Ofisa wa Afghanistan tarehe 26 alithibitisha kuwa, jeshi la serikali ya Afghanistan na jeshi la Marekani tarehe 25 usiku lilifanya operesheni ya kijeshi katika mkoa wa Uruzgan, kusini mwa Afghanistan kuwaua wanamgambo 50 wa kundi la Taliban, na kuwakamata watuhumiwa wengine 25. Wachambuzi wanaona kuwa, kutokana na kukaribia kwa uchaguzi wa bunge la Afghanistan, mapambano kati ya jeshi la serikali ya Afghanistan na jeshi la Marekani nchini Afghanistan na nguvu za Taliban yatakuwa makali zaidi.
Baada ya uchaguzi mkuu wa Afghanistan uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana, hali ya sehemu ya kusini na kusini mashariki ya Afghanistan iliwahi kutulia kwa muda. Lakini kuanzia mwaka huu, nguvu zilizobaki za Taliban zilirejesha shughuli zao, na kuzusha matukio ya mashambulizi ya kigaidi hapa na pale nchini humo, pia kudai kuvuruga uchaguzi wa bunge. Tarehe 25 mwezi huu, kituo cha televisheni na magazeti ya Afghanistan kwa nyakati mbalimbali yalitangaza na kuchapisha mazungumzo ya kiongozi wa kundi la Taliban Mulla Mohammed Omar. Katika mazungumzo yake, Bw. Omar aliwataka watu wenye silaha wa Taliban waache tofauti zao, kupigana vita kwa pamoja dhidi ya jeshi la Marekani, na kuendelea kususia serikali ya Hamid Karzai. Bw. Omar alisema kuwa, ameongeza idadi ya viongozi kufikia 18 kutoka 10 wa kamati ya Taliban. Zaidi ya hayo, kundi la Taliban pia limeunda kamati ya kijeshi inayoundwa na makamanda 14 katika mikoa ya Kunar, Heratt na Ghazni. Hii ni mara ya kwanza kwa Omar kufanya mazungumzo hadharani tangu vita vya Afghanistan imalizike. Kabla ya miezi mitatu iliyopita, aliwahi kutoa taarifa ya maandishi, kukataa msamaha uliotolewa na rais Karzai.
Katika siku za karibuni, wanamgambo wa Taliban walifanya mashambulizi mara kwa mara dhidi ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan an jeshi la serikali. Takwimu za mwanzo zinaonesha kuwa, tangu mwezi Machi mwaka huu, watu zaidi ya 800 wamekufa katika matukio mbalimbali ya kigaidi, wakiwemo askari 50 wa Marekani.
Ili kuhakikisha uchaguzi wa bunge la Afghanistan unafanyika bila vizuizi, jeshi la serikali ya Afghanistan na jeshi la Marekani limepambana kithabiti na wanamgambo wa Taliban. Mwezi Juni mwaka huu, polisi wa Afghanistan na jeshi la Marekani nchini humo yalifanya msako dhidi ya Taliban katika mkoa wa Kandahar, kusini mwa nchi hiyo, na kuwaua wanamgambo 32 wa Taliban na kuwakamata watuhumiwa 15.
Wachambuzi wanaona kuwa, ingawa jeshi la muungano la Marekani na Afghanistan limeweka mkazo kupambana na wanamgambo wa Taliban, lakini hali ya usalama wa nchini humo bado hairdhiki. Ili kuhakikisha uchaguzi wa baraza la chini la bunge la Afghanistan na mabunge ya mikoa ufanywe bila matatizo, licha ya kupambana na nguvu za Taliban, serikali ya nchi hiyo pia inatakiwa kufanya juhudi kubwa zaidi katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kidipolomasia.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-27
|