Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-26 21:06:56    
Kwanini Rumsfeld amekwenda Asia ya Kati?

cri

Waziri wa ulinzi wa Marekani Bw. Donald Rumsfeld tarehe 25 alifunga safari ya kwenda Kyrgyzstan kwa ziara ya siku 3 katika Asia ya kati. Alikuwa na mpango wa kuwa na mazungumzo na rais mteule Kurmanbek Bakiyev wa nchi hiyo tarehe 26. Halafu baadaye atakwenda Tajikistan. Hiyo ni ziara ya pili ya Bw. Rumsfeld katika Asia ya kati katika muda wa miezi minne. Wachambuzi wanaona kuwa lengo la ziara yake hiyo ni kuisihi Kyrgyzstan ikubali Marekani kudumisha kituo chake cha kijeshi nchini humo.

Asia ya kati iko sehemu ya kati, kati ya mabara mawili ya Asia na Ulaya, sehemu hiyo ina raslimali nyingi za mafuta ya asili ya petroli na gesi ya asili, hivyo ni sehemu muhimu sana katika mambo ya kijeshi. Tokea muda mrefu uliopita nchi za Asia ya kati zilikuwa katika eneo la taathira ya Jumuiya ya madola huru (CIS) inayoongozwa na Russia, ambalo ni udhaifu wa mpango wa kivita wa dunia nzima wa Marekani. Tangu kulipuka vita vya Afghanistan mwaka 2001, Marekani ikitumia kisingizio cha mapambano dhidi ya ugaidi imeweka jeshi lake katika Uzbekistan, Tajikistan na Kyrgyzstan ili kujipenyeza kijeshi na kiuchumi, na kuiweka Asia ya kati katika eneo la taathira yake na kupunguza nafasi ya kimkakati ya Russia. Hivyo kwa Marekani kudumisha vituo vyake vya kijeshi katika nchi za Asia ya kati ni muhimu sana kwa kudumisha athari zake katika sehemu hiyo na kuimarisha mpango wake wa kijeshi katika dunia nzima.

Katika mwezi May mwaka huu, rais Karimov wa Uzbekistan alizima jaribio la uasi wa kijeshi ulioungwa mkono na nchi za nje kwa kutumia nguvu za kijeshi, ambapo Marekani ilishutumu kitendo hicho. Baada ya hapo serikali ya Uzbekistan iliweka vizuizi vipya kwa Marekani kutumia kituo chake cha kijeshi cha Karshi-Khanabad. Tarehe 5 mwezi huu, nchi wanachama wa jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai zilitoa azimio la wakuu wa nchi likisema kuwa vitendo vya kijeshi vya kupambana na magaidi wa Afghanistan vimemalizika kwa muda, hivyo inatakiwa kuthibitisha kuwa muuganowa kimataifa wa kupambana na ugaidi utumie kwa muda miundo-mbinu na njia za uchukuzi za safari za ndege za nchi wanachama wa jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai na kuweka kikomo cha kukaa kwa majeshi ya nchi za nje katika nchi hizo". Kutokana na kukabiliwa na wito wa jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai, mwenyekiti wa mkutano wa pamoja wa wakuu wa majeshi ya Marekani Bw. Richard B. Myers hivi karibuni alisema kuwa usalama na utulivu wa sehemu ya Asia ya kati ni muhimu sana. Marekani inaweza kuipa sehemu ya Asia ya kati vitu vingi, mtu anayeweza kuleta usalama na utulivu angekaribishwa.

Rais mteule wa Kyrgyzstan Bw. Kurmanbek Bakiyev ingawa hivi karibuni alieleza mara kadhaa mashaka yake kuhusu haja ya jeshi la Marekani kuendelea kutumia kituo chake kilichoko katika nchi hiyo, lakini katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 11 mwezi huu baada ya yeye kuchaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo, alisema kuwa uhusiano kati ya Kyrgyzstan na Marekani hauko tu katika suala la kuendelea kuweko au la kwa kituo cha jeshi la Marekani. Hivyo wachambuzi wengine wanaona kuwa waziri wa ulinzi wa Marekani huenda amechagua nafasi ya kushika madaraka kwa serikali mpya ya Kyrgyzstan katika mapinduzi ya rangi akitaka kupata mafanikio katika ziara yake kwenye Asia ya kati. Tarehe 25 akiwa njiani kwenda Kyrgyzstan Bw. Rumsfeld aliwaambia waandishi wa habari kuwa Marekani ina uhusiano mzuri na nchi za Asia ya kati. Anatarajia kujadili suala la Jeshi la Marekani kuendelea kutumia kituo cha Zkarshi-Khanabad wakati atakapokuwa na mazungumzo na rais Bakiyev.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-26