Milipuko minne ilitokea tena tarehe 21 mjini London, ambapo mitatu ilitokea katika subway na mmoja mwingine ulitokea katika basi. Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote kuhusu kuuawa au kujeruhiwa ila mtu mmoja tu aliyejeruhiwa kidogo. Baada ya wiki mbili tangu milipuko iliyotokea tarehe 7 mwezi Julai mjini London, mfululizo wa milipuko hiyo iliwatetemesha tena watu mjini London.
Wataalam wa usalama wa Uingereza wanaona kuwa tukio la tarehe 21 linafanana na milipuko ya tarehe 7 Julai ila tukio hilo ni dogo zaidi. Kwa hiyo wataalam wanaona kuwa milipuko hiyo ilifanywa na kundi jingine la washambulizi kwa kuiga milipuko ya tarehe 7 Julai. Wataalam wengine wanaona kuwa mashambulizi hayo yalifanywa na magaidi wanaohusika na kundi la Al-Qaeda, lakini polisi walieleza kuwa ni mapema sana kuzungumzia matukio hayo mawili.
Baada ya milipuko iliyotokea wiki mbili zilizopita, kwa upande mmoja, polisi waliwasaka magaidi kwa makini na kwa upande mwingine, polisi waliwaonya raia wasilegeze tahadhari kwa kutokea tena kwa mashambulizi ya ugaidi, Tukio la tarehe 21 limethibitisha kuwa ingawa polisi na idara za upelelezi ziko katika hali ya tahadhari, magaidi bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi mapya.
Kwa kuwa watu wana wasiwasi kuhusu usalama wao, watu wanataka kujua kuwa kwa nini London imeshambuliwa tena. Siku mbili kabla ya kutokea kwa tukio la tarehe 21, ofisi ya utafiti wa mambo ya kimataifa ya Uingereza ilitoa ripoti ikiainisha kuwa tukio la milipuko ya London linatokana na ushiriki wa Uingereza kwenye vita vya Iraq. Uingereza inaifuata Marekani nyayo kwa nyayo katika suala la Iraq, hivyo Uingereza imekuwa shabaha ya magaidi. Ofisi hiyo ilibashiri kuwa tukio kama hayo huenda litatokea tena mjini London. Uchunguzi mpya wa maoni ya raia wa Uingereza unaonesha kuwa theluthi mbili za Waingereza wanaona kuwa tukio la tarehe 7 Julai linahusika na vita vya Iraq na theluthi moja ya Waingereza wanaona kuwa waziri mkuu Tony Blair anapaswa kuwajibika kutokana na tukio hilo.
Lakini Tony Blair alikanusha tena na tena kuwa mashambulizi ya kigaidi yanahusika na vita vya Iraq.
Siku moja kabla ya kutokea kwa milipuko ya tarehe 21, waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Bw. Charles Clarke alitangaza hatua mpya za Uingereza kupambana na ugaidi, zikiwemo namna kuzuia itikadi potovu isiathiri Waislam vijana nchini humo na kuweka orodha kuhusu watu wenye msimamo mkali duniani. Wachambuzi wanaona kuwa kutokea tena kwa milipuko mjini London kunaonesha kuwa kama serikali ya Blair haitarekebisha sera yake katika suala la Iraq, basi hata hatua za kupambana na ugaidi zitafanywa kwa makini namna gani, Uingereza huenda itaendelea kuwa shabaha itakayoshambuliwa na magaidi.
Idhaa ya kiswahili 2005-07-22
|