Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-28 22:37:28    
Siku kuu ya Mwaka mpya wa jadi wa kichina

cri

Sikukuu ya Mwaka mpya wa jadi wa kichina ni sikukuu kubwa kabisa kwa Wachina katika mwaka mzima ambayo ni kama sikukuu ya Krismasi katika nchi za Magharibi. Ingawa namna ya kusherehekea sikukuu hiyo inabadilika badilika kutokana na jinsi muda unavyokwenda, lakini nafasi muhimu ya sikukuu hiyo katika maisha ya Wachina haitabadilika kabisa. Yafuatano ni maelezo kuhusu sikukuu hiyo.

Inasemekana kuwa hadi sasa Sikukuu ya Mwaka mpya wa jadi wa kichina imekuwa ikiadhimishwa kwa miaka elfu nne nchini China, lakini mwanzoni sikukuu hiyo haikuitwa sikukuu ya Spring na wala haikuwa na tarehe maalumu. Hadi miaka elfu mbili na mia moja iliyopita wahenga wa China walihesabu mwaka kwa mzunguko kamili wa sayari ya Jupita, sikukuu hiyo iliitwa sikukuu ya Jupita, ilipofika miaka elfu moja iliyopita ndipo Wachina walipoanza kuiita siku hiyo sikukuu ya Spring.

Kutokana na desturi ya Wachina sikukuu hiyo inaanzia tarehe 23 mwezi wa 12 kwa kalenda ya Kichina hadi tarehe 15 mwezi wa Januari yaani kuwadia kwa sikukuu ya taa, ambapo ni jumla ya wiki tatu. Katika siku hizo za mwaka mpya, siku ya mwisho yaani tarehe 30 ya mkesha wa sikukuu na siku ya kwanza ya Januari ni siku za sherehe, au kwa maneno mengine siku hizi mbili ni kilele cha sikukuu ya Spring.

Ili kusherehekea sikukuu ya Spring, kuanzia mijini hadi vijijini watu huwa katika pilikapilika za matayarisho. Huko vijijini wakulima hufanya usafi wa nyumba, kufua nguo, kubandika mlangoni karatasi pacha zenye maandishi ya baraka na kubandika picha maalumu za mwaka mpya vyumbani, huku wakitayarisha mahitaji ya mwaka mpya kwa kununua keki, peremende, nyama, vinywaji na matunda ili kutumia nyumbani na kukaribisha wageni. Katika miji maandalizi ya mwaka mpya yanaanza mapema zaidi, maduka na masoko ya kujihudumia hutayarisha vitu tele. Kutokana na takwimu, Wachina hutumia pesa kiasi cha thethuli moja au pengine hata zaidi ya matumizi yote ya mwaka mzima katika kipindi cha sikukuu ya Spring.

"Kukesha usiku" wa kuamkia sikukuu ya Spring ni desturi ya Wachina, kwa kawaida katika usiku huo jamaa hukusanyika pamoja kwenye chakula, hali ambayo inaonekana kote iwe ni sehemu ya kaskazini au kusini ya China. Jamaa hula chakula kwa pamoja, na baada ya chakula huburudika hadi mapambazuko. Katika usiku huo wazee huwazawadia watoto pesa kama ishara ya baraka kwa mwaka unaokuja. Katika miaka kadhaa iliyopita watu walisherehekea sikukuu hiyo kwa kuwasha fataki ikimaanisha kuwafukuza mashetani, lakini kutokana na usalama na uchafuzi wa mazingira desturi hiyo imepigwa marufuku katikati ya miji mikubwa.

Wakati wa sikukuu halisi yaani siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza watu huvalia rasmi wakisubiri kutembelewa na wageni au kutoka kwenda kuwatembelea jamaa na marafiki. Wanapokutana huamkiana "Heri ya Mwaka Mpya", au "Heri ya Sikukuu ya Spring" na kuwakaribisha ndani kwa peremende, chai na vitafunwa na kuzungumzia maisha yao ya kila siku. Kama majirani walikuwa na mkwaruzano katika mwaka uliopita, wanapaswa kuondoa kinyongo na kutembeleana katika sikukuu.

Wakati wa sikukuu ya Mwaka mpya wa jadi wa kichina, idara za utamaduni hushirikisha michezo ya sanaa ya aina mbalimbali. Kwa mfano, usiku wa mkesha vituo vya televisheni huonyesha sherehe maalumu ya michezo toka saa mbili za usiku hadi saa saba usiku, ambapo huwepo watazamaji zaidi ya milioni mia moja. Licha ya michezo ya Wachina pia kuna vikundi vya sanaa kutoka nchi nyingine kama Russia, Uingereza na Marekani vikifanya maonesho ya muziki au dansi.

Shamrashamra za sikukuu pia zinafanyika katika bustani, ambapo kwamba kuna magulio, michezo ya mazingaombwe n.k.

Kutokana na mabadiliko ya maisha, watu wameanza kutumia simu za waya, simu za mkononi, na hata mtandao wa kompyuta kupelekeana salamu.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-28