Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-12 14:25:01    
Barua 0712

cri
       Msikilizaji wetu Ras Franzi Manko Ngogo wa Kemogemba CRI Listeners Club sanduku la posta 71 Tarime Mara Tanzania ametuletea barua pepe akisema kuwa, shukrani zake za dhati zitumiminikie hapo tulipo Beijing. Matokeo ya chemsha bongo juu ya ujuzi wa miaka 55 ya China mpya katika idhaa hii ya kiswahili yamempa moyo wa dhati wa kuzidisha bidii yake ya kushiriki na kuendelea kusikiliza CRI.

Ushindi wa Bwana Xavier Telly Wambwa wa Bungoma Kenya umedhihirisha nia thabiti ya CRI ya kushirikiana vyema na wasikilizaji wake na inavyowajali. Kwake yeye kupata nafasi ya kwanza kwa mara ya pili mfululizo kumemwongezea imani ya kuwa mvumilivu wa kila wakati na kuzidi kujipa moyo na kujikumbusha kauli mbiu ya Kemogemba, isemayo" Asili sio kushinda bali ni kupigana vizuri".

Anasema ama kwa hakika hatimaye pengine kwa majaliwa yake Mwenyezi huenda akaja kuwa miongoni mwa wale washindi ambao watakuja kuwa washindi wa kuja mjini Beijing mwaka 2006/2007 au hata mwaka mahususi wa safari ya kwenda Beijing China 2008 kuona mashindano ya Olimpiki.

Na mwisho anapenda kumpongeza Bwana Wambwa kwa kuja Beijing China na kuwawakilisha wasikilizaji hao wa idhaa ya kiswahili, hivyo anaomba wasikilizaji wenzake wakune vichwa ili wapigane vizuri kushindana na wasikilizaji wa idhaa nyingine ndipo washinde. Hatimaye angeomba e-mail ya Wambwa au simu yake ili aweze kuwasiliana naye juu ya ile zawadi yake.

Tunashukuru Bwana Ngogo kwa maelezo yake mazuri kuhusu matokeo ya chemsha bongo ya mwaka jana, tunamtakia mafanikio mema katika shindano lijalo. Na tumemtumia e-mail na kumwambia anuani ya Bwana Wambwa.

Na msikilizaji wetu mwingine Makoye Mazoya wa sanduku la posta 200 Magu Mwanza Tanzania anajiita katika barua yake kuwa Bingwa msikilizaji wa CRI nisiyekata tamaa Makoye Mazoya, anasema, anapenda kutoa shukrani nyingi ziwafikie watangazaji wa idhaa ya kiswahili kwa kazi nzito ya kila siku ya kuelimisha jamii. Yeye anazidi kupata ufahamu zaidi kupitia Radio China kimataifa ni kama jua kila mtu linamulika humu duniani.

Madhumuni ya bara hii ni kutushukuru kwa mafanikio ya kuchapisha jarida zuri la daraja la urafiki, amepata toleo la kwanza. Anashukuru sana. Kuhusu matokeo ya chemsha bongo mwaka 2004, matokeo yake ni ushindi kwa wote wanaoisikiliza idhaa ya kiswahili. Mkenya alichaguliwa, anampongeza sana kwa mafanikio hayo. Na anawaombea wote wanaosikiliza Radio China kimataifa wakae makini ili wapate mwanga zaidi.

Msikilizaji wetu George Njogopa ambaye barua zake huhifadhiwa na Clouds FM sanduku la posta 31513 Dar es Salaam Tanzania ametuletea barua pepe akisema kuwa, kwanza anatushukuru sote na pili anashukuru sana kwa majibu ya barua yake, majibu hayo ama hakika yamezidi kumpa matumaini kwamba pengine siku moja tunaweza kufanya kazi pamoja.

Anasema anaendelea kusoma sana taarifa zetu kwenye tovuti yetu ya Kiswahili, anaona ni habari zilizochambuliwa barabara, anapenda sana na hata yeye wakati mmoja mmoja anazitumia kwenye vipindi vyake vya habari, akikikariri chombo chetu kwamba ndicho kilichotoa taarifa hiyo.

Tunamshukuru sana Bwana George K. Njogopa, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kusoma makala mbalimbali za vipindi vyetu kwenye tovuti yetu ya mtandao wa internet, na kuwajulisha wengine kuhusu matangazo yetu.

Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai Falme za Kiarabu ametuletea barua akisema kuwa, moja kati ya janga kubwa linalomkabili mwanaadamu wa leo ni maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi. Leo hii angependa kutumia nafasi hii, kutuletea shairi fupi ambalo pia angependa liwekwe kwenye toleo lijalo la jarida letu la daraja la urafiki, shairi ambalo lina nasaha zake juu ya tahadhari za kujikinga na balaa hilo. Shairi hilo linasema :

Hodi hodi naingia, hebu nipeni nafasi

Nataka wasimulia , yatiayo wasiwasi

Ugonjwa umeingia, watisha bila kiasi

Ukimwi unatishia , uwasharati uwe basi !!!

Tukae na tukijua , tufanyayo ni maasi

Bila ya kufikiria , yote hayo ni mkosi

Mwisho tunajijutia, tushaingia nuhusi

Ukimwi unatishia, uwasharati uwe basi !!!

Lazima kuzingatia, tuseme nazo nafusi

Tuyaache mazoea, haraka tena upesi

Mauti yatunyemelea, tena yaja kwa kasi

Ukimwi unatishia, uwasharati uwe basi!!!

Tamati nimefikia, naifunga karatasi

Mema nimekusudia, wala kamwe si matusi

Ujumbe niliotoa, hakika ukweli halisi

Ukimwi unatishia, uwasharati uwe basi !!!

Tunamshukuru msikilizaji wetu Mbarouk Msabah kwa shairi lake linalotoa onyo kwa watu kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, hakika tutalichapisha kwenye jarida letu, ili wasikilizaji wetu wengi waweze kulisoma na kupata mafunzo.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-12