Saa 4 za tarehe 13 asubuhi kwa saa za huko, mlipuko ulitokea tena katika mji mkuu wa Iraq Baghdad. Mlipuko huo wa kujiua uliolenga gari la jeshi la Marekani umesababisha vifo vya watoto 24 wa Iraq, na watoto wasiopungua 18 kujeruhiwa.
Baada ya mlipuko huo kutokea, mwandishi wetu wa habari wa Mashariki ya Kati Bw. Jin Lixi alitoa ripoti akisema:
"Polisi ya Iraq ilisema kuwa, tarehe 13 asubuhi saa 4 hivi, mshambulizi wa kujiua aliendesha lori na kulipua gari la kijeshi la 'Humvee' la Marekani. Kwa kuwa wakati huo kulikuwa na watoto wengi wa Iraq mbele ya gari la jeshi la Marekani, hivyo tukio hilo lilisababisha vifo na majeruhi ya watoto wengi. Jeshi la Marekani nchini Iraq siku hiyo lilitoa taarifa likisema kuwa, mlipuko huo pia ulisababisha kifo cha askari wa Marekani, na askari wengine watatu wa Marekani kujeruhiwa."
Daktari wa Baghdad alifahamisha kuwa, watoto hao 24 wote walikuwa na umri kati ya miaka 10 hadi 13. Mtu aliyeshuhudia tukio hilo alisema kuwa, vifo vingi vya watoto vilitokea kutokana na kuwepo kwa watoto wengi wa Iraq mbele ya gari la kijeshi la Marekani.
"Jeshi la Marekani mara kwa mara linawapa zawadi watoto ili kuwashawishi. Jeshi la Marekani pia linawafanya watoto kuwa ngao yao, hivyo katika mlipuko huo, askari wa jeshi la Marekani waliouawa au kujeruhiwa wachache, lakini na watoto waliouawa na kujeruhiwa ni wengi."
Baada ya mlipuko huo kutokea, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alitoa taarifa kupitia msemaji wake akishtushwa na tukio hilo na alililaani vikali. Taarifa hiyo ilisema kuwa, hakuna kisingizio chochote kinachoweza kutetea kitendo hicho kiovu cha kulenga raia na watoto wasio na hatia yoyote, na kitendo hicho cha kigaidi hakiwezi kutimiza lengo lolote. Msemaji wa ikulu ya Marekani Bw. Scott McClellan siku hiyo pia alilaani vikali tukio hilo, na kusema kuwa tukio hilo linaonesha kuwa watu wenye silaha hawajali maisha ya watu wasio na hatia, wala maisha ya binadamu. Alisema, watu wenye silaha walijaribu kuharibu mchakato wa demokrasia ya Iraq, lakini hawana kisingizio chochote cha kuwaua raia wasio na hatia, hasa watoto.

Lakini, Wairaq wengi hawaoni uhalifu huo ulifanywa na watu wenye silaha. Wanaona kuwa, shabaha ya watu wenye silaha ni jeshi la Marekani tu, lakini watu wa Iraq wamedhuruwa vibaya. Kuikalia Iraq bila sababu za haki kwa jeshi la Marekani ni chanzo cha Iraq kukumbwa na mashambulizi mengi ya kigaidi bila kusita baada ya vita. Hivyo, watu wa Iraq wanalitaka jeshi la nchi nyingi linaloongozwa na Marekani liweke ratiba ya kuondoka mapema iwezekanavyo, na kuondoka baada ya jeshi la Iraq kuweza kulinda amani.
Lakini, bila ya kujali nani angewajibika na mlipuko huo, ushenzi na ukatili wa vita ni hali halisi isiyofutika, hasa vita inasababisha madhara makubwa kwa raia wasio na hatia, hususan wanawake na watoto.
Hili ni tukio kubwa la pili la mashambulizi ya kigaidi lililotokea huko Baghdad ndani ya wiki moja tokea tukio la mlipuko wa mabomu uliosababisha vifo vya watu 25 kwenye kituo kimoja cha kuandikisha askari tarehe 10 huko Baghdad, vilevile ni shambulio lililosababisha vifo na majeruhi ya watoto wengi tokea mwezi Septemba mwaka jana.
Madhara ya vita si kama tu yanahusiana na afya za watoto, madhara mabaya zaidi ni kwa roho za watoto, na kuleta athari ya muda mrefu kwa saikolojia ya watoto. Watoto wanaokua katika mazingira ya vita wanaweza kuona kuwa dunia hii haina usalama, madhara ya kawaida huleta athari mbaya kwa ukuaji na afya za watoto.
Juhudi zinatakiwa kufanyika ili kuwawezesha binadamu wawe mbali na vita, na kuifanya vita iwe mbali na watoto. Hii ni kwa ajili ya watoto, pia ni kwa ajili yetu.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-14
|