Mkutano wa 59 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 12 ulimaliza majadiliano wa hadhara juu ya mswada wa azimio uliotolewa na Japan, Ujerumani, Brazil na India kuhusu upanuzi wa baraza la usalama. Majadiliano ya siku mbili yameonesha kuwa, kuna migongano mikubwa kati ya pande mbalimbali za Umoja wa Mataifa kuhusu mswada huo, nchi nyingi zinaona kuwa haifai kuupiga kura mswada huo kwa haraka katika kipindi cha hivi sasa.
Katika majadiliano hayo yaliyoanzia tarehe 11, wajumbe wa nchi 49 walitoa hotuba. Miongoni mwa nchi 5 wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama, Marekani, China na Russia zimeeleza bayana kupinga kupiga kura kwa haraka kuhusu mswada huo.
Mshauri maalum wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani kuhusu suala la mageuzi ya Umoja wa Mataifa Bibi Tahir Kheli tarehe 12 alipotoa hotuba alisema kuwa, Marekani haioni kuwa mswada huo utasaidia kuimarisha kazi ya Umoja wa Mataifa. Amezitaka nchi mbalimbali ziupige kura ya hapana mswada huo. Bibi Tahir Kheli alieleza kuwa, katika wakati wowote, Marekani inapinga pendekezo lolote la mageuzi litakaloweza kudhoofisha ufanisi wa baraza la usalama, pia inapinga kulazimisha kupiga kura kuhusu pendekezo lolote ambalo halijaungwa mkono na nchi nyingi zaidi na ni vigumu kutekelezwa. Alisema, Marekani inaona kuwa katika kipindi cha hivi sasa, baraza kuu la Umoja wa Mataifa halipaswi kulipigia kura pendekezo lolote kuhusu upanuzi wa baraza la usalama,
Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Bwana Wang Guangya alidhihirisha kuwa, nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kuzingatia kulinda mshikamano na maslahi ya siku za usoni ya Umoja wa Mataifa, na kufanya juhudi kubwa kadiri ziwezavyo kuepuka kutoa masharti ya mwisho kuhusu suala la upanuzi wa baraza la usalama katika hali isiyopevuka.
Bwana Wang Guangya alisema kuwa, kuwalazimisha watu kuupigia kura mswada usiopevuka hakika kutasababisha mfarakano kati ya nchi wanachama na makundi ya kikanda, na kudhoofisha heshima na umuhimu wa Umoja wa Mataifa. Hii imekwenda kinyume na nia ya mageuzi ya baraza la usalama. Hivyo China inapinga kithabiti kuweka kikomo cha muda kwa mageuzi ya baraza la usalama, na kupinga kuwalazimisha watu kuupigia kura mswada ambao bado una migongano mikubwa.
Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa Andrey Denisov alisema kuwa, upigaji kura wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa haupaswi kusababisha mfarakano kati ya nchi wanachama, na kudhoofisha kazi na umuhimu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la usalama kutokana na hayo. Alisema, kufanya mageuzi ni kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa baraza la usalama, na kuleta uwiano zaidi kati ya nchi wajumbe wa Baraza la usalama. Russia inapinga kithabiti kupanua haki ya kupiga kura ya turufu. Hatua kama hiyo na nyingine yoyote ya kudhoofisha hadhi ya nchi tano wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama zilizopo kwa hivi sasa kamwe haziwezi kukubaliwa.
Wajumbe wa Indonesia, Uturuki, Canada, Mexico, Korea ya kusini, Hispania na Costa Rica pia walitoa hotuba na kuukosoa mswada wa azimio uliotolewa na nchi nne.
Mbali na hayo, kundi la "mshikamano wa kutafuta maoni ya pamoja", Umoja wa Afrika na Marekani pia zimetoa miswada yao ya azimio na pendekezo. Majadiano hayo yameonesha zaidi kuwa, migongano kati ya nchi mbalimbali kuhusu upanuzi wa baraza la usalama haijapungua bali inaelekea kupanuka. Hivyo hivi sasa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa bado halijaamua kufanya majadiliano mapya kuhusu mswada wa azimio uliotolewa na nchi 4 za Japan, Ujerumani, Brazil na India.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-14
|