Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Tony Blair tarehe 26 alikutana kwa dharura na viongozi wa vyama visivyo tawala vya wahafidhina pamoja na uhuru na demokrasia, kujadili namna kukabiliana na hali mpya kuhusu London kukumbwa na mashambulizi ya kigaidi na kubadilishana maoni kuhusu yaliyomo muhimu kwenye sheria mpya ya kupambana na ugaidi. Siku hiyo, kwenye mkutano na waandishi wa habari Tony Blair aliapa kutorudi nyuma katika mapambano dhidi ya ugaidi. Wachambuzi wanaona kuwa hali ya kupambana na ugaidi kwa hivi sasa nchini Uingereza inamsaidia Blair atoe sheria ya kupambana na ugaidi iliyo kali zaidi.
Vyombo vya habari vya Uingereza vilieleza kuwa kiongozi wa chama cha wahafidhina Bw. Michael Howard alieleza kwenye mkutano huo kuwa sheria mpya ya kupambana na ugaidi ingeruhusu kumbukumbu za simu zilizopatikana na idara za upelelezi zitolewe ushahidi mahakamani. Waziri mkuu Blair aliunga mkono kimsingi pendekezo hilo, lakini anaona kuwa inapaswa kusikiliza maoni ya idara za upelelezi. Zaidi ya hayo, viongozi hao walijadili suala la kuahirisha siku 14 za kuwatia nguvuni watuhumiwa magaidi za hivi sasa hadi siku 90. Lakini viongozi hao hawakueleza hadharani misimamo yao na matokeo ya majadiliano.
Baada ya milipuko kutokea mjini London, sheria ya kupambana na ugaidi iliyopitishwa mwezi Machi kwenye bunge la Uingereza imetiliwa mashaka. Vyama vya Uingereza vilitaka kutunga upya haraka iwezekanavyo sheria ya kupambana na ugaidi na vilifikia kikanuni makubaliano kuhusu kutunga sheria mpya ya kupambana na ugaidi. Habari zinasema kuwa yaliyomo kwenye sheria hiyo mpya ni pamoja na kuwa kila mtu anayeshiriki katika shughuli za kigaidi au kuwafanyia mazoezi magaidi ataadhibiwa kisheria na kila mtu anayewatia moyo watu wazushe mlipuko kwa kujiua kwa njia ya kidini, atatiwa nguvuni au kufukuzwa nchini na idara za utekelezaji sheria. Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Bw Charles Clarke alikadiria kuwa sheria hiyo mpya inatazamiwa kuwasilishwa bungeni na kujadiliwa mwezi Oktoba na kujitahidi kutekelezwa mwaka huu.
Baada ya kusikika kwa yaliyomo ya sheria mpya ya kupambana na ugaidi, imesababisha mara moja majibu ya mashirikisho ya Waislam wa Uingereza. Wana wasiwasi kuwa sheria hiyo italenga makundi ya Waislam na kuzidisha uwezekano wa vijana Waislam kufanya shughuli za ugaidi. Kuhusu jambo hilo, inspekta mkuu wa polisi ya London Bw. Ian Blair tarehe 25 alipokutana na viongozi wa mashirikisho ya Waislam alieleza kuwa hatua za kupambana na ugaidi kwa polisi hazifanywi dhidi ya kundi fulani la jamii. Pia aliahidi kuwa polisi watajitahidi kuwalinda Waislam wa Uingereza.
Baada ya kutokea mashambulizi ya ugaidi mjini London, sheria ya kupambana na ugaidi haikuwazuia magaidi wasifanye shughuli hizo, jambo ambalo linavihimiza vyama vitatu vifikie makubaliano kuhusu kurekebisha sheria hiyo. Wachambuzi wanaona kuwa hali hiyo inamsaidia waziri mkuu Blair atunge sheria ya kupambana na ugaidi iliyo kali zaidi. Lakini kama atashindwa kudhibiti kuhakikisha haki za msingi za raia na kuhimiza masikilizano ya jamii, itaibua zaidi migogoro ya jamii.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-27
|