Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-19 21:02:27    
Barua 0719

cri

        Kuanzia tarehe 10 hadi 17 mwezi Julai, ujumbe kutoka Zanzibar Tanzania ukiongozwa na waziri wa nchi katika ofisi ya waziri kiongozi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna ulifanya ziara ya wiki moja hapa nchini China. Ukiwa hapa Beijing ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea Radio China kimataifa, kituo cha telelevisheni CCTV na shirika la habari la China Xinhua. Walipokuwa hapa Radio China kiimataifa, mtagazaji wetu Fadhili Mpunji alipata fursa ya kumhoji Mheshimiwa Shamuhuna.

F: Mheshimiwa waziri, wewe sijui ni mara yako ngapi kuitembelea China. Ningependa nijue picha yako ya jumla ya China jinsi ulivyoiona, na jinsi ulivyoifikiria kabla ya kuja kwako hapa China.

W: Hii ni mara yangu ya tatu kuitembelea China. Na nimebahatika mara zote tatu nilikuja kwa kufanya kazi na sio kutalii. Mara kwanza nilikuja na marehemu makamu wa rais Dk.Omari Ali Juma, wakati alipokuwa waziri kiongozi wa Zanzibar. Tulikuja hapa kutangaza uanzishaji wa biashara, uanzishaji wa vitega uchumi pale Zanzibar, ambapo Zanzibar tulianzisha maeneo huru. Sisi tuliona eneo kubwa linaweza kufanya kazi pale Zanzibar au kuwekeza pale Zanzibar kwenye eneo la nguo, yaani textile industry, kwa hivyo tunaona nchi ambazo zimepata ujuzi mkubwa, ni nchi za . Tukatembelea sehemu nyingine, tukaishia Hong Kong, na kumaliza ziara yetu nchini China. Hiyo ilikuwa ni safari ya kwanza, safari ya pili nilibahatika kuja na rais wa Jamhuri, na tulikuja mwaka wa 1999, kukuza mawasiliano zaidi na kutia saini mkataba wa ushirikiano, na nilipata nafasi ya kufika pale Tiananmen Square, na katika jengo kubwa la mikutano pale Tiananmen ndiko tulikosaini mkataba. Na sasa mara ya tatu nimeongoza ujumbe huu kama nikiwa ni waziri katika ofisi ya waziri wa kiongozi, lakini ninayeshughulikia mambo ya habari, utangazaji, na si mambo haya tu bali pia nashughulikia mambo ya uchaguzi, mambo ya bunge letu, eneo la mambo ya ukimwi na mambo ya dawa. Haya ndio mambo hasa ninayoshughulikia kama waziri kwenye ofisi ya kiongozi, lakini sekta ya habari ndiyo inayochukua muda mkubwa sana katika kazi zangu kutokana na umuhimu wake. Kwa sababu sekta hiyo inahitaji kukuzwa zaidi. Kila ninapokuja China naona China inabadilika, na nakuta Beijing imekuwa kwa haraka sana. Najua kwa nini China inabadilika, kwa sababu nimesoma kwenye magazeti, kwenye mitandao, kwenye majarida kwamba, China sasa imetoka katika uchumi tunaouita wa kisaili, uchumi wa kujitegemea kwa kujifunga ndani, yaani closed economy, na wameingia katika uchumi wa soko huria, na katika uchumi wa namna hii, kwa nchi kama ya kichina, yenye watu wengi, yenye wataalum wengi, wanaweza kuweka ushindani mkubwa katika soko la dunia, na kufanya vizuri sana katika biashara zao, na ndiyo maana mpaka sasa hivi hata Marekani kwenye sekta ya nguo, inayumba ikihangaishwa na China. Kwa sababu, China katika sekta hiyo ina nguvu kubwa ya ushindani, wamejiandaa vya kutosha, wana nguvu kazi ya kutosha na nzuri, na wana uwezo mkubwa wa kuanzisha vitega uchumi vya namna hiyo, na kutokana na ujuzi wao, na gharama ndogo ya uzalishaji wanatoa ushindani mkubwa katika soko la dunia, ndio maana hata nchi nyingine duniani, zinaogopa ushindani kutoka China, na ndiyo maana nasema China imebadilika, ile China ya zamani kila nikija naikuta imebadilika, tena mabadiliko yenyewe ni ya kwenda kwa haraka sana. Kwa sababu, malezi waliyopata wachina ni kufanya kazi, na kuacha maneno mengi, wanafanya kazi sana wanajituma, hiyo ndiyo imeleta mabadiliko makubwa ya China.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-19