Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-13 18:38:46    
Makubaliano ya kusimamisha vita kati ya Palestina na Israel yajaribiwa na mlipuko wa mabumo ya kujiua

cri

Tarehe 12, mlipuko wa mabomu ya kujiua ulitokea huko Netanya, kaskazini mwa Israel, na kusababisha vifo vya wanawake watatu wa Israel na watu wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa. Huo ni mlipuko wa pili kutokea tangu Israel na Palestina zifikie makubaliano ya kusimamisha vita mwezi Februari mwaka huu, na athari ya mlipuko huo kwa hali tulivu kwa ujumla ya hivi sasa na mpango wa upande mmoja wa Israel inafuatiliwa na jumuiya ya kimataifa.

Tarehe 12 saa 12 na nusu mchana, kijana mmoja wa Palestina alilipua mabomu aliyokuwa nayo kwenye sehemu ya wapita njia ambayo ilikuwa imejaa watu karibu na duka kubwa la SHARON. Habari zimesema kuwa, kijana huyo alijaribu kuingia kwenye duka hilo, lakini kutokana na ulinzi mkali, aliacha mpango huo na kulipua mabomu njiani. Imefahamika kuwa kijana huyo ana umri wa miaka 18, anatoka Tulkarm, mji usio mbali na Netanya, kando ya magharibi ya Mto Jordan.

Baada ya mlipuko huo kutokea, jumuiya moja chini ya kundi la Jihad lilitangaza kuhusika na tukio hilo, pia lilisema kuwa litaendelea kulinda hali ya kusimamisha vita kati ya Israel na Palestina. Tangu mwezi Februari mwaka huu, kundi hilo limekuwa likitoa mara kwa mara taarifa zenye mgongano, likisema kuwa halitakukiuka makubaliano ya hivi sasa ya kusimamisha vita, lakini litalipiza kisasi kwa hatua za kijeshi za Israel.

Idara ya upelelezi ya Israel inaona kuwa kundi la Jihad limekuwa moja ya makundi yenye msimamo mkali na fedha za kutosha. Mwezi Februari mwaka huu, kundi hilo lilizusha mlipuko mmoja wa mabomu ya kujiua, na kusababisha vifo vya watu kadhaa. Katika mwezi uliopita, wanachama wa kundi hilo walishambulia makazi ya wayahudi kwenye ukanda wa Gaza, na kusababisha vifo vya wafanyakazi watatu kutoka nchi za nje, akiwemo mmoja kutoka China. Nusu saa kabla ya mlipuko huo kutokea mjini Netanya, mwanachama mmoja wa kundi hilo aliendesha gari lililojaa mabomu kuingia kwenye makazi ya wayahudi kwenye kando ya magharibi ya Mto Jordan, na kuligonga gari la jeshi la Israel na kulipuka, lakini halikusababisha vifo vya wayahudi. Idara ya upelelezi ya Israel imeona kuwa nguvu ya kundi hilo imefufuka katika miezi kadhaa baada ya kusimamishwa kwa vita kati ya Israel na Palestina, ingawa jeshi la Israel lililichukulia hatua za kijeshi mara nyingi, lakini halikuathirika sana.

Mwezi uliopita, wakati mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas alipokutana na waziri mkuu wa Israel Bw. Ariel Sharon alisema: "Kila risasi iliyofyatuliwa kwako ni kwangu vilevile." Hatua hiyo ya kundi la Jihad iliifanya mamlaka ya utawala wa Palestina ijitumbukize kwenye hali ya wasiwasi. Baada ya muda zaidi ya mwezi mmoja, Israel itaondoka kutoka kwenye ukanda wa Gaza, na Palestina itashika kwa pande zote madaraka ya ukanda huo miaka 12 baada ya kusainiwa kwa mkataba wa Oslo. Ingawa mpango wa kuondoka kwa Israel hauambatani kikamilifu na matarajio ya Palestina, lakini kama mpango huo utatekelezwa bila matatizo, utasaidia kuanzishwa kwa mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel, ambao unalingana na maslahi ya nchi hizo mbili. Hivyo, baada ya mlipuko uliotokea huko Netanya, Bw. Abbas alilaani kuwa kitendo hicho ni cha kijinga, pia ni uhalifu kwa wapalestina.

Baada ya kutokea kwa mlipuko huo, waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Shaul Mofaz aliitisha mkutano wa dharura na maofisa wanaoshughulikia mambo ya usalama, na kujadiliana namna ya kukabiliana na hali ya hivi sasa. Ofisa mmoja wa ofisi ya waziri mkuu wa Israel aliilaani mamlaka ya utawala wa Palestina kushindwa kuyadhibiti vizuri makundi yenye msimamo mkali ya Palestina, na kutishia kuwa Israel itachukua hatua kali. Lakini wachambuzi wanaona kuwa ingawa mlipuko huo umewafanya viongozi wa nchi hizo mbili wakabiliwe na tatizo kubwa, lakini kulinda hali ya amani kabla ya kuondoka kwa Israel kutoka kwenye ukanda wa Gaza kunaambatana na maslahi ya pande mbili, hivyo makubaliano ya kusimamisha vita kati ya nchi hizo mbili hayataharibika kutokana na mlipuko huo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-13