Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-22 22:03:43    
Vipuzi vya miti

cri

Katika wilaya ya Tancheng, mkoa wa Shandong kuna kijiji maarufu kinachojulikana nchini kote kwa utengenezaji wake wa vipuzi vya miti. Kijiji hicho si kingine isipokuwa ni Kijiji cha Fannian. Wanakijiji wa huko wamerithi ufundi wa kutengeneza vipuzi vya namna hii kutoka kwa mababu zao vizazi kwa vizazi. Takriban watu wote?wanaume kwa wanawake, wazee kwa vijana?wanafahamu ufundi huo.

Vipuzi vya Fannian hutengenezwa kutokana na miti ya Chinese parasol, poplar na willow kwa njia ya kuviringisha. Vipuzi vimekuwa vikivuma kwa miaka mingi kwa kuwa vina maumbo sahili ya kikale na ya kiajabu. Katika misimu isiyo na shughuli nyingi za kilimo, wakulima hutengeneza vipuzi vyao. Ndani ya nyua na vyumba huwa mmejaa vikapu vya vipuzi. Wakati huu, wateja kutoka kwenye sehemu nyingine huja kufanya maagizo ya bidhaa.

Aina za vipuzi zinavuka 10, zikiwemo vijisanamu vya binadamu, magurudumu ya kusokotea nyuzi, watoto wanaopanda magari na mikuki. Mtoto anayepanda gari, ni sanamu ambayo mtoto mtundu husimama juu ya gari huku akipiga upatu kwa mkono na ngoma kwa mguu. Vikifuatana na uzungukaji wa magurudumu, upatu na ngoma hulia pamoja. Kijisanamu cha binadamu, kichwa chake hukubali kuzunguka, macho na masikio yanaweza kugeuka kulia na kushoto, na tumbo lake hutoa mlio. Wazee wa vijiji vya karibu huenda kwenye kijiji hicho kununua, baadhi ya vipuzi kwa ajili ya watoto wao.

Utengenezaji wa vipuzi huhitaji makumi ya hatua. Zana za kuviringisha hutengenezwa na mafundi wa kienyeji, na sehemu zote za zana hizo ni za miti isipokuwa kekee na gololi. Zana hizo zinaweza kuviringisha vitu na kutoboa matundu. Kuhusu upakaji rangi, mafundi kwanza hupaka rangi nyekundu, ya manjano au nyeupe kwenye vipuzi ikiwa ni rangi ya msingi. Kisha, huchora nakshi za rangi mbalimbali zilizochangywa na gundi. Nakshi zilizochorwa kwa ustadi mkubwa huonekana kama zinajitokeza nje.