Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-18 21:17:29    
Maonesho Makubwa ya Maadhimisho ya Miaka 600 Tokea Zheng He Asafiri Baharini Yafanyika Mjini Beijing

cri

Miaka 600 iliyopita msafiri mkubwa wa China ya kale, Zheng He aliuongoza msafara mkubwa wa merikebu kusafiri mbali baharini na alisafiri mara saba katika muda wa miaka 28, na kufika kwenye nchi zaidi ya 30. Kitendo chake kilikuwa cha ujasiri mkubwa, chenye watu wengi na teknolojia ya hali ya juu, na safari yake ilikuwa ya mbali.

Tarehe 11 Julai ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 600 tokea Zheng He asafiri kwa mara ya kwanza. Ili kukumbuka mchango wake mkubwa katika historia ya usafiri baharini, siku hizi shughuli nyingi na za aina mbalimbali zinafanyika nchini China, moja kati ya shughuli hizo ni "Maonesho ya Miaka 600 ya Zheng He Kusafiri Baharini". Hayo ni maonesho makubwa yenye vitu vingi vya kumbukumbu. Naibu waziri wa mawasiliano wa China Bw. Huang Xianyao kwenye ufunguzi wa maonesho alisema,

"Miaka 600 iliyopita kitendo cha Zheng He kusafiri mbali baharini kilitingisha ulimwengu, na leo miaka 600 baadaye jumba la makumbusho la taifa la China linaonesha hali ilivyokuwa ya safari ya Zheng He kwa vitu vilivyosalia na kuonesha kiwango kikubwa cha utengenezaji wa merikebu na teknolojia ya hali ya juu katika zama zake. Tokea enzi na dahari, China ni taifa linalopenda amani, nchi nyingi za Asia ya Kusini Mashariki mpaka sasa zinahifadhi vitu na alama zilizobaki za Zheng He, na kwa njia mbalimbali zinamkumbuka mjumbe wa utamaduni na amani. Maonesho hayo yana lengo la kufahamisha kuwa China ni taifa linalopenda amani na ujirani mwema."

Kwenye ukumbi wa maonesho, sampuli tatu kubwa za merikebu zinaonekana kama zikisafiri mbele ya picha kubwa ya bahari ya buluu. Kutokana na maelezo, sampuli hizo tatu zimetengenezwa kwa kuiga merikebu aliyotumia Zheng He. Kwenye maonesho kuna vitu zaidi ya 80 vilivyokuwa katika safari za Zheng He na picha karibu 200 ambazo zimeonesha jinsi Zheng He alivyokuwa maishani na alivyosafiri baharini na msafara wake.

Maonesho pia yameonesha mahali alipozaliwa mkoani Yunnan, kusini mwa China. Zheng He jina lake la awali ni Ma Sanbao, alizaliwa mwaka 1371 katika ukoo wa kabila la Wahui, alikuwa ni muumini wa dini ya Kiislamu. Baadaye Zheng He alikuwa towashi aliyekuwa karibu na mfalme Zhu Li katika kasri la kifalme. Kutokana na mchango wake mfalme alimpatia jina la Zheng He badala ya jina lake la awali. Mwaka 1405 kwa kufuata amri ya mfalme aliuongoza msafara wake kusafiri mbali baharini.

Kwenye maonesho, ramani ya njia aliyosafiri iliyopanuliwa inaonesha wazi miji, visiwa na njia za baharini na jinsi dira ilivyotumika katika safari zake saba. Katika ramani hiyo, majina ya sehemu yalitiwa alama zaidi ya 500, na kati ya majina hayo sehemu za nje ya China zilikuwa 300, ambazo tokea mji wa Saigon wa Vietnam, Cambodia, Sri Lanka, Maldive hadi Kenya, jumla ya nchi 30 ziliandikwa kwenye ramani hiyo.

Kutokana na uchunguzi wa maandishi ya kale kulikuwa na zaidi ya njia 40 alizosafiri, umbali wa jumla wa njia hizo ulikuwa maili za bahari laki 1.6, ni safari yenye watu wengi na ya mbali kabisa duniani katika enzi za kale. Lakini jambo la kusikitisha ni kuwa mafaili yanayohusu safari yalichomwa moto. Kwenye maonesho mpini wa usukani wenye urefu wa mita 11 unawashangaza watazamaji, mpini wenyewe unatosha kueleza kwamba merikebu yenyewe ilikuwa kubwa sana. Mpini huo ulifukuliwa mwaka 1957 kwenye mahali palipokuwa na kiwanda cha kutengeneza merikebu karibu na mji wa Nanjing, kwenye mwisho wa mpini huo kuna alama ya kuunganisha usukani, urefu wa alama hiyo ni mita 6, yaani usukani wenyewe ulikuwa na urefu wa mita sita. Mwelezaji wa maonesho Bi. Wang Hong alisema,

"Vitu vya kihistoria vinavyohusika na Zheng He moja kwa moja ni vichache, mpini huo uligunduliwa katika mahali palipokuwa na kiwanda cha kutengeneza merikebu ya uongozi karibu na Nanjing, lakini hatuna uhakika kama mpini huo wa usukani ndio uliokuwa kwenye merikebu ya Zheng He, hata hivyo mpini mrefu kama huo unatosha kutuambia kuwa merikebu yenyewe ilikuwa kubwa sana.."

Kutokana na maandishi ya kihistoria, kila mara msafara wa Zheng He ulikuwa na merikebu kiasi cha mia moja, na kati ya merikebu hizo, merikebu ya uongozi iliyotumiwa na Zheng He ilikuwa na urefu wa mita 126, upana mita 51 na nafasi za kuondoa maji tani elfu 15 na uwezo wa kubeba mizigo tani elfu 7.

Kwenye maonesho, picha kubwa iliyochorwa katika Enzi ya Ming "Ustawi wa Mji wa Nanjing" na picha yenye urefu wa mita 24 ya "Ustawi wa Mji Mkuu" zote zimeonesha hali ilivyostawi katika miaka aliyoishi Zheng He nchini China. Kutokana na picha hizo kuna matangazo ya biashara "Bidhaa za Kimashariki na Kimagharibi Zote Zapatikana", na mahekalu ya Zheng He yaliyokuwa katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia, na watu wa nchi hizo walivyomheshimu Zheng He kama ni mjumbe wa amani. Sababu za Zheng He kupata heshima kubwa kama hiyo ni kuwa akiwa mjumbe wa China alitekeleza sera za amani na ujirani mwema, ingawa wakati huo Enzi ya Ming ilikuwa na nguvu kubwa, na msafara wa merikebu za Zheng He ulipita zaidi ya nchi 30 lakini haukunyakua ardhi hata inchi moja, na badala yake alieneza urafiki wa kuheshimiana kidini na kiutamaduni.

Ingawa msafiri mkubwa Zheng He anajulikana kwa wote wa China, maonesho yake yanawavutia watu wengi na hasa wanafunzi ambao wako likizoni sasa. Mwanafunzi aliyetoka mbali alisema, aliwahi kusoma historia ya Zheng He katika shule, lakini maonesho hayo yamempa ufahamu mpya kuhusu msafiri huyo mkubwa, anaona Zheng He ni fahari ya Watu wa China. Alisema,

"Nimeelewa zaidi historia ya safari ya mbali baharini ya Zheng He, na pia nimeelewa zaidi jinsi Zheng He alivyokuwa. Kwa kweli ilikuwa si rahisi kwa Zheng He na kuongoza watu wengi kusafiri mbali, alikuwa anataka kueneza utamaduni wa China nje ya nchi na kuingiza utamaduni wa nje nchini China. Kwa kweli alikuwa mtu shupavu."

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-18