Msafara wa magari wa naibu waziri mkuu na waziri wa ulinzi wa serikali ya mpito ya Lebanon Bw Ilias Murr, tarehe 12 asubuhi ulishambuliwa kwa mabomu yaliyotegwa ndani ya gari kwenye mtaa wa waumini wa dini ya Kikristo kaskazini mwa Beirut. Tukio hilo limetokea kwa mara ya kwanza dhidi ya maofisa wa serikali na wanasiasa waliochukua msimamo wa kuipendelea Syria, tangu waziri mkuu wa zamani wa Syria Bw. Hariri alipouawa mwezi Februari mwaka huu.
Polisi wa Lebanon alisema kuwa mlipuko huo uliwaua watu wasiopungua wawili waliofuatana na Bw. Murr na kuwajeruhi wengine akiwemo mke wa balozi wa Mexico nchini Lebanon. Gari alilotumia Bw. Murr lilikuwa nyuma ya msafara wa magari, yeye mwenyewe alijeruhiwa kidogo tu usoni na miguuni. Bw. Ilias Murr alitoa taarifa fupi hospitalini akisema kuwa taifa liko katika wakati mgumu na watu wote wangevumilia na kujizuia.
Rais Emile Lahoud wa Lebanon na waziri mkuu mpya Fouad Siniora walikwenda hospitalini kumpa pole Bw. Murr. Bw. Siniora alisisitiza kwenye hospitali kuwa kitendo hicho kiovu hakitazuia mchakato wa wananchi wa Lebanon kujenga taifa na wananchi wataungana zaidi kwa ajili ya kuleta mustakbali mzuri. Rais Emile Lahoud alitoa taarifa katika usiku wa siku hiyo akisema kuwa waliozusha tukio hilo ni adui wa Lebanon, ambao wanafululiza kuwashambulia wazalendo kwa lengo la kuchochea migogoro ya kidini na kuitia Lebanon kwenye hali ya vurugu na hofu. Waziri mkuu wa baraza la mawaziri la mpito la Lebanon Bw. Nagib Miqati aliyekuwa ziarani nchini Ufaransa alirudi nyumbani mara moja na kuzitaka idara za usalama zifanye uchunguzi kwa haraka.
Baada ya mashambulizi hayo kutokea, Syria ilitoa taarifa haraka. Shirika la habari la Syria lilitoa taarifa likisema kuwa Syria inaona kuwa mlipuko huo ni kitendo cha kigaidi chenye lengo la kujaribu kuvuruga utulivu wa Lebanon na kudhoofisha umoja.
Bw. Ilias Murr atakayeondoka madarakani anaiunga mkono Syria kisiasa na ni mume wa binti wa rais wa sasa wa Lebanon. Baada ya Syria kukamilisha kuondoa jeshi lake kutoka Lebanon, rais Lahoud anayeiunga mkono Syria anashutumiwa na kundi linaloipinga Syria kwenye vyombo vya habari. Wachambuzi wanaona kuwa tukio la kumshambulia Bw. Murr huenda limefanywa na makundi yenye msimamo mkali yanayoupinga utawala wa Syria na kupigania uhuru kamili wa Lebanon dhidi ya rais Lahoud na watu wanaoiunga mkono Syria.
Lakini, tukio hilo limeimarisha nia ya watu wa hali mbalimbali wa Lebanon kulinda umoja wa taifa. Makundi mbalimbali yanayoipinga Syria ya Lebanon yote yalishutumu kitendo hicho. Kiongozi wa kundi linaloipinga Syria kwenye bunge Bw. Saad Al-Hariri alitoa taarifa akisisitiza kuwa bila kujali kuna tofauti gani kisiasa kwa watu wa Lebanon, wote wanapaswa kuungana na kupambana na jaribio lolote na kuzusha migogoro na kutishia utulivu wa jamii.
Idhaa ya kiswahili 2005-07-13
|