|
Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 60 na jumuyia za kimataifa wakiwemo wajumbe wa Benki ya Dunia walihudhuria mkutano huo wa siku mbili. Lengo la mkutano huo ni kupima kazi za ukarabati zilivyokuwa tokea vita vya Iraq kuanza hadi hivi sasa, na kujumulisha uzoefu na mafunzo yaliyopatikana katika miradi ya kusaidia ukarabati na kujadili namna ya kukabiliana na matatizo yaliyotokea katika miradi ya ukarabati.
Tarehe 24 Juni mwaka 2003 Umoja wa Mataifa ulifanya mkutano usio rasmi katika makao makuu ya Umoja huo, mkutano huo ulijadili mpango wa ukarabati na ujenzi wa miundombinu nchini Iraq. Huu ulikuwa ni mkutano wa kufungua mazungumzo ya kuidhamini Iraq. Tarehe 23 Oktoba mwaka huo, chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, mkutano wa kuisaidia Iraq ulifanyika katika mji wa Madrid, Hispania. Wajumbe wa nchi mbalimbali waliahidi kutoa misaada ya dola za Kimarekani bilioni 33 kabla ya mwaka 2007, na mkutano huo ulianzisha mfuko wa kuisaidia Iraq ili kuhakikisha fedha za msaada zinatumika ipasavyo.
Lakini waziri wa mpango wa Iraq aliyehudhuria mkutano huo Bw. Barham Saleh alisema, hivi sasa miundombinu ya maji, umeme na kuondoa majichafu na elimu imekuwa katika hali mbaya ambayo haikuwahi kutokea katika miongo kadhaa iliyopita, na inahitaji misaada ya jumuyia ya kimataifa. Alitumai kuwa nchi hizo zitatekeleza ahadi zao haraka iwezekanavyo.
Imefahamika kuwa ingawa nchi hisani zimetoa ahadi za misaada mikubwa, lakini ni ahadi chache tu zilizotekelezwa, na kati ya fedha hizo zilizopatikana nyingi zilitumika katika shughuli za ulinzi wa maslahi ya nchi za nje nchini Iraq, hivi sasa akiba katika Benki ya Dunia haikuzidi dola za Kimarekani bilioni moja. Sababu muhimu za kutotimiza fedha zilizoahidiwa na nchi mbalimbali ni mbili. Moja ni kuwa hali ya Iraq haijatengemaa, milipuko inatokea siku hadi siku, matukio ya utekaji nyara hayaishi na shughuli za uchumi hazifanyiki katika hali ya kawaida; vikundi vyenye silaha dhidi ya Marekani vinaharibu mabomba ya mafuta. Sababu nyingine ni kuwa ufisadi umeshamiri na usimamizi wa kazi ni mbovu, hivyo nchi hisani zina wasiwasi kuwa fedha zao zitapotea bure. Bw. Barham Saleh alisema wazi kuwa suala la ufisadi nchini Iraq ni "tishio kubwa" ambalo linazuia nchi hisani kutoa fedha zao.
Nchi iliyoandaa mkutano huo, Jordan, inatumai kutoa mchango mkubwa katika ukarabati wa Iraq. Nchi hiyo ikiwa ni jirani ya Iraq ina uhusiano mkubwa wa kiuchumi na Iraq. Tarehe 18 waziri mkuu wa Jordan alipohotubia mkutano alisema, Jordan lazima isaidie Iraq ipite kipindi chake cha taabu na kurejesha hadhi yake inayostahili katika kanda iliyopo. Aliahidi kuwa Jordan itasaidia Iraq kufufua uchumi kadiri iwezavyo, utulivu wa jamii na siasa. Lakini kwa kweli Jordan inakabiliwa na shida nyingi baada ya kuzuka kwa vita nchini Iraq. Ilipoteza misaada ya mafuta kutoka Iraq, na sasa inavumilia maisha ya taabu kwa kutegemea mafuta za nchi za Ghuba. Katika hali kama hiyo ambayo mkono unaweza tu kukuna mahali unapofikia, Jordan haitaweza kuisaidia sana Iraq.
Mkutano huo wa nchi zinazofadhili ukatabati wa Iraq hautafanikiwa sana, hata hivyo mafanikio madogo yalipatikana. Benki ya Dunia ilisema kuwa katika muda wa miaka 27 iliyopita kwa mara ya kwanza benki hiyo ilitoa mkopo kwa Iraq, mkopo huo wenye fursa nafuu wa dola za Kimarekani milioni 500 na kulipwa baada ya miaka 10 utatumika katika miradi inayohitajika sana nchini Iraq. Benki ya Maendeleo ya Kiislamu na serikali ya Iraq pia zilitia saini mkataba ambao benki hiyo itatoa msaada na mkopo wa dola za Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Iraq.
Idhaa ya kiswahili 2005-07-18
|