu, hivyo wenyeji wa huko walisema kuwa daraja hilo lilijengwa na babu wa wajenzi wa China Lu Ban.

Wimbo wa kienyeji wa China unaoitwa "mfugaji mdogo wa ng'ombe" uliimba hivi:

Daraja la Zhaozhou lilijengwa na babu Lu Ban, mihimili ya mawe ya daraja yaletwa na malaika, na malaika Zhang Guolao na Caiwangye waliwahi kupita kwenye daraja hilo.

Bwana Zhao Guangge aliyeona daraja hilo kwa mara ya kwanza alivutiwa sana na daraja hilo akisema:

Naona daraja hilo kweli lilijengwa vizuri sana, limeonesha historia ndefu ya taifa la China na akili na uhodari wa wachina.

Hekalu la Bolinchan la Zhaoxian lilijengwa zaidi ya miaka 1700 iliyopita, hekalu hilo liko karibu kidogo na daraja la Zhaozhou, hili ni moja kati ya mahekalu ya kale zaidi nchini China. Katika hekalu hilo kuna ukumbi wa kuabudu sanamu za budhaa, na miti mingi ya misonobari ya miaka mingi. Mtalii Bibi Zhang Ron anapenda sana hekalu hilo akisema:

Nimekuja kwenye hekalu hili kwa mara ya pili, kwani naona hekalu hilo linaonesha utamaduni halisi wa dini ya budhaa.

Watalii wengi ambao walikuja kwenye hekalu hilo, siyo tu kuwa walikuja kwa ajili ya kuangalia majengo ya hekalu hilo, bali wanapenda kuwasikiliza masufii wa hekalu wakifahamisha kuhusu misahafu ya dini ya budhaa.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-11