Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-27 21:19:40    
Safari ya "Discovery" na mustakabali wake

cri

Chombo kilichobeba satellite ya Marekani kinachojulikana kwa jina la "Discovery", ambacho urushwaji wake uliahirishwa mara kadhaa kutokana na matatizo ya kiufundi, kilirushwa angani kwa mafanikio tarehe 26 . Hicho ni chombo cha kwanza cha aina hiyo kurushwa angani toka ajali ya chombo kingine kama hicho kijulikanancho kwa jina la "Columbia" itokee. Mbali na vigeregere na kushangiliwa na wafanyakazi wa idara ya safari za vyombo vya anga ya juu na watu wa kawaida, watu wana wasiwasi kidogo kuhusu usalama wa chombo hicho, kwani chombo hicho kimetumika kwa miaka mingi. Hivyo kukagua hali ya usalama wake na kuongeza imani ya watu kuhusu safari za anga ya juu ni majukumu mawili ya "Discovery".

Hata katika mwezi Aprili mwaka huu idara ya safari za anga ya juu ya Marekani iligundua kasoro ya chombo cha kuchunguza hali ya nishati katika tanki lililowekwa nje ya ndege, hali ambayo inafanya marubani kutoweza kujua kiasi cha nishati iliyomo ndani tanki. Tarehe 13 mwezi Julai katika saa mbili na kidogo kabla ndege hiyo kurushwa angani, kasoro hiyo ilitokea tena, wahandisi waliona kuwa ukarabati huo unahitaji muda, hivyo waliamua kubatilisha mpango wa urushaji wa siku ile. Tarehe 17 mpango wa urushaji uliahirishwa kwa mara nyingine tena. Kwa bahati nzuri, ingawa wahandisi hadi hivi sasa bado hawajafahamu sababu zilizofanya chombo cha kuchunguzia hali ya nishati kutofanya kazi vizuri, lakini baada ya kuweka upya waya za kuunganisha zana husika na kupima kwa chombo cha elektroniki, hali ya chombo hicho cha nishati inafanya kazi barabara, hivyo chombo cha "Discovery" kiliingia kwenye njia iliyotarajiwa bila tatizo lolote muda mfupi baada ya kurushwa angani.

Vyombo vya kubeba satellite vya Marekani vilitengenezwa katika miaka ya 70 ya karne iliyopita. Watu wamekuwa na wasiwasi kuwa uchakavu wa vyombo hivyo unaweza kusababisha ajali kama ya chombo cha "Colombia". Hivyo idara ya safari za anga ya juu ya Marekani ilitenga fedha nyingi kufanya marekebisho ya vyombo vya aina hiyo kikiwemo "Discovery".

Hata hivyo, usalama wa "Discovery" bado unafuatiliwa na watu wengi na idara ya safari za anga ya juu ya Marekani. Kwa kuwa "Discovery" ni alama ya kurejea kwenye anga ya juu kwa Marekani. Baadhi ya watu wa Marekani wana mashaka kuhusu usalama wa vyombo hivyo, baadhi ya jumuiya na mashirika yanakosoa mpango wa vyombo hivyo. Shirika la fedha la safari za anga ya juu la Marekani linasema kuwa urushaji wa vyombo vya kubeba satellite ni kupoteza fedha watu wanaolipa kodi nchini Marekani. Katika miaka 15 iliyopita shirika hilo lilisimama kidete na kuukosoa mradi wa kubeba satellite kutumia fedha na nguvu kazi nyingi na kuzuia maendeleo ya mpango wa safari za anga ya juu.

Kutokana na mpango uliotolewa na serikali ya Bush vyombo vyote vya kubeba satellite havitatumika tena kabla ya mwaka 2010 na kuanza kutumika vyombo vya aina mpya, na mpango wa utafiti kwenye anga ya juu utahusu kurejea tena kwenye mwezi, kufanya utafiti kwenye sayari ya Mars kwa kutumia chombo chenye binadamu. Endapo chombo cha"Discovery" kitaweza kurushwa angani na kurejea duniani bila matatizo, basi Marekani itafanya utafiti wa kutengeneza chombo kipya cha aina hiyo na kuendelea na utafiti kwenye anga ya juu iliyoko nje ya dunia; Ikiwa chombo cha "Discovery" kitashindwa, basi imani ya watu kwa vyombo hivyo itapata pigo kubwa, na mipango mingine ya idara ya safari za anga ya juu ya Marekani itakwama.

Inakisiwa kuwa ili kujenga vituo vya kimataifa kwenye anga ya juu, Marekani itahitaji kurusha vyombo vya aina hiyo mara 12 au zaidi ili kupeleka vipuri na kuondoa takataka kwenye vituo vya kimataifa vilivyojengwa kwenye anga ya juu, shughuli ambazo zitakuwa mzigo mkubwa kwa bajeti ya idara ya safari za anga ya juu ya Marekani. Kiongozi wa idara ya safari za anga ya juu ya Marekani Bw. Michael Griffin amesema kuwa wanatakiwa kupunguza zaidi safari za vyombo vya kubeba satellite, ikiwezekana ziondolewe mapema zaidi kuliko mpango uliopangwa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-27