Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-20 14:39:18    
Iraq na Nchi za Jirani Zaimarisha Ushirikiano wa Usalama

cri

Mkutano wa pili wa mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za jirani na Iraq tarehe 19 ulifanyika mjini Istambul,Uturuki. Taarifa ya mkutano huo ilisisitiza kuwa nchi hizo zitaimarisha ushirikiano wa usalama ili kupambana kwa pamoja na ugaidi na kulinda usalama na utulivu wa kikanda.

Mkutano huo ulifanyika wakati hali ya usalama ya Iraq inazidi kuwa mbaya. Licha ya waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki, nchi iliyoandaa mkutano huo, mawaziri wa mambo ya ndani kutoka Iraq, Bahraini, Saudi Arabia, Kuwait, Misri, Syria na Iran pamoja na wajumbe wa Umoja wa Mataifa walihudhuria mkutano huo na kujadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa usalama nchini Iraq.

Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano ilisema kuwa, nchi zote hizo zinapaswa kuimarisha mapambano dhidi ya ugaidi na kuimarisha upashanaji habari kuhusu magaidi, na kukaza dhibiti wa sehemu za mipakani ili kuzuia magaidi kuanzisha vituo katika nchi nyingine na kuandikisha wafuasi, kupanga shughuli za ugaidi, na kusaidiana katika uchumi. Taarifa inataka kesi ya rais wa zamani wa Iraq, Sadaam, na maofisa wake waandamizi isikilizwe mapema. Mkutano huo umeamua kuwa mkutano wa tatu wa mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi jirani za Iraq utafanyika katika mji wa Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, na tarehe ya mkutano huo itapangwa baada ya majadiliano.

Waziri wa mambo ya ndani wa Iraq Beyan Jabbor Salagh aliridhika na mafanikio ya mkutano huo. Alisema, mkutano umepata maoni ya namna moja katika majadiliano. Kati ya maoni hayo, mawili yalikuwa muhimu. Moja ni kuanzisha sekretarieti. Imefahamika kuwa ofisi hiyo itawekwa katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, na kazi yake ni kusimamia utekelezaji wa uamuzi uliofanywa na mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani. Maandalizi ya ofisi hiyo yatashughulikiwa na Uturuki. Pili, nchi zote zilizoshiriki kwenye mkutano huo zinataka kesi ya Sadaam na maofisa wake waandamizi isikilizwe mapema.

Katika muda mrefu uliopita, Uturuki ilikuwa inashambuliwa na kutishiwa na vikundi vyenye silaha vya chama cha wafanyakazi wa Kurd. Tokea mwaka 1984 vikundi vyenye silaha vya chama cha wafanyakazi cha Kurd vilipofanya mashambulizi makubwa, raia na askari zaidi ya elfu 30 wa Uturuki walipoteza maisha, na hivi karibuni vikundi hivyo vimeanza tena shughuli zao na kutishia usalama wa Uturuki. Na hali mbaya zaidi ni kuwa watu wenye silaha wa chama cha wafanyakazi cha Kurd elfu 5 wamejificha milimani katika sehemu ya kaskazini ya Iraq. Kwa hiyo Uturuki inatumai kuwa Iraq itachukua hatua za kuwazuia watu hao wasiingie nchini Uturuki.

Kuhusu matakwa ya Uturuki waziri wa mambo ya ndani wa Iraq Jabbor Salagh alisema kuwa, Iraq haiungi mkono vikundi vya ugaidi ikiwa ni pamoja na chama cha wafanyakazi cha Kurd. Lakini alisisitiza kuwa Uturuki ikichukua hatua dhidi ya vikundi vyenye silaha vya chama cha wafanyakazi cha Kurdi ndani ya mpaka wa Iraq lazima ipate ruhusa ya Iraq.

Iran na Iraq zote ni nchi zenye waislamu wengi. Lakini vita vilivyopiganwa kwa miaka minane katika karne iliyopita kati ya nchi hizo mbili vilisababisha vifo vya watu zaidi ya milioni moja, na nchi hizo mbili zimekuwa na uhasama. Waziri wa mambo ya ndani wa Iran Mossavi Lari alisema, Iran inaunga mkono ukamilifu wa ardhi wa Iraq na kupenda kutoa msaada kwa ajili ya utulivu wa Iraq. Kadhalika, Iran inaunga mkono ushirikiano wa mapambano dhidi ya ugaidi na kuchukua hatua za kuzuia kujipenyeza kwa magaidi mipakani. Msimamo huo wa Lari umeonesha matumaini ya Iran kutaka kuboresha uhusiano na nchi jirani za Kiarabu.

Wachambuzi wanaona kuwa ingawa nchi zote zilizoshiriki kwenye mkutano huo zina maoni ya namna moja katika kuimarisha ushirikiano wa usalama, lakini kutokana na kuwa Iraq inatofautiana na nchi nyingine katika mkakati, kwa hiyo ushirikiano wa usalama hautakuwa shwari kama unavyotazamiwa.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-20