Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-14 15:47:27    
Mlipuko watetemesha tena mji wa Baghdad

cri

Jeshi la Marekani nchini Iraq na polisi wa Iraq tarehe 13 walithibitisha kuwa mashambulizi ya kujiua kwa magari yenye mabomu dhidi ya jeshi la Marekani yalitokea siku hiyo kusini mashariki ya mji wa Baghdad, ambayo yaliwaua watu 27 wakiwemo watoto 24 wa Iraq na kuwajeruhi wengine wasiopungua 70. Jeshi la Marekani nchini Iraq siku hiyo lilitoa taarifa likisema kuwa katika mashambulizi hayo, askari mmoja wa jeshi la Marekani aliuawa na wengine watatu kujeruhiwa.

Watu walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa mashambulizi hayo yalitokea saa nne asubuhi, gari moja liitwalo Humvee la jeshi la Marekani lilikuwa likikaribia kundi la watoto wa Iraq na kuwapa. Peremende. Wakati huo mtu mmoja aliendesha gari aina ya Toyota Land Cruiser na kuligonga gari la jeshi la Marekani na kulipua mabomu. Daktari mmoja mjini Baghdad alisema kuwa miili ya watoto 24 waliokufa wenye umri kati ya miaka 10 hadi miaka 13, ilipelekwa hospitali.

Hili ni shambulizi kubwa la pili kufanyika mjini Baghdad katika wiki moja tangu tarehe 10 kituo kimoja cha kuwaandikisha askari mjini Baghdad kiliposhambuliwa kwa mabomu na kuwaua watu 25. Kuanzia mwezi Aprili mwaka huu serikali ya mpito ya Iraq ilipoundwa, Wairaq 1600 hivi wakiwemo akina mama na watoto wengi waliuawa katika mashambulizi mbalimbali.

Baada ya kutokea kwa mashambulizi ya tarehe 13, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alitoa taarifa kwa kupitia msemaji wake, akionesha kushtushwa na kushutumu vikali mashambulizi hayo. Taarifa hiyo inasema kuwa hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha kitendo hicho cha kiovu cha kuwaua raia na watoto, tena kitendo hicho hakiwezi kutimiza madhumuni yoyote. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Bw. Scott McClellan siku hiyo pia alishutumu vikali tukio hilo la kigaidi. Alisema kuwa watu wenye silaha wanajaribu kuharibu mchakato wa demokrasia wa Iraq, lakini hawana kisingizio chochote cha kuwaua raia na watoto.

Lakini Wairaq wengi hawawakosoi watu hao wenye silaha kwa mashambulizi hayo, wanaona kuwa shabaha ya watu hao wenye silaha ililenga jeshi la Marekani tu, lakini raia wa Iraq ni waathirika wakubwa kabisa na ukaliaji usio wa haki wa jeshi la Marekani nchini Iraq ni chanzo cha mashambulizi mfululizo yanayotokea baada ya vita vya Iraq. Kwa hiyo raia wa Iraq wanataka jeshi la nchi nyingi linaloongozwa na Marekani litunge ratiba ya kuondoka mapema iwezekanavyo.

Sasa, baadhi ya Wairaq wana wasiwasi kuhusu hali ya usalama ya Iraq katika siku za baadaye.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-14