Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-20 15:14:46    
Uundwaji na umaalum wa serikali mpya ya Lebanon

cri

Waziri mkuu wa Lebanon Bw. Fouad Siniora tarehe 19 alitangaza kuunda serikali mpya baada ya kushauriana na rais Emile Lahoud. Hii ni serikali ya kwanza iliyoundwa baada ya kuondoka nchini Lebanon kwa jeshi la Syria. Waziri mkuu huyo alieleza kuwa uundwaji wa serikali mpya ni kamili na alieleza matumaini yake kuwa baraza jipya la mawaziri litatumia madaraka yake likiwa kikundi chenye umoja na kukabiliana na changamoto kubwa.

Orodha ya mawaziri wa serikali mpya imetolewa kwa kuzingatia maslahi za makundi mbalimbali ya Lebanon. Waziri mkuu Siniora siku zote amejitahidi kuunda baraza la mawaziri tangu mwishoni mwa mwezi Juni alipoteuliwa kuwa waziri mkuu wa serikali mpya. Pendekezo la kwanza kuhusu uundwaji wa baraza la mawaziri alilomtumia rais lilipingwa na baadhi ya makundi kwenye bunge. Pendekezo la pili kuhusu kuunda serikali ya wataalam na watu wasio wa vyama pia halikukubaliwa na bunge na rais. Mapema ya tarehe 19, rais Lahoud ambaye ni muumini wa madhehebu ya Maronite ya kikristo alikataa orodha ya mawaziri 24 iliyotolewa tarehe 15 na waziri mkuu Siniora na kuona kuwa idadi ya mawaziri wa madhehebu ya Maronite ni ndogo sanaa na kumtaka Siniora afanye marekebisho kuhusu mawaziri watakaoteuliwa. Usiku wa siku hiyo, Siniora na Lahoud walishauriana tena na kutoa pendelezo la nne. Pendekezo hilo lilikubaliwa na rais Lahoud usiku huo na kutangazwa hadharani.

Serikali mpya inaundwa na mawaziri 24 na kila upande wa Wakristo na Waislam unachukua nusu ya idadi hiyo. Naibu waziri mkuu wa serikali ya awamu iliyopita ambaye pia alikuwa waziri wa ulinzi Elias Murr na waziri wa mambo ya ndani Hassan Al-Sabaa wataendelea kushika madaraka hayo na Fawzi Salloukh wa mwislam wa madhehebu ya Shiah atakuwa waziri wa mambo ya nje.

Serikali mpya ya Lebanon ina umaalum wa aina tatu. Wa kwanza ni kuwa chama cha Hizbullah kimejiunga na serikali kwa mara ya kwanza. Marekani siku zote inakichukulia chama hicho kuwa ni kundi la kigaidi na azimio nambari 1559 la baraza la usalama pia linataka wanamgambo wote wa chama hicho nchini Lebanon wasalimishe silaha. Wanachama wa Hizbullah wameingia kwenye baraza jipya la mawaziri, jambo ambalo lina maana ya kutambua hadhi halali ya chama hicho kwenye jukwaa la kisiasa la Lebanon. Bw. Siniora alieleza baada ya kutangaza orodha ya baraza la mawaziri kuwa anaona fahari kwa wanachama wa Hizbullah kuingia kwenye baraza hilo, chama hicho kina msingi mkubwa kwa umma kwenye sehemu kadhaa nchini Lebanon na hali hiyo ingeonekana katika serikali bila matatizo.

Wa pili, waungaji mkono wa waziri mkuu wa zamani Bw Hariri wanakuwa uti wa mgongo katika serikali. Katika serikali mpya, mawaziri 15 ni wa makundi yanayoipinga Syria yanayoongozwa na mtoto wa Hariri Bw. Saad Al-Hariri.

Wa tatu, hakuna waungaji mkono wa Michel Aoun, kiongozi wa kundi linaloipinga Syria. Kwa hiyo, watu wana wasiwasi kuwa Michel Aoun akiwa nguvu kubwa ya madhehebu ya Kristo bila shaka atakuwa kwenye kundi la upinzani katika bunge na huenda atakuwa chanzo cha hali ya kutokuwepo kwa utulivu katika mchakato wa kisiasa wa siku za usoni nchini Lebanon.

Idhaa ya kiswahili 2005-07-20