Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-25 15:36:18    
Misri yaharakisha uchunguzi kuhusu milipuko iliyotokea mjini Sharm el-Sheikh

cri

Baada ya kutokea kwa mfululizo wa milipuko katika mji wa utalii Sharm el-Sheikh, idara za usalama na uchunguzi za Misri zimefanya msako mkali dhidi ya watuhumiwa na kuharakisha uchunguzi.

Kikosi cha usalama cha Misri tarehe 24 kiliendelea kufanya msako mkali, na kuwakamata watuhumiwa. Idara ya usalama ya nchi hiyo ilidokeza kuwa, baada ya kuwakamata watuhumiwa 30 tarehe 23, kikosi chake tarehe 24 kiliendelea na msako katika peninsula ya Sinai, na kuwakamata watuhumiwa wengine 60, lakini hadi sasa, bado hakuna mtu yeyote aliyeshitakiwa kuhusika na milipuko hiyo.

Wachunguzi wa Misri walisema kuwa, matokeo ya mwanzo ya uchunguzi yanaonesha kuwa, tukio hilo halina uhusiano moja kwa moja na milipuko ya London iliyotokea tarehe 7 na 21 mwezi huu, lakini polisi wa Misri walishuku kuwa, milipuko hiyo huenda inahusiana na tukio la mlipuko wa Taba lililotokea mwezi Oktoba mwaka jana huko peninsula ya Sinai. Mlipuko wa Taba ulisababisha vifo vya watalii wa Israel zaidi ya 30.

Idara za usalama na uchunguzi za Misri tarehe 24 zilimaliza ukusanyaji wa ushahidi, na zitafanya ufafanuzi na utafiti pamoja na vikundi vya usalama kutoka Uingereza na Marekani.

Hivi sasa watu wa vikundi viwili wanashukiwa kuhusika na milipuko ya Sharm el-Sheikh, yaani kundi la Al-Qaeda na vikundi vyenye siasa kali vya kidini nchini Misri.

Milipuko hiyo ya mfululizo ilitokea katika tarehe ya kuadhimisha miaka 53 ya siku ya taifa la Misri. Washambulizi walifanya milipuko hiyo kwa lengo la kuleta athari mbaya na kuleta pigo kwa serikali. Utalii ni chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni nchini Misri, pia ni sekta binafsi inayotoa nafasi nyingi za ajira, mashambulizi makubwa yaliyotokea katika mji wa Sharm el-Sheikh, ambao ni mji maarufu wa utalii bila shaka yataleta uharibifu mkubwa kwa sekta ya utalii kwa nchi hiyo. Kushuka kwa utalii kutaathiri vibaya sekta ya mambo ya fedha, kuharibu uchumi wa nchi hiyo, na kuongeza tatizo la ukosefu wa nafasi za ajira nchini Misri.

Watu wamegundua kuwa, tukio hilo mjini Sharm el-Sheikh linahusiana na hali mbaya duniani ya mapambano dhidi ya ugaidi. Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, matukio ya mashambulizi dhidi ya watalii wa ng'ambo na maofisa wa serikali yalitokea mara kwa mara nchini Misri. Baada ya tukio la Luxor lililotokea mwaka 1997, serikali ya Misri ilichukua hatua kali kulinda usalama katika sehemu za utalii, na kuchukua sera ya kufarakanisha nguvu za upinzani ikiwemo nguvu zenye siasa kali za kidini, na kupata mafanikio mazuri. Lakini baada ya tukio la "9.11", baadhi ya nchi zilichukua sera ya umwamba kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, na kutumia vigezo mbili tofauti, matokeo yake ni kuwa hali ya mashariki ya kati imezidi kuwa wasiwasi, na tofauti kati ya dunia ya Kiislamu na nchi za magharibi zimeongezeka. Katika hali hiyo, labda watu wanaweza kufahamu, ni kwa nini Misri yenye uhusiano mzuri na nchi za magharibi inakumbwa na mashambulizi ya milipuko ambayo ni makali kabisa katika miaka 10 iliyopita.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-25