Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-28 17:33:57    
Michezo ya sanaa ya watoto mjini Guiyang

cri

Katika miaka ya karibuni, Guiyang, mji mkuu wa mkoa wa Guizhou, kusini magharibi mwa China unafuatilia sana mafunzo na maendeleo ya michezo ya sanaa za watoto, na ngoma zilizochezwa na watoto wa mji huo zenye umaalum wa kikabila zinapendwa sana nchini China na ng'ambo.

Mwezi Juni mwaka huu, mwandishi wetu wa habari alipokitembelea kikundi cha sanaa cha Xiaohua cha Guiyang, alimkuta msichana Yu Yuzhu akisema kuwa, maonesho ya kikundi chao yanakaribishwa sana, na wamekwenda kwenye miji mingi nchini China na ng'ambo kufanya maonesho ya michezo ya sanaa. Anasema:

"Sisi tunafanya maonesho katika sehemu nyingi, tunaimba nyimbo na kucheza ngoma, tunaona furaha kubwa. Safari hii nitakwenda Hong Kong kushiriki kwenye mashindano ya michezo ya sanaa. Tumepata tuzo nyingi za kimataifa, pamoja na nafasi ya tatu ya mashindano ya kwaya ya dunia ya Olimpiki."

Mji wa Guiyang una vikundi vingi vya michezo ya sanaa ya watoto. Watoto wa vikundi hivyo wamewahi kufanya maonesho ya michezo ya sanaa katika vijiji vya kabila la wamiao, ukumbi wa muziki wa Beijing, hadi nchini Marekani, Ujerumani, Italia na nyinginezo. Waliwahi kushiriki katika mashindano mengi ya michezo ya sanaa ya kimataifa na kupata tuzo nyingi.

Mstaafu Yang Kailiang alikuwa mtungaji na mwongozaji wa ngoma, ngoma nyingi za watoto alizozitunga zimepata tuzo nyingi nchini China na nchi za nje. Anasema:

"Tumeamua kuzifanya ngoma za watoto za Mji wa Guiyang ziwe na mtindo maalum wa kikabila, kuonesha maisha ya watoto wa makabila madogo madogo, hivyo zinakaribishwa sana duniani."

Guiyang ni mji wenye makabila mengi, ambayo ni pamoja na kabila la wamiao, kabila la watujia na kabila la watong. Mji huo unapoendeleza michezo ya sanaa ya watoto, pia unatukuza umaalum wake wa kikabila. Kwa mfano, ngoma iitwayo "sketi ya rangi" inaelezea kuwa, wakati wa kusherehekea sikukuu, wasichana kadhaa wa kabila la wamiao wanacheza ngoma wakivaa sketi zilizotengenezwa kwa kitambaa cha maua. Wanacheza ngoma wakifuata midundo ya ngoma ya shaba, na milio ya filimbi ya Lusheng. Ngoma hiyo imeonesha mtindo pekee wa kikabila. Katika ngoma hiyo, msichana mwenye sketi ya rangi anampatia sketi msichana asiyekuwa na sketi ya rangi, na kumwalika kucheza ngoma pamoja naye. Hadithi hii inaonesha wazo kuwa, ukimpatia mwingine furaha wewe mwenyewe utaona furaha kubwa zaidi.

Mji wa Guiyang ulianza kuendesha shughuli za kuwaelimisha watoto michezo ya sanaa kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita. Mwalimu msanii alitangulia kuanzisha kikundi cha michezo ya sanaa ya watoto, na serikali ya mji huo imechukua hatua nyingi kuhimiza maendeleo ya michezo ya sanaa ya watoto.

Mhusika wa idara ya utamaduni ya mji wa Guiyang Bwana Deng Chiyong anasema:

"Tunashughulikia michezo ya sanaa ya watoto kwa kufuata ujenzi wa miundombinu, kuwaandaa wachezaji watoto na kubuni kazi mpya za michezo ya sanaa. Guiyang ni mji wenye makabila mengi, hivyo wakati wa kubuni michezo ya sanaa ya watoto tunazingatia zaidi vitu vyenye umaalum wa kikabila, kwani umaalum huleta uhai."

Mwandishi wa habari alifahamishwa kuwa, majumba ya watoto na vikundi vya michezo ya sanaa vya Guiyang hutoa mafunzo ya michezo ya sanaa au kufanya maonesho ya michezo ya sanaa baada ya watoto kumaliza masomo yao shuleni, hivyo hawawezi kuathiri masomo yao. Watoto wanapoingia katika vikundi vya michezo ya sanaa, walimu au wazazi wao huwathibitishia kozi ya michezo ya sanaa inayowafaa, ili waweze kudumisha nia ya kujifunza.

Usitawi wa michezo ya sanaa ya watoto mjini Guiyang umeufanya mji huo uwe chanzo cha kuwaandaa wachezaji wasanii, ambao wengi wao wameingia katika chuo kikuu cha muziki cha China, chuo kikuu cha muziki cha Shanghai, na chuo kikuu cha ngoma cha Beijing, baadhi yao wamekuwa maarufu katika jukwaa la ngoma na muziki nchini China.

Ngoma zilizochezwa na watoto wa vikundi vya michezo ya sanaa vya Guiyang huoneshwa kwenye vituo vya televisheni vya taifa na mikoa na huwaburudisha watoto milioni 360 nchini China.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-28