Baada ya kutangazwa kwa habari kuhusu kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya pande 6, pande mbalimbali zinazohusika zimeanza maandalizi yao ya kabla ya mkutano, na zimeahidi kuwa zitafanya juhudi kadiri ziwezavyo ili kuhimiza mazungumzo hayo yapate maendeleo halisi.
Katika ziara yake ya hivi karibuni nchini China, Japan na Korea ya kusini, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice alieleza mara kwa mara kuwa, duru jipya la mazungumzo ya pande 6 linapaswa kupata maendeleo halisi, Marekani inapenda kufanya juhudi ili kuyafanikisha. Na amesifu "pendekezo kubwa" la Korea ya kusini, na kuahidi kuwa kwenye mazungumzo ya kikazi kati ya Korea ya kusini na Marekani na wakati wawakilishi wakuu wa Korea ya kusini, Marekani na Japan kwenye mazungumzo ya pande sita watakapokutana watajadili namna ya kutumia ipasavyo "pendekezo kubwa" hilo la Korea ya kusini, tena kusawazisha misimamo na Marekani.
Wachambuzi wanaona kuwa, aliyoyaeleza Bibi Rice yameonesha tena kuwa Marekani itaonesha usuluhishi wake wa kiasi fulani kwenye duru jipya la mazungumzo ya pande 6, ili kuyafanya mazungumzo hayo yapate maendeleo fulani halisi.
Wajumbe wa Marekani na Korea ya kaskazini tarehe 9 walipowasiliana hapa Beijing walikubaliana kufanya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili ndani ya mazungumzo ya pande 6, hii pia ni ishara moja ambayo itasaidia Korea ya kaskazini na Marekani zijadiliane rasmi ana kwa ana kuhusu masuala halisi baada ya kuanzishwa kwa duru jipya la mazungumzo ya pande 6, pia inasaidia kuhimiza mazungumzo hayo yapate matokeo.
Baada ya kutangazwa kwa habari kuhusu kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya pande 6, Korea ya kaskazini pia imeeleza kuwa inapenda kufanya juhudi kadiri iwezekanavyo ili kuhimiza mazungumzo hayo yapate matokeo. Mazungumzo ya pande sita yamekuwa katika hali ya kukwama kwa miezi 13. Kutatuliwa mapema iwezekanavyo kwa suala la nyuklia la peninsula ya Korea kunalinga na mahitaji ya kimsingi ya maendeleo ya Korea ya kaskazini. Kutokana na hali ya kimataifa ya hivi sasa tunaweza kuona kuwa, duru jipya la mazungumzo ya pande 6 litakuwa fursa moja kwa Korea ya kaskazini, kama itatoa ahadi fulani kwenye mazungumzo hayo, itaisaidia kuaminiwa na kuungwa mkono na nchi nyingine duniani.
Juhudi za China pia ni umuhimu mwingine wa kuhimiza duru jipya la mazungumzo ya pande 6 yapate maendeleo. Mjumbe wa taifa wa China Bwana Tang Jiaxuan hivi karibuni akiwa mjumbe maalum wa rais Hu Jintao wa China yuko Korea ya kaskazini kwa ziara. Ziara yake hiyo inafanyika baada ya ziara ya China ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Rice. Wachambuzi wengi wameona kuwa, ikiwa nchi mwenyeji wa mazungumzo ya pande sita, hakika China itatumia ziara ya Bwana Tang kuhimiza duru jipya la mazungumzo ya pande 6 yapate maendeleo.
Wachambuzi pia wanaona kuwa, Korea ya kusini itaonesha umuhimu wake katika kuhimiza mazungumzo hayo yapate matokeo. Korea ya kusini na rafiki mshiriki wa Marekani, pia nchi hiyo iko kwenye peninsula ya Korea pamoja na Korea ya kaskazini, utatuzi wa suala la nyuklia la peninsula ya Korea unahusiana na maslahi halisi ya Korea ya kusini, hivyo nchi hiyo ikifanya juhudi zaidi itasaidia mazungumzo ya pande 6 yapate maendeleo.
Lakini hali halisi ni kuwa, duru jipya la mazungumzo ya pande 6 linakabiliwa na fursa ya kupata matokeo, na pia linakabiliwa na changamoto kubwa. Pande husika zinatakiwa kuonesha zaidi unyumbufu wao ndipo zitakapoweza kutumia fursa na kuhimiza mazungumzo hayo yapate matokeo mapema iwezekanavyo.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-13
|