Duru la 4 la mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea linatazamiwa kufanyika tarehe 26 hapa Beijing, China. Hivi sasa ujumbe wa pande 5 za Korea ya kaskazini, Korea ya kusini, Marekani, Japan na Russia umefika Beijing, ambapo wawakilishi wao wamefanya mawasiliano, pande zote zinatarajia mazungumzo hayo yatapata matokeo halisi.
Ofisa wa Wizara ya mambo ya nje ya China na mtaalamu wa masuala ya Asia na Pasifiki wanaona kuwa, duru jipya la mazungumzo ya pande 6 linalenga kupata maendeleo halisi, lakini kutokana na hali ya utatanishi na vipengele ya suala la nyuklia la peninsula ya Korea, pande mbalimbali zinatakiwa kuwa na uvumilivu wa kutosha na kuendelea na juhudi zenye taabu.
Suala la nyuklia la peninsula ya Korea lililoonekana dhahiri kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2002 limeathiri vibaya amani na utulivu wa peninsula ya Korea na sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki. Serikali ya China ilifanya usuluhishi kati ya pande mbalimbali, na kuanzia mwezi Agosti mwaka 2003, pande 6 za China, Korea ya kaskazini, Marekani, Korea ya kusini, Japan na Russia zilifanya duru tatu za mazungumzo kuhusu utatuzi wa suala hilo. Kwenye mazugumzo hayo, pande mbalimbali zilipata maoni muhimu kuhusu kutatua suala la nyuklia la peninsula ya Korea kwa njia ya amani, ambapo pande hizo husika zilifanya majadiliano kuhusu masuala muhimu na pia kutoa mapendekezo ya utatuzi wa masuala hayo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bwana Liu Jianchao hivi karibuni alieleza matarajio juu ya duru jipya la mazungumzo ya pande 6 akisema:
Pande mbalimbali zinaweza kufanya mawasiliano wakati wa kufanya mazungumzo hayo, pia zinaweza kubadilsihana maoni kwa njia mbalimbali. Lengo ni moja tu yaani kuelewa kwa kina msimamo wa upande mwingine, ili kuongeza maoni ya pamoja kwa kiasi kikubwa. Mazungumzo ya pande 6 yanalenga kuifanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na nyuklia, hivyo masuala yote yanayohusika na lengo hilo yanaweza kujadiliwa kwenye mazungumzo hayo. Suala la kuifanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na nyuklia ni suala lenye utatanishi mkubwa, tukitaka kutatua suala hilo tunatakiwa kuwa na uvumilivu wa kutosha, na kuelewa ipasavyo utatanishi na vipengele vya suala lenyewe na kufanya maandalizi ya lazima, ili kufanya juhudi kubwa zenye taabu kwa ajili ya utatuzi wa suala hilo.
Mkurugenzi wa ofisi ya utafiti wa masuala ya Asia na Pasifiki katika Idara ya utafiti wa masuala ya kimataifa ya China Bwana Jin Linpo alidhihirisha kuwa, ni vigumu kufikia makubaliano ya kimsingi kwenye mazungumzo ya pande 6 ni kwa sababu ya kuwa pande mbili Korea ya kaskazini na Marekani hazikuweza kuaminiana, Korea ya kaskazini inaona kuwa sera ya Marekani juu ya Korea ya kaskazini inalenga kuupindua utawala wa nchi hiyo, na Marekani inaona kuwa si rahisi kwa Korea ya kaskazini kuweza kuacha mpango wa nyuklia. Bwana Jin alisema:
Korea ya kaskazini imeahidi kuwa hatimaye itaweza kuacha mpango wa nyuklia, lakini maana ya "hatimaye" haieleweki wazi; kwa upande wa Marekani na jumuiya ya kimataifa, ingawa zimeahidi kutoa msaada kwa Korea ya kaskazini, lakini msaada huo wa kiuchumi ama ahadi ya usalama, bado hazieleweki kihalisi. Kama mapendekezo ya pande hizo mbili yatawekwa kwa makini na kihalisi zaidi, itakuwa ni rahisi kwa pande husika kufanya majadiliano, na tena itasaidia zaidi kusukuma mbele mazungumzo ya pande 6.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-25
|