Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-28 17:22:20    
Marekani yataka kubwaga mzigo wa kulinda usalama wa Iraq

cri

Waziri wa ulinzi wa Marekani Bwana Donald Rumsfeld tarehe 27 aliizuru Iraq kwa ghafla, na kufanya mazungumzo na viongozi wa Iraq kuhusu Marekani kuikabidhi Iraq jukumu la kulinda usalama nchini humo na kuondoa jeshi lake kutoka Iraq.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, Bw. Rumsfeld alisema kuwa, sasa umewadia wakati wa kuzingatia kulikabidhi jeshi la usalama la Iraq jukumu la kulinda usalama. Lakini alisema kuwa, hivi sasa Marekani bado haijatunga ratiba halisi ya kuondoa jeshi lake. Lakini alitumai kuwa, jeshi la Marekani litaondoka Iraq mapema iwezekanavyo. Siku hiyo, mkuu wa jeshi la Marekani nchini Iraq Bwana George Casey pia aliainisha huko Baghdad kuwa, huenda Marekani itaanza kuondoa jeshi lake kutoka Iraq katika majira ya chipuko mwaka kesho. Hii ni mara ya kwanza kwa maofisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani kuzungumzia kikomo cha kuondoa jeshi tangu hali ya usalama ya Iraq izidi kuwa ya wasiwasi mwezi Aprili mwaka huu.

Sababu hasa kwa Marekani kuondoa jeshi lake kutoka Iraq ni kama zifuatazo: Kwanza, serikali ya Iraq na watu wake wanatumai kuwa, jeshi la Marekani litaondoka nchini humo haraka iwezekanavyo, ili kutuliza shughuli za kimabavu zinazotokea mara kwa mara. Kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Iraq kumekuwa kisingizio cha wanamgambo wanaoipinga Marekani kufanya mashambulizi mara kwa mara. Bw. Rumsfeld tarehe 27 alikiri huko Baghdad kuwa, kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Iraq hakuwezi kuhakikisha usalama wa watu wa Iraq.

Pili, jeshi la Marekani nchini Iraq limekumbwa na vifo na majeruhi wengi, serikali ya Bush inapaswa kuzingatia suala la kuondoa jeshi lake kutoka Iraq ili kupunguza shinikizo nchini Marekani. Takwimu zinaonesha kuwa, tangu vita vya Iraq vitokee mwaka 2003, idadi ya askari wa Marekani waliokufa nchini Iraq imefikia 1782. Uchunguzi mwingine umeonesha kuwa, asilimia 58 ya watu wa Marekani wanaona kuwa, Marekani haiwezi kupata ushindi wa vita vya Iraq, na haiwezi kujenga nchi ya kidemokrasia ya Iraq.

Wachambuzi wameainisha kuwa, kiasi cha askari wa jeshi la Marekani kuondoka kutoka Iraq na ratiba yake bado inazuiliwa na sababu mbalimbali. Ya kwanza, kama Bw. Casey alivyosema kuwa, jeshi la Marekani linapaswa kuondoka kutoka Iraq hatua kwa hatua kutokana na mchakato wa kisiasa wa nchini humo. Pili, Waziri mkuu wa Iraq Bw. Ibrahim al-Jaafari aliainisha kuwa, kuondoka kwa jeshi la Marekani kunahusiana na uwezo wa jeshi la usalama la Iraq, ambalo hivi sasa bado haliwezi kushinda kazi ya kulinda usalama katika muda mfupi. Tatu, jeshi la Marekani na serikali ya mpito ya Iraq bado hazijatunga mpango halisi kuhusu kukabidhi jukumu la kulinda usalama, zinatakiwa kuimarisha mashauriano na kuzidisha ushirikiano kati yao.

Kwa hivyo, Marekani inapaswa kuondoa jeshi lake kutoka Iraq, lakini bado haijulikani kama inaweza kubwaga mzigo wa kulinda usalama wa Iraq katika muda mfupi.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-28