Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-22 22:02:08    
Makazi ya China Kwenye Stempu

cri

China ina maeneo mapana na makabila mengi. Kutokana na tofauti za mazingira asilia na jadi mbalimbali za utamaduni, makazi ya watu katika sehemu mbalimbali yanatofautiana kabisa kiujenzi. Katika hali ya maendeleo ya ujenzi wa kisasa na kuongezeka siku hadi siku kwa nyumba zenye ghorofa nyingi, makazi ya kijadi ya mitindo mbalimbali pamoja na mila na desturi za kienyeji vikiwa ni sehemu ya mirathi ya utamaduni wa taifa la China vinazidi kupendwa na wananchi wa China. Walimu na wanafunzi wa Idara ya Mapambo ya Chuo Kikuu cha Sanaa na Uchoraji walichagua "makazi ya watu" kuwa ujumbe katika usanifu wao wa stempu. Chini ya maelekezo ya Prof. Chen Hanmin, Li Zhongfe, Hua Jianxin na He Jie walisanifu "michoro ya makazi ya watu" ambayo iliteuliwa na Kamati ya Uteuzi wa Michoro ya Stempu ya Wizara ya Posta na Simu na kuchapishwa kuwa stempu. Kuanzia mwaka 1986, stempu 21 za "Makazi ya China" zikiwa katika seti nne zilifululiza kutolewa katika nchi nzima ya China. Stempu za "Makazi ya China" zilisifiwa sana nchini na pia nchi za nje. Washabiki wengi wa stempu walionyesha hamu ya kuzitunza na washabiki wa Japani waliziteua stempu hizi kuwa stempu bora kabisa zilizotolewa na China mnamo mwaka 1986.

Stempu hizi zilionyesha kwa usahihi mazingira ya watu wanaoishi katika sehemu mbalimbali za China. Wasanifu walitumia kwa uangalifu kila mbinu za uchoraji na kila rangi katika michoro midogo ya stempu ili kuonyesha vilivyo hali pekee za kikabila. Sifa-bainifu moja ya stempu hizi ni kwamba kila stempu inatumia rangi moja tu. Wasanifu walitumia uzito tofauti wa rangi moja kuonyesha mandhari ya mbali na ya karibu kwenye mchoro wa stempu. Mbinu hii imeifanya michoro ya stempu hizi iwe na uzuri wa kiasili.