Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-18 16:21:04    
Saddam Hussein atasomewa mashitaka mahakamani

cri

Mahakama maalum ya Iraq inayoshughulikia kesi za maofisa waandamizi wa utawala wa zamani wa Iraq tarehe 17 ilidokeza kuwa, mahakama hiyo imetoa mashitaka ya kwanza kwa rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein na kutangaza tarehe ya kumfikisha mahakamani kumsomea mashitaka katika siku kadhaa zijazo. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Saddam kufikishwa mahakamani kusomewa mashitaka tangu mwaka 2003 alipokamatwa.

Jaji mkuu wa mahakama maalum ya Iraq Bw. Raed Juhi tarehe 17 alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Baghdad kuwa uchunguzi kuhusu kesi ya kijiji cha Dujail uliofanywa na mahakama hiyo kwa Saddam na maofisa wengine watatu waandamizi wa utawala wa zamani wa Iraq umemalizika na mahakama itatangaza tarehe ya kuwafikisha mahakamani kuwasomea mashitaka katika siku kadhaa zijazo. Kutokana na ratiba ya hukumu ya Iraq itatumia muda usiopungua mwezi mmoja na nusu tangu washitakiwa watakaposomewa mashitaka hadi kuhukumiwa. Kwa hiyo, Saddam atapelekwa mahakamani kusomewa mashitaka mapema ya mwezi Septemba mwaka huu.

Tukio la kijiji cha Dujail ni kesi ya zamani iliyotokea mwaka 1982. Mwaka huo, Saddam alipopita kwenye kijiji hicho cha waumini wa madhehebu ya Shia kilichoko kaskazini mwa Baghdad nusura auawe. Baada ya siku kadhaa, kijiji hicho kilishambuliwa kwa hatua ya kulipiza kisasi na wanakijiji wasiopungua 50 waliuawa. Mwezi Juni mwaka huu, mahakama maalum ilionesha video ambayo jaji mkuu Juhi alikuwa akisikiliza mashitaka ya Saddam na maofia wengine waandamizi.

Tangu mwishoni mwa mwaka 2003, Saddam amekuwa akishikiliwa katika kambi ya jeshi la Marekani iliyoko mjini Baghdad na kulindwa na askari wengi, huku akisubiri kusomewa mashitaka. Lakini katika suala la kumhukumu Saddam, mahakama hiyo ilikabiliwa na mashinikizo mbalimbali, kwa hiyo mahakama hiyo imeshughulikia kesi hiyo kwa tahadhari na kuchagua kesi isiyo ngumu, hivyo tukio la kijiji cha Dujail limechukuliwa kama ni jaribio kabla ya kuhukumu kesi nyingine kubwa. Zaidi ya hayo, Marekani haiungi mkono kumhukumu Saddam kwa haraka. Sababu ya Marekani ni kuwa jambo la haraka la serikali ya mpito ya Iraq ni kukamilisha kazi ya kutunga katiba ya taifa kabla ya katikati ya mwezi Agosti, ili raia wapige kura kuhusu mswada wa katiba hiyo kabla ya mwezi Desemba uliopangwa. Lakini wachambuzi wanaona kuwa sababu kweli ya Marekani kupinga kumhukumu Saddam kwa haraka ni kuwa, Marekani ina wasiwasi kuwa Saddam atatoa hadharani mambo ya aibu ya Marekani kuuunga mkono utawala wa Saddam miaka ile katika mchakato wa kumsomea mashitaka Saddam, na itaifanya Marekani ijitie katika hali mbaya.

Lakini viongozi wa kundi la Kurd na madhehebu ya Shiah waliokandamizwa na Saddam kwa muda mrefu wanataka kulipiza kisasi haraka baada ya kushika utawala wa Iraq, kwa hiyo wana malalamiko kwa Marekani kuahirisha kumhukumu Saddam.

Wachambuzi wanaona kuwa kumsomea mashitaka Saddam kwa mahakama maalum ya Iraq ni hatua muhimu ya kwanza ya kuwahukumu Saddam na maofisa wengine waandamizi wa utawala wa zamani wa Iraq. Kwa kuzingatia msimamo wa Marekani, ni dhahiri kuwa hatua hiyo itafanywa kama ni jaribio.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-18