Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-14 15:34:27    
Watoto Yatima wa Kivita wa Japan waliolelewa na wachina

cri

Zaidi ya miaka 60 iliyopita, vita ya uvamizi iliyoanzishwa na Japan dhidi ya Wachina ilisababisha vifo na majeruhi ya askari na raia wa China zaidi ya milioni 35, na hasara kubwa za kiuchumi. Mwaka 1945 baada ya Japan kushindwa vita, watoto yatima zaidi ya 5000 wa Japan waliachwa nchini China. Raia wa China waliwalea watoto hao yatima badala ya kulipiza kisasi kwa uvamizi wa Japan.

Bi. Shiobara Hachumi anayeishi mjini Tokyo anapendelea kuitwa kwa jina lake la kichina?Du Dongmei, kwa sababu alitunzwa na baba na mama wa China akiwa mtoto yatima. Mwezi Juni mwaka huu, kama kawaida, Bi. Hachumi alirudi nyumbani kwake katika mji wa Changchun, mkaoni Jilin, kaskazini mashariki mwa China kumwangalia mama yake mlezi wa China Bi. Yu Shifang. Anasema:

"nisingeweza kuwa na maisha mazuri kama ya leo, kama nisingekuwa na baba na mama walezi wa China. Hivyo siwezi kuwasahau."

Bi. Hachumi alikuwa mmoja kati ya watoto yatima wa Japan walioachwa nchini China. Zaidi ya miaka 60 iliyopita, ili kutimiza lengo la kuikalia China daima, Japan ilipoishambulia China, iliharakisha hatua ya kunyang'anya mali za China, na kuhamisha wajapan wengi katika mikoa mitatu ya kaskazini mashariki mwa China, na mkoa unaojiendesha wa kabila la mongolia ya ndani nchini China. Wazazi wa Hachumi walikuwa wahamiaji wa Japan miongoni mwao.

Mwaka 1945, baada ya kushindwa kwenye vita ya kuivamia China, askari na wahamiaji wa Japan walihangaika kuondoka China na kurudi nchini kwao. Ili kupunguza vikwazo vya kuondoka China, askari wakatili wa Japan waliwaua wanawake wa Japan na watoto wao njiani, hata kuwaamrisha kina mama kuwaua watoto wao wenyewe.

Bi. Nakamura Kiyoko anayeishi mjini Nagoya, Japan bado anakumbuka jinsi alivyonusurika na mauaji ya askari wa Japan. Anasema:

"Alasiri ya siku moja, askari wa Japan walikuja nyumbani kwangu wakiwa na panga mikononi, walitaka kutuua sisi sote wanawake na watoto wa Japan. Mama aliniambia mimi niliyekuwa na umri wa miaka 8 kwa wakati huo, na dada yangu mdogo tutoroke. Sisi tulinusurika, lakini mama yangu na kaka mdogo na dada mdogo mwingine wote waliuawa."

Takwimu husika zinaonesha kuwa, kutokana na wazazi kutoroka au kuuawa, watoto yatima zaidi ya 5000 wa Japan walibaki nchini China, kati ya watoto hao, mkubwa zaidi alikuwa na umri wa miaka 13, baadhi yao walikuwa wachanga kabisa.

Watoto hao yatima walioachwa na wazazi wa Japan au jamaa zao wote walichukuliwa na wakazi wa China na kutunzwa kwa upendo. Kwa kweli, raia wa China waliwachukiza sana wajapan, lakini walifahamu kuwa, ni serikali ya Japan iliyopenda kutumia nguvu za kijeshi katika mambo ya siasa na ilizusha vita dhidi ya wachina, watoto hao yatima hawakuwa na hatia yoyote. Hivyo waliwalea yatima hao kama watoto wao weneywe, wakati wakiweka chuki zao dhidi ya wavamizi wa Japan.

Vitendo vya wakazi wa China kuwalea watoto yatima wa Japan viliungwa mkono na serikali ya China mpya. Profesa Rong Weimu kutoka idara ya utafiti wa historia ya kisasa ya Taasisi ya Sayansi ya Jamii ya China alisema:

"Vita ya uvamizi ya Japan ilileta hasara kubwa sana kwa China, lakini serikali ya China ikifuata kanuni ya kibinadamu, haikuwa na ubaguzi dhidi ya yatima wa Japan, ilitoa msaada wa kimali kwa wachina waliowalea yatima hao."

Chini ya uangalizi wa serikali ya China na malezi mazuri ya wachina, watoto hao yatima wa Japan wote walikua, kuajiriwa na kujenga familia zao.

Mwaka 1972, uhusiano kati ya China na Japan ulifanyiwa kuwa wa kawaida, ambapo maingiliano ya kiraia yaliongezeka siku hadi siku. Baadhi ya yatima hao walitafutwa na kutambuliwa na jamaa zao wakarudi nchini Japan. Lakini hawakuweza kujizuia kuwakumbuka baba na mama walezi wao wa China, walikuja China mara kwa mara kuwatembelea.

Na Yatima wengine wengi walichagua kubaki nchini China kuishi pamoja na walezi wao. Bi. Wu Yun aliyeishi katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani jina lake la Kijapan ni Tachibana Akemi. Mwaka 1981 alirudi nchini Japan kumtembelea kaka yake mkubwa, lakini baada ya miezi mitano tu, alirudi China. Alisema kuwa, alipokuwa mtoto, ni baba na mama walezi wake wa China walimlea, sasa baba mlezi amefariki dunia, hawezi kumwacha mama yake mlezi aliyezeeka bila ya mtu kumtunza. Aliishutumu serikali ya Japan kwa kuzusha vita iliyowatumbukiza watoto wengi katika maisha ya msiba. Anasema:

"Vita ya uvamizi wa Japan dhidi ya China ilileta madhara makubwa si kwa watu wa China peke yake, bali pia kwa wajapan wenyewe. Familia elfu kadhaa kama yangu zilivunjika kutokana na vita hiyo."

Idhaa ya kiswahili 2005-07-14